25 April 2011

Chuji, Shamte ngoma nzito Yanga

Na Zahoro Mlanzi

WAKATI pilikapilika za usajili zikiendelea, Klabu ya Yanga, inawafikiria upya kuwaongezea mikataba wachezaji Athuman Idd 'Chuji' na Shamte Ally kwa ajili ya
msimu ujao wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Mbali na hilo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwao Uganda, juzi alionekana uwanjani akisaka wachezaji wakati timu ya Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) ikiumana Harua.

Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuanzia Juni 20 mwaka huu mpaka Julai 20, ndicho kipindi rasmi cha kufanya usajili huku klabu zikitakiwa kutangaza wachezaji itakaowaacha.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwesigwa Celestine alisema wachezaji hao pekee ndio waliomaliza mikataba yao na wanatarajiwa kwenda kujadiliwa ndani ya wiki hii.

"Chuji na Shamte walishamaliza mikataba yao, lakini Kamati ya Utendaji na ya Usajili imekuwa ikikutana mara kwa mara kujadili masuala hayo na mengine, nadhani wiki ijayo tutajua hatma ya wachezaji hao," alisema Celestine.

Alisema katika kipindi hiki cha usajili mambo mengi yanazungumzwa juu ya wachezaji hao lakini kila kitu kitakuwa wazi baada ya kamati ya usajili kuliweka sawa suala hilo ila kwa wachezaji wa kigeni watabaki na kipa Yaw Berko na Davies Mwape.

Wakati huohuo, Celestine alizungumzia suala la Timbe baada ya kuulizwa kwamba alionekana katika mchezo kati ya URA na Harua na kuna taarifa kwamba anamsaka beki mmoja wa URA, alikiri kuwepo kwa Timbe katika mchezo huo.

Alisema aliongea naye kwa simu juzi na alimwambia kwamba yupo uwanjani akishuhudia mchezo huo lakini suala la kuwepo uwanjani hapo kusaka wachezaji alidai halitambui.

Alisema kocha huyo anatarajiwa kurudi nchini Juni 15, mwaka huu ikiwa ni siku tano kabla ya pazia la usajili halijaanza ili aje kuweka mambo sawa.

No comments:

Post a Comment