Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Mganda Sam Timbe amesema kwamba timu yake ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, endapo
watashinda mechi zao mbili zilizosalia, huku akiwaombea Simba wapoteze mchezo mmoja.
Timu ya Yanga juzi ilifanikiwa kuzoa pointi tatu kutoka kwa Azam FC, baada ya kuwafunga mabao 2-1 na hivyo kufikisha poiti 43 wakitofautiana pointi mbili na Simba, ambao ndiyo vinara wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 45.
Akizunguma juzi mara baada ya mchezo na Azam FC kumalizika, Timbe alisema lolote linaweza kutokea mbele ya safari ya kwenda katika ubingwa na anaona wazi kwamba timu yake bado ina nafasi ya kutwaa taji hilo.
"Kwa hapa tulipofikia ubingwa upo endapo tu, tutashinda mechi zetu mbili zilizosalia na Simba endapo watapoteza mchezo mmoja au yote, hakuna timu isiyotaka kuchukua ubingwa," alisema Timbe.
Alisema kwanza kabisa anashukuru kuona wamewazuia Azam FC, kukaa katika nafasi ya pili, kwani Azam wangeshinda jana walikuwa na uhakika mkubwa kabisa ya kuchukua nafasi ya pili.
Timbe amewataka wachezaji wake wasibweteke na ushindi wa juzi na badala yake waendelee kujituma, ili washinde michezo yao iliyosalia na kubwa zaidi wazidishe kufanya mazoezi ambayo ndiyo yaliwapa ushindi.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall ameitabiria timu ya Simba kutwaa ubingwa wa Bara pamoja na tofauti ya pointi mbili na Yanga.
'Bado ninaamini kabisa Simba, ndiyo mabingwa wa Bara muhimu wajitume katika mechi zao mbili zilizosalia, kwa upande wangu bado sijakata tamaa nitaendelea kupambana ili tushinde mechi zetu mbili zilizosalia," alisema Stewart.
Alisema katika mchezo wao wa juzi, kipa wake Vladimir Niyonkuru aliiangusha timu hiyo baada ya kutema mipira ovyo na hivyo kuwapa mwanya Yanga kufunga.
Hata hivyo kocha huyo alisema msimu ujao wa ligi, atahakikisha anafanyia marekebisho kikosi chake na kuongeza wachezaji wenye uwezo zaidi, ili timu yake itwae ubingwa.
No comments:
Post a Comment