Na Waandishi Wetu
CHAMA cha Wanasheria cha Tanzania Bara (TLS), kimemuomba Rais Jakaya Kikwete kuondoa hati ya dharura iliyoambatanishwa kwenye muswada wa
katiba uliowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita na badala yake utafutwe utaratibu wa kawaida ili wabunge na umma wote upate fursa ya kutosha kujadili na kutoa maoni
kuhusu muswada huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Rais wa TLS, Bw. Francis Stolla, chama hicho kitafikisha ujumbe huo kwa Rais Kikwete pamoja na mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kutunga kwa Katiba Mpya.
Bw. Stolla alisema TLS katika mapendekezo yake kuhusu muswada huo ni kuwa wa lugha ya Kiswahili ili kuzingatia haki ya kila mtu kupata nakala inayoeleweka.
"TLS imejizatiti kwa dhati kuimarisha na kuendeleza
utawala wa sheria nchini Tanzania, kwa kujua kwamba sheria inapozingatiwa ipasavyo, utawala wa sheria huwalinda wananchi dhidi ya matumizi ya kibabe ya mamlaka ya serikali, "alisema Bw. Stolla.
Alisema mbali ya kutoa msaada wa kitaalamu kitatoa mapendekezo stahiki kwa Halmashauri yao, umma na vyombo vinavyohusika na mchakato wa kutunga Katiba pia kuishauri Serikali kujifunza uzoefu kutoka nchi nyingine kama vile Kenya na Uganda.
Alisema pia TLS inashauri jina la muswada liitwe Muswada wa Kutunga Katiba Mpya ya mwaka 2011 ili kuonesha dhahiri nia ya wananchi kuwa wanataka katiba mpya, siyo marekebisho na kupendekeza tamko la awali lirekebishwe na lioneshe wazi
madhumuni ya muswada wa Sheria itakayoweka mfumo wa kutunga na kuweka Katiba mpya inayokidhi vigezo vinavyokubalika kimataifa vya demokrasia na utawala bora.
"Ukomo wa Katiba na utungaji wa rasimu ya Katiba mpya,TLS kinatoa tahadhari kwamba katiba ya sasa haisemi lolote kuhusu ukomo wa katiba na utungaji wa katiba mpya, kwa mujibu wa Ibara ya 98 ni utaratibu pekee unaotajwa wa kufanya marekebisho, kutokuwepo kwa vipengele vya suala hili kutafanya michakato yoyote ya kuunda katiba mpya kuwa batili," ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa.
"Kuhusu kifungu cha 6 cha Muswada uteuzi wa wajumbe wa tume TLS kinatoa maoni na mapendekezo ya kuwa tume iwe na uwakilishi wa Tanzania Bara na Visiwani kwa idadi sawa, kuwe na uwiano stahiki unaozingatia sura halisi ya mambo,".
Pia imependekezwa kuwa tume iwe na jopo la wataalamu watakaoteuliwa kutoka mchanganyiko wa kada za taaluma, mashirika na jumuiya mbalimbali kwa kuzingatia jinsia, dini na ngazi za utaalamu na hadidu ziandikwe na chombo huru na ziidhinishwe na Bunge la Tanzania, badala ya Rais.
Maoni ya wananchi yazingatiwe
Mtandao wa Haki za Binadamu (SAHRiNGON) umeitaka Serikali kuzingatie maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau mbalimbali kuhusu muswada wa sheria ya kutunga katiba mpya ya Tanzania na kwamba mijadala yote ya katiba lazima iwe wazi kwa kila mtu, ipewe muda wa kutosha na si kitu cha dharura kwani kwa kufanya hivyo nchi itakuwa hatarini.
Hayo yalisemwa na Bodi ya wakurugenzi ya mtandao huo katika taarifa yao iliyosainiwa na Mratibu wa mtandao huo Taifa, Bi. Martina Kabisama na kusambazwa kwa vyombo vya habari jana.
Bodi hiyo kwa makubaliano ya pamoja ilitoa rai kwa Serikali kwamba iwachukulie hatua kali wote waliowarubuni watoto na kuwanyima haki yao ya uhuru wa maoni na kuwatumia kama vibaraka kwenye mjadala wa katina uliofanyika Dar es Salaam.
Ilisema pia watoto na wanafunzi wasirubuniwe na kutumiwa na watu wachache wenye kupotosha ukweli na kushambulia raia wenzetu wanaotumia haki yao ya kikatiba kutoa maoni yao kwa ajili ya maslahi ya taifa.
"Pamoja na jitahada zote za Serikali, Mtandao wa Haki za Binadamu – SAHRiNGON tumestushwa na tunasikitishwa sana kwa sheria hii muhimu ya mstakabali wa nchi ambapo inaonekana imewekwa makusudi ili wananchi wasijue na hatimaye washindwe kuchangia kutokana ukweli kwamba mifumo yetu ya upashanakji habari ni duni," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Muswada hauna manufaa
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Chris Maina amesema muswada huo hauna msaada kwa Watanzania na hauwasaidii kwa sababu hauna utaratibu unaoonesha lini utawapatia katiba mpya.
Pia amesema watu waliohusika kutengeneza muswada huo hawakuwa na nia ya kuleta katiba mpya bali kubadilisha iliyopo.
Akizungumza katika mdajala wa kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya Mwaka 2010 ulioandaliwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya TADIP, Profesa Maina alisema uhitaji wa Watanzania siyo kubadilisha katiba iliyopo ambayo ina mapungufu, bali kupata mpya.
Alisema kuwa sasa hivi ni mara ya 14 tangu katiba ianze kubadilishwa lakini bado ina mapengo na mapungufu mengi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi.
Alisema kutokana na hali hiyo kuna umuhimu wa kuunda tume ambayo itasimamia suala la katiba na siyo Tume ya Uchaguzi ambayo Watanzania waliowengi hawana imani nayo.
"Ukweli ni kwamba Watanzania hawana imani na Tume ya Uchaguzi ambayo ilionesha mapungufu makubwa katika uchaguzi mkuu," alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Maina, Watanzania wanapigia kelele suala la katiba ili iweze kutengenezwa iliyo bora na itakayokidhi mahitaji ya wananchi wote bila ubaguzi.
"Pamoja na itikadi kali za kisiasa badala ya sheria Watanzania wajitokeze kwa wingi kulizungumzia suala ili ambalo ni letu wote," alisema.
Pia alisisitiza ushiriki wa makundi yote ya jamii katika mchakato mzima wa katiba nzima.
Alisistiza kuwa hakuna haja ya serikali kuharakisha ili kupata katiba mpya wakati asilimia kubwa ya Watanzania hawajuhi nini maana ya katiba, kilichopo kwenye ya zamani badala yake elimu ya uraia itolewe nchi nzima.
Aliongeza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu nao waelimishwe ili waweze kutoa msaada kwa wanajamii ambao hawajui kitu kuhusu katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Maendeleo (CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa alisema ushabiki wa vyama vya siasa ambao umeingizwa katika mchakato wa kutengeneza katiba mpya utasababisha matatizo makubwa.
Pia alisema ibara ya 98 iliyopo kwenye katiba iliyopo iondolewe kwa sababu haiwapi fursa wananchi kuonesha ushiriki wao.
Alisema Watanzania wengi hawana uelewa wa mchakato wa kuandaa katiba mpya kwa sababu iliyopo hawajaipitia.
Alisisitiza kuwa suala la kupata katiba mpya siyo rahisi kama ambavyo serikali inalichukulia.
Wanafunzi wa vyuo vikuu nao walitoa mwito kwa serikali kuwaachia Watanzania nafasi ili watoe maoni kuhusu nini wanataka kiwepo kwenye katiba mpya kabla muswada haujapitishwa.
Mkurugenzi wa TADIP Bw.Steven Mmogo alisema baadhi ya maudhui ya muswada unaojadiliwa umewatia wasiwasi wadau mbalimbali na hauonesha jinsi ilivyo vigumu kupata katiba mpya inayotokana na wananchi kupitia muswada huo.
Imeandikwa na Peter Mwenda, Kulwa Mzee na Agnes Mwaijega
Wizara inayoshughulikia maswala ya katiba inachelesha mambo yenyewe;
ReplyDelete1: Je , haikutambua kama muswada ulitakiwa kuandikwa kwa lugha ya kueleweka ( Kiswahili )na wengi ( Watanzania ) .
2. Kuweka vipingele wanavyojua wazi kuwa vitakuwa vigumu lupitishwa na Watanzania.
Tuache mdhaha katika mambo ya muhumu na yanayo husu maisha ya watanzania kwa muda wa nusu karne.
Mcha