Na Zahoro Mlanzi
NYOTA watatu wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), huenda wasiwepo katika kikosi kitakachoivaa Simba Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kushindwa kufika kambini kwa wakati.
Wachezaji hao ni Kanda Deo ambaye alikuwa Ouagadougou, Burkina Faso kuitumikia timu ya taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 23 ya DRC, Cheiban Traore akiwa na Mali na Abdoulaye Mohamed akiwa na Niger.
TP Mazembe ambao ndiyo mabingwa watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, wanatarajiwa kuwasili nchini leo tayari kwa mchezo wa Jumapili ambapo ule wa awali walishinda mabao 3-1 nyumbani kwao.
Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa klabu hiyo iliyotolewa juzi, ilieleza kwamba wachezaji mbalimbali wa timu hiyo walioitwa kwenda kuzitumikia timu zao za taifa walianza kurudi kambini tangu Jumatano jioni, lakini hao watatu bado.
Ilieleza siku ya mwisho waliotakiwa kuwasili kambini ni jana ambapo timu hiyo ilikuwa katika maandalizi ya mwisho wakifanyia mazoezi kwenye Uwanja wao wa Stade de Kenya, uliopo Lubumbashi nchini humo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa endapo hawatafika wataangalia uwezekano wa kuwatumia tiketi na moja kwa moja waje Dar es Salaam na ikishindikana hawana budi kubaki Lubumbashi.
"Wachezaji wengine waliendelea na mazoezi tangu Jumanne asubuhi na mchana, kundi la kwanza lilifanya bila kuwepo wale waliokuwepo katika timu za taifa na walifanya mazoezi chini ya Lamine Ndiaye," ilieleza taarifa hiyo.
Wachezaji hao walikuwa wakizitumikia timu za taifa za nchi hiyo katika mashindano ya Mataifa ya Afrika (CAN), ambazo fainali zake zitafanyikia Gabon na Guinea ya Ikweta na wengine katika mashindano ya Olimpiki.
No comments:
Post a Comment