Na Said Njuki, Loliondo
MCHUNGAJI Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Tanzania Ambilikile Mwasapile (78) wa Kijiji cha Samunge-Loliondo wilayani
Ngorongoro, Arusha,
ameonya wasafirishaji wanaopandisha nauli za kwenda eneo hilo hawatafika mbali na mwisho wa siku watafilisika.
Mbali na kupanda kwa bei hiyo pia mchungaji huyo amewashukia wanaopandisha bei za vyakula, huduma mbalimbali na vinywaji kuwa hizo ni baadhi tu ya kero zinazomchukiza Mwenyezi Mungu huku akikemea vikali wagonjwa wanaofanya vurugu wakati akitoa huduma, wanaodai kupatiwa dawa kabla zamu zao.
Nauli ya za kwenda kwa mchungaji huyo kutoka Arusha zilikuwa ambazo zilikuwa kati ya sh. 35,000 na 50,000 sasa zimepanda na kuwa kati ya sh 120,000 na 180,000 kwenda na kurudi kutegemeana na aina ya usafiri huku bei za bidhaa mbalimbali kama maji na vyakula zikiwa zimepanda maradufu katika kijiji hicho.
Mchungaji huyo anayejulikana zaidi kwa jina la ‘Babu’ akizungumza na waandishi wa habari juzi, kijijini hapo alielezea kusikitishwa na ulanguzi huo kuwa unafanywa
na watu wachache wasiojali tiba anazotoa kwa wagonjwa hao ambao wengi wao wana vipato vya chini, hivyo akaonya kwamba watafilisika kwani vitendo hivyo havimpendezi Mwenyezi Mungu.
“Nasikitishwa sana na tabia hiyo inayofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu na wasiojali maisha ya wenzao. Hii siyo biashara, kwa hiyo yeyote anayewanyonya wagonjwa hawa kwa kisingizio chochote kile nawambia wazi kuwa atafilisika tu,” alisema mchungaji huyo.
Akizungumza kwa upole huku akionekana kukerwa na tabia hiyo, alisema dawa anazotoa zinatokana na mti shamba na gharama yake ni sh 500 kwa wenyeji na dola moja kwa wageni kwa wageni kutoka nje na kwamba hayo ni maelekezo ya Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa ukusanyaji wa pesa hiyo naye amepewa maono ya kubaini mkusanyaji miongoni mwa wasaidizi wake.
Aliongeza kuwa baada ya kumwonyesha maono hayo alimkabidhi mzaidizi wake ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina na kubanisha kuwa tangu amkabidhi kazi hiyo hajui kiasi
gani cha fedha kilichokusanywa kupitia tiba hiyo iliyoanza miezi takribani minne iliyopita japo lengo la ukusanyaji wa pesa hiyo ni kwa ajili ya shughuli za upanuzi wa huduma hiyo.
Akizungumzia kuhusu uvumi uliosambazwa kuwa mchungaji huyo atasitisha huduma hiyo kipindi cha Kwaresma kinachoaanza leo, Mchungaji huyo alisisitiza kwamba si kweli na kwamba huduma zitaendelea kama kawaida isipokuwa siku ya Ijumaa Kuu na Jumapili ya Pasaka ambazo kwa kawaida ni siku za mapumziko kisheria.
Uvumi huyo umesababisha msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaokimbilia eneo hilo kupata tiba wakihofia kuchelewa huduma hiyo wakati wa kipindi cha Kwaresima, jambo
lililosababisha kupanda ghafla kwa kila kitu katika kipindi cha wiki moja.
Majira alishuhudia idadi kubwa ya magari ya aina mbalimbali yakiwemo mabasi yaliyojazana abiria, malori na kila aina ya usafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi yakiwa katika msururu mrefu unaoweza kufikia umbali wa kilomita 10 kutoka nyumbani kwa mchungaji huyo yakisubiri zamu ya kupatiwa huduma.
Msururu huyo unaweza kuwa na magari 2,000 yenye wastani wa wagonjwa 10 kila moja, huku magari mengine yakiendelea kumiminika katika eneo hilo kutoka maeneo mbalimbali
nchini kila kukicha.
Akizungumzia wingi huo wa watu, alisema “hilo ni tone tu la wingi wa watu wanaotarajiwa kufika eneo hilo kwa lengo la kupata tiba hiyo akieleza kuwa bado watu wengine wengi watakuja kutoka barani Afrika, Asia, Amerika, Ulaya na
kwingineko”.
Hata hivyo wakati huduma hiyo ikiendelea, hali ya mazingira na miundombinu mibovu imekuwa tishio kubwa la afya za wagonjwa hao kwani kila mmoja anajipikia mwenyewe
kwa wenye uwezo bila mpangilio wowote, huku mangenge ya vyakula yakiwa yametapakaa kila mahali bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari kwa wagonjwa hao.
Kukosekana kwa huduma ya vyoo na huduma nyinginezo kama mashimo ya kutupa taka ngumu nalo ni tatizo linalotishia afya za watu wanaoongezeka kwa kasi isiyowiana na kiwango cha huduma hiyo.
Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa harufu mbaya kila kona unayopita inayosababishwa na vinyesi na mikojo, huku takataka zingine zikiwemo mabaki ya chupa tupu za maji, mifuko ya mikate na boksi za biskuti zikizagaa, jambo linalohitaji utatuzi wa haraka.
Hata hivyo pamoja na dosari hizo bado wagonjwa hao wakiwemo viongozi na watendaji wakuu serikali wanamiminika katika kijiji hicho wakiwa na matumaini ya kupona magonjwa yao kama kisukari, kansa, ukimwi, presha na magonjwa mengine sugu.
Wakati huo huo, Bryceson Mathias anaripoti kutoka Dodoma kuwa mmoja wa waliokunywa dawa hiyo na kupata matokeo mazuri amemuomba Mchungaji Masapila atembee mikoani na kutoa huduma
hiyo, ili wasio na uwezo wa kufika huko, nao wanufaike na sauti waliyodai ni ya Mungu.
Akizungumza mbele ya kundi la watu na majirani waliompokea kutoka Loliondo, Bi. Ester Raphael Shinje (30) wa Nkuhungu ambaye alitoka Dodoma wiki iliyopita akiongozana na kaka zake aliomba, Bw. Masapila ateembee mikoani ili wasio na uwezo wa kufika kwake nao watibiwe.
“Namshukuru sana kaka yangu Bw. Fanuel Raphael (35) aliyekuwa Chunya (Machimboni), kufika na kunichukua ghafla akinitaka twende Loliondo, kwamba kuna mtu anatibu magonjwa sugu kwa maji ya sh. 500," alisema Bi. Shinje.
Alisema kisukari kilikua kinamsumbua kiasi ambacho alikata tamaa ya kuishi, lakini baada ya kunywa dawa sasa anajisikia mwepesi na afya inaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment