MILAN, Italia
TIMU ya AC Milan imejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia, Serie A baada ya kuwatandika Inter Milan kwa mabao 3-0 na kuongeza
pengo la pointi tano dhidi ya mahasimu wao.
Katika mechi hiyo ya juzi, mchezaji Alexandre Pato ndiye aliifungia timu yake mabao mawili huku beki, Cristian Chivu akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumwangusha Mbrazil huyo mapema kipindi cha pili.
Pato alipachika bao lake dakika za kwanza za mchezo huo kabla ya kupachika la pili, muda mfupi baada ya Inter Milan kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Bao la tatu na la ushindi lilifungwa na Antonio Cassano kwa mkwaju wa penalti, ikiwa imesalia dakika moja mpira umalizike.
“Tulibaki kuwa watulivu na kucheza soka,” alisema Allegri. “Hatukuwaachia Inter wapate nafasi nyingi za kufunga na kwa upande wetu pia tulipata nafasi nyingi," aliongeza mchezaji huyo.
Timu zote mbili zimebakiza mechi saba na Inter Milan, huenda ikapitwa na Napoli kama itakuwa imeshinda mechi yake ya jana dhidi ya Lazio.
“Sidhani kama mchuano umemalizika, lakini pointi tano ni pointi tano ambazo ni nyingi,” alisema kocha wa Inter Leonardo. “Kwa ujumla bao la mapema liliathiri mno mechi na liliwapa AC Milan kujiamini. Endapo tungeweza kusawazisha kabla ya kwenda mapumziko tungeweza kubadili mechi," aliongeza.
No comments:
Post a Comment