Na Kulwa Mzee
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi (RPC) mkoani Rukwa, Bw. Abdallah Zombe amefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania akiidai Serikali fidia ya sh. bilioni tano kwa
kumuunganisha katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini kinyume cha sheria.Kesi hiyo ya madai namba 35 ilifunguliwa katika mahakama hiyo juzi, akiwakilishwa na Wakili Richard Rweyongeza.
Hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya mdaiwa ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Zombe anaiomba mahakama kuruhusu alipwe kiasi hicho cha fedha kwa sababu taratibu za kukamatwa na kushitakiwa kwake zilikiukwa.
Ilidaiwa Bw. Zombe akiwa anakaimu nafasi ya RPC Mkoa wa Dar es Salaam watu wanne wakiwemo wachimba madini watatu wa Mahenge mkoani Morogoro waliuawa, na yeye alipata taarifa hizo kutoka kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni.
Inadaiwa baada ya kumaliza muda wa kukaimu alikabidhi ofisi na kurudi Rukwa Februari 2, 2006. Rais Jakaya Kikwete aliunda tume ya kuchunguza vifo hivyo lakini katika mapendekezo yao walipendekeza askari polisi 15 wakamatwe na wafunguliwe mashtaka ya mauaji.
Alidai baada ya siku 14 alipata uhamisho wa kurudi Dar es Salaam ambapo Juni 9, 2006 IGP alisema Bw. Zombe aunganishwe katika kesi ya mauaji ya watu hao.
Kutokana na uamuzi huo, Bw. Zombe anadai kuwa alifikishwa mahakamani kwa kesi ya mauaji na baada ya kusomewa mashtaka alipelekwa rumande Ukonga, lakini waliomkamata hawakumuhoji kuhusu na tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa mdai hayo, akiwa mahabusu Ukonga na Keko alilalamika kwa waziri mwenye dhamana kutokana na aliyokuwa akifanyiwa lakini hakukuwa na hatua zilizochukuliwa.
Hati hiyo ilidai kwamba polisi walishindwa kupata vielelezo vya kumuunganisha katika kesi hiyo na matokeo yake wakashindwa kesi, akaachiwa huru kwa kukosekana kwa ushahidi.
Bw. Zombe anadai aliathirika katika kipindi chote cha kesi hiyo, na hali hiyo ilisababishwa makusudi kwa kuacha kuchukua maelezo yake ambayo anadai yangesaidia aachiwe huru kabla hajafikishwa mahakamani.
Kutokana na hali hiyo na athari alizopata Bw. Zombe anadai fidia ya sh. 5,000,000,000.
Zombe na wenzake walituhumiwa kuwaua wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Matias Lukombe na dereva taksi, Juma Ndugu katika msitu wa Pande, Mbezi Louis, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Januari 14, 2006. Waliachiwa huru Agosti 17, 2009.
Ingekuwa vipi kama kila raia wa kawaida aliyedhulumika kupitia vyombo vya sheria naye angeidai serikali. hakuna ambaye angelipwa na mwisho wa siku jiuliza ingetokea nini? Ukweli ni kuwa huyu bwana Zombe lake limekwisha, kesi imeisha, kama 'sory bwana mkubwa' atapewa. lakini hilo ng'o, halitokea kwa sisi kabuku
ReplyDeleteNaye huyo Zombe aache hizo zake, kaponyoka kwenye mdomo wa mamba atulie, asijitafutie tena umaarufu kama ni umaarufu ashapitwa na wakati, hata waliofiwa hawtaki hata kusikia ten jina lake kwenye vyombo vya habari kwani linawaletea kichefu+2 kabla ya yote, fikiria uliyofanyia wananchi ulipokuwa mtumishi wa serekali ndipo udai hiyo BILION TANO.
ReplyDelete