01 April 2011

Malumbano yazidi kuipasua CCM

*Jumba bovu lamwangukia Kapteni Chiligati

Na Mwandishi Wetu

MOSHI unazidi kufuka ndani ya chama tawala CCM kufuatia migongano ya kauli kutoka makundi na makada mbalimbali ndani ya chama hicho.Katika siku za
karibuni, chama hicho kikongwe nchini kimejikuta kikigubikwa na malumbano ya wao kwa wao huku baadhi ya vijana wake wa UVCCM, wakimng'ang'ania kooni Waziri mkuu mstaafu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Bw. Fredereck Sumaye kwa kilichodaiwa, masimamo wake kukosoa chama nje ya vikao.

Machi 5, mwaka huu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Kapteni mstaafu John Chiligati, alikaririwa na vyombo vya habari akiitaka dola idhibiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kile kilichoelezwa, kuendesha nyendo zenye agenda ya siri ya kuing'oa madarakani CCM kwa kutumia nguvu kinyume cha katiba.

Bw. Chiligati alisema tangu CHADEMA walipoanza ziara zao mikoa ya Kanda ya Ziwa, viongozi wa chama hicho walikuwa wakitoa kauli za kuupotosha umma, zenye kuchochea uasi na machafuko.

"Wanachochea wananchi wakisema 'peoples power!' (nguvu ya umma). Je, mpo tayari kufanya kama Tunisia na Misri?" alikaririwa akisema, Bw. Chiligati.

Aliongeza, "CCM inaviomba vyombo vya dola viwe imara kuchukua hatua za kisheria...wanachofanya CHADEMA ni kutuchonganisha na wananchi kutoa kauli hatari za kujaribu kughilibu akili za watu ili kuchochea, machafuko, umwagaji damu na uasi".

Hata hivyo, alisema CCM haipingi kukosolewa kwani hiyo ni kazi ya vyama vya upinzani na baada ya uchaguzi, walitegemea CHADEMA kutumia wabunge wake 48 bungeni kuweka bayana kasoro za serikali ya chama hicho tawala ili zirekebishwe.

Siku moja baada ya kauli hiyo, Bw. Sumaye alikaririwa akiishauri CCM kukabiliana na CHADEMA kisiasa badala ya kuitaka serikali ipambane nao kwa kutumia dola.

Gazeti moja la kila siku (si Majira) lilimkariri Bw. Sumaye, akisema kazi ya siasa ni ya chama, si serikali hivyo CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na CHADEMA kwa sera na kujibu hoja zao zote ili kuongeza imani ya wananchi kwa chama hicho.

Bw. Sumaye alisema si ishara njema kwa CCM kukaa kimya wakati wapinzani wanaendelea kukishitaki kwa wananchi kuwa kimeshindwa kufanya kazi.

Kauli hiyo ilifungua uwanja wa malumbano makali kati ya Bw. Sumaye na baadhi ya makada wenzake wa chama hicho, huku UVCCM wakimshambulia kwa madai ya kukiuka taratibu za chama katika kutoa madukuduku yake. 

Akizungumza na Majira jana katika mahojiano maalum, mmoja wa makada wakongwe wa chama hicho aliyewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alieleza kusikitishwa kwake na mashambulizi dhidi na wastaafu wenzake na hali halisi ilivyo ndani ya chama hicho.

Kada huyo, aliyeomba kutoandikwa jina gazetini kwa hofu ya kuibua malumbano zaidi kutokana na nafasi yake, aliliambia Majira kuwa kauli ya Sumaye haikuwa na madhara kwa chama hicho kama inavyodaiwa,ilipaswa kufanyiwa kazi na si kulaumiwa.

Alisema haoni sababu ushauri wa Bw. Sumaye kusakamwa na kufafanua kuwa kauli ya Bw. Chiligati kutaka dola idhibiti CHADEMA hadharani, ndiyo potofu.

"Tunakosea kumsakama Sumaye anaposema CCM ijibu hoja za CHADEMA si kuiambia dola iwadhibiti. Tatizo liko wapi hapa? Kweli hili linahitaji vikao au mtu akanong'onezwe sikioni?  Lile la Chiligati kutamka hadharani kuomba dola iwadhibiti CHADEMA ndilo lenye tatizo. Lilipaswa kuzungumzwa na kuishia ndani ya vikao vya chama, vinginevyo maagizo yake yatolewe kimyakimya kwa maandishi kama taarifa tu ya tahadhari kwa vyombo vya dola. Kutamka hadharani moja kwa moja ni tishio kwa demokrasia. Mataifa mengine yatatushangaa chama makini kama CCM kutoa kauli ya rejareja."

"Mfano juzi juzi Waziri Mkuu Pinda (Mizengo) akiwa Kagera, alimtaka Magufuli (John, Waziri wa Ujenzi) kupunguza kasi ya bomoabomoa, alitamka hilo hadharani. Ikafuata kauli kama hiyo ya Rais Kikwete akimtaka apunguze ubabe kwenye utekelezaji wa zoezi hilo, naye alimwambia hili hadharani alipotembelea Wizara ya Ujenzi. Magufuli hakuwa na makosa alikuwa anatekeleza sheria. Lakini pamoja na kusemwa hadharani na wengine kuona kaonewa, huo ni ukosoaji wa kawaida wenye nia njema ya kujenga.

"Rais na Waziri Mkuu wake walifanya hivyo wakijua kuna vikao vya Baraza la Mawaziri lakini hawakuwa na sababu kungoja huko kwa kuwa nia yao ilikuwa njema, ililenga maslahi ya wengi, hata wangelisemea wapi,  kadhalika Sumaye nia yake ilikuwa njema kukinusuru chama chake kisizidi kuumbuliwa na CHADEMA hata angesemea wapi, ukweli ungebaki pale pale! Tuchambue mambo kwa fikra yakinifu," alishauri na kuongeza;

"Kusubiri vikao kwa kila jambo haiwezekani, lazima tubadilike. Tunanyonga demokrasia ya wanachama wetu. Kama utajaza maji ya moto kwenye 'themosi', ufunge kwa nguvu halafu uendelee kuyachemsha, nini kitatokea? Chupa itapasuka. Tusifike huko chama kijiumbe upya, kimevamiwa na sasa kinayumba."

"CHADEMA kuimba 'peoples power' wameanza leo? Tangu mwaka 2000 wameimba sana hayo. Leo wakitaja Misri na Tunisia wanamtisha nani? Mazingira na siasa za Misri na Tunisia hayana uhusiano na yetu. Waimbe na kuhubiri hayo yote kama chama chetu kinatekeleza ilani yake vizuri, hakina sababu kulilia fadhila za dola".

Mwanasiasa huyo aliendelea kusema "Kama CHADEMA wataingia mitaani na kutafsiri maneno yao kwa vitendo, hapo dola ichukue nafasi yake kudhibiti, wala haitangoja kuombwa na CCM ni wajibu wake. Amani ni ya Watanzania wote si ya CCM, CHADEMA, TLP, CUF wala vyama vingine."

Kada huyo alilaani hatua ya UVCCM kuendesha malumbano na wastaafu hao na kushauri kuwa walipaswa kujua ni nini walichosema kabla ya kuanza kushambulia hoja zao bila msingi.

"UVCCM walipaswa kwanza wajue nini walichosema wastaafu hao kabla ya kuanzisha malumbano. Inawezekana huo si mtazamo wao. Hii inafanya wengine tujiulize vijana hawa wanatumwa na nani? Kazi yao ndani ya chama si kulumbana na viongozi ndani ya chama chao. Tunakielekeza chama kubaya," alionya.

Jitihada za kumpata, Bw. Chiligati kutoa maoni yake kuhusu hoja hizo hazikuweza kuzaa matunda baada ya kutoa maelezo mafupi kwamba alikuwa Monduli mkoani Arusha kuhudhuria mazishi ya mke wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Parseko Kone.

Ingawa aliahidi kuzungumza na mwandishi jioni baada ya shughuli hiyo, muda huo ulipofika simu yake iliita mara kadhaa bila kupokelewa na baadaye haikupatikana hewani. 

6 comments:

  1. ccm kwa kuendeleza malumbano ni ishara ya kushindwa kisiasa.Ccm inatakiwa kupambana na viongozi wao wanao kichafua chama chao na sio chadema.chadema wanatumia mapungufu ya viongozi hao wa ccm kufanya maandamano kwa wananchi kama viongozi mafisadi,mikataba mibovu inayofanya na viongozi wa ccm kama DOWANS n.k CCM inatakiwa kujipanga na kuwaondoa uwanachama viongozi wazembe
    mwananchi mwenye hasira kali

    ReplyDelete
  2. Hiyo ni kweli kabisa. alichokisema mstafu hoyo ni sahihi.

    Unapotumia dola ikujibie hoza za kisiasa we ni mwanasiasa kweli? CCM acheni hizo, jibuni hoja za siasa kisiasa na si kwa kutumia dola.Watanzania sasa hivi wanauelewa mkubwa hawadanganyiki na vitisho v ya dola.

    By mtanzania wa ukweli.

    ReplyDelete
  3. eng.mwakapango, E,P,AApril 1, 2011 at 8:26 PM

    Bwana sumaye endelea kuwasaidia CCM. watu kama akina shigella hawana ubavu wa kupambana na Sumaye watabaki wamenyoa mapanki hii ndiyo unaweza kumpima mtu Kuwa ana busara kweli? kazi ya umoja wa vijana ni kujibu hoja za upinzani na sio kuingia kwenye malumbano ndani ya CCM. Mimi nadhani vijana wenyewe ndiyo wamejigeuza daraja la kupitisha mafisadi kwa tamaa ya pesa na sio uzalendo na mapenzi kwa chama. acheni wastaafu waseme yaliyomoyoni mwao.

    ReplyDelete
  4. uvccm ndio wanaotufanya sisi vijana tuichukie ccm na wengi wetu kukimbilia chadema kwenye muelekeo wala sio kauli za sumaye wala sitta..

    ReplyDelete
  5. Hapa bwana watu wamesahau kuwa kiti cha mkataba sio cha nyumbni kwako unachoweza kukalia muda wowote unaotaka kukalia n ahakina muda wa kukutosa, ila uongozi ni kama kiti cha mkataba, utakalia ila ukifika muda wa kukiacha utaachana nacho na kurudi kwenu kijijini kulima mihogo au ubaki mjini unapiga umbea kwa kung'ang'ania mambo yaliyokwisha kukukataa kulingana na umri, mfano Mzee Kingunge alitakiwa kuwa pembeni akiona chezo linakwenda vipi ili atoe ushauri, ajabu yeye ndiye kachaguliwa kuwa kamanda wa Uvccm sijui nalo ni jeshi hadi kuwa na makamanda na maluten Kanali? yaani ni vichekesho tupu! ila mie nazidi kuwaombea waendeleze malumbano kwani ndiyo itakuwa nafuu yetu sisi watoto wa Vizee Maskini tusio na uwezo wa kuhimili hata kuwahudumia hao wazazi wetu, ila wao Uvccm wanaonekana wazazi wao wanahali nzuri hadi wanakosa muda wa kufikiri kuwahudumia matokeo yake wanawatusi watu wazima mithili ya wazazi wao tena wako nao chama kimoja. Aahh Eebwanaeeee tumechoka na kelele zao watuletee kitu kingine cha kujadili sio hayo malumbano yao kila siku. Ras David Say's

    ReplyDelete
  6. TATIZO, VIJANA WA CCM nasi tunataka ulaji,maanake wazee wameshakwapua vya kutosha huku wakila kwa mikono miwili...pasi na kutukumbuka,hivyo sasa watuachie.CHILIGATI,hana shule,kwahiyo yeye lolote linalokuwa karibu ndilo hutamka,anafikiri ujeshijeshi tu ukiongeza na shule yakendogo basi unapata jibu halikadhalika Katibu mkuu Yusuf Makamba.

    ReplyDelete