Na James Gashumba wa EANA
BURUNDI na Rwanda wanatarajia kufikia maafikiano ya nchi gani ichukue nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo itakuwa wazi
kuanzia Aprili, mwaka huu.
Kwa kuzingatia utaratibu wa kuzunguka nchi hadi nchi nyingine ambao hata hivyo si wa kisheria, Rwanda na Burundi ambao ni wanachama wapya katika jumuiya hiyo ndio mataifa yaliyobaki katika kutwaa nafasi ya Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki nchini Rwanda, Bw. Robert Ssali, aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya nchi hizo.
Hata hivyo alisema kwamba mazungumzo hayo ni ya kupeana ushauri na wala si wa kufanya maamuzi ya nini kitakachojiri.
"haya si majadiliano kutokana na ukweli kwamba sasa ni zamu ya ama Rwanda au Burundi. Ni suala la kukubaliana nani aanze kwanza," alisema.
Pamoja na ukweli huo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kwamba Burundi kwa sasa haijakomaa vya kutosha kuliko Rwanda katika masuala ya kisiasa na wengine wanasema kwamba haijawa na uzoefu wa kutosha katika masuala ya kimataifa na inaweza kusambaratika kimsimamo kama kutakuwepo na shinikizo kubwa kutoka nje.
Huku ikiwa na hali isiyoridhisha kwenye uchumi, EAC iliruhusu Burundi kuchangia dola milioni moja katika bajeti ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2007/08 na 2008/ 09. Uongozi wa Juu wa Afrika Mashariki ulitaarifiwa kwamba hali ya kifedha ya Burundi si njema kiasi cha kutekeleza wajibu wake.
Kutokana na mazingira hayo taifa hilo lilisamehewa mchango wake ambao ulipaswa kuwa dola za Marekani milioni 4.5 kwa mwaka.
Kwa upande wake Rwanda imeshawahi kuchukua nafasi katika medani za kimataifa na ina uzoefu na siasa za kimataifa.
Ofisa wa ngazi za juu katika Jeshi la Rwanda, Luteni Jenerali Patrick Nyanvumba, aliwashinda maofisa wa kijeshi kutoka Nigeria na Ethiopia na kuwa Mkuu wa Majeshi ya Umoja wa Afrika (AU) yanayolinda amani Darfur nchini Sudan.
Baadaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilimchagua kuongoza majeshi ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa na y ale ya Umoja wa Afrika (UNAMID) mwaka 2009.
Aidha benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) inaongozwa na raia wa Rwanda Donald Kaberuka.
Awali katika kinyang’anyiro hicho mataifa ya Kenya na Uganda yalionesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya kiutendaji katika jumuiya ya Afrika Mashariki, hali ambayo ilitishia kuzuka kwa mgogoro. Mataifa hayo mawili kwa sasa yanaripotiwa kuacha kuwania nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment