28 March 2011

UVCCM wapigwa kombora jipya

*Yadaiwa 'wanaotukana wazee' mawakala wa mafisadi
*Shigela ang'aka, ataka anayewatuhumu awahi kortini


Na Waandishi Wetu

SASA ni wazi kuwa bundi ameendelea kukiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuendeleza minyukano ya siasa za kimakundi zilizoanza kujidhihirisha
takribani miaka minne iliyopita, huku hoja ya urais wa mwaka 2015 ikitawala sambamba na ile ya vita dhidi ya mafisadi.

Katika mwendelezo wa minyukano hiyo ya makundi, kila kundi likiwa na maslahi yake katika vita hiyo, jana kada mwingine kijana wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) ameibuka akisema kuwa vijana wenzake wa chama hicho ambao wamekuwa 'wakiwatukana' wazee wastaafu na hata viongozi wengine ndani ya chama hicho, wamekiuka katiba, wanatumiwa na mafisadi, hivyo waachie nafasi zao ndani ya siku saba.

Hatua hiyo ya kada huyo wa jana, imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa mnyukano wa kauli kutoka kwa baadhi ya viongozi wastaafu, viongozi wa CCM, viongozi wa serikali na wale wa UVCCM, ambapo hoja ambazo zimekuwa zikidhihirika kutamalaki ni ufisadi na harakati za kusaka ugombea wa urais wa 2015, kumrithi Rais Jakaya Kikwete, kupitia chama hicho.

Tukio la hivi karibuni linaloonekana kutibua mambo ndani ya chama hicho ni tamko la Baraza Kuu la UVCCM mkoani Pwani, ambalo kupitia kwa mwenyekiti wake Bw. Abdalla Ulega liliwataka viongozi wastaafu ambao wameshashiba, kuwaachia vijana hao zamu yao ya kula, wakisema pia jina la mgombea urais wa 2015 tayari liko mezani kwa rais wa sasa na mweyekiti wa taifa wa chama hicho.

Tamko hilo ambalo lilionekana kuwalenga baadhi ya viongozi walioko serikalini, wastaafu na wanachama ambao wamekuwa wakitoa maoni yao juu ya mwenendo wa chama hicho na taifa kwa ujumla, lilikuja baada makada waandamizi kama Fredrick Sumaye, Edward Lowassa, Samuel Sitta, kuonekana wakitoa kauli ambazo zilijibiwa na viongozi wa chama hicho kuwa hazikustahili kusemwa hadharani, bali kwenye vikao.

Hivi karibuni Baraza la UVCCM taifa baada ya kukutana katika kikao chake Dodoma, liliazimia pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa viongozi wa namna hiyo hawapati nafasi yoyote ya uongozi katika chama hicho, kuwa wako tayari kuzunguka nchi nzima, usiku na mchana katika kusimamia suala hilo.

Hata hivyo, tamko hilo limeelezwa na wachunguzi wa mambo kuwa linalenga kupindisha hoja, ili ionekanae wanaoifanya CCM ichukiwe na wananchi ni wakosoaji wa chama wanaotoa hoja zao nje ya vikao, wakati chuki kubwa inatokana na chama hicho kuwakumbatia wanachama wenye tuhuma za ufisadi.

Baadhi ya vyombo vya habari vilinukuu yaliyojiri katika kikao hicho, ambapo vita ya makundi mawili iliyoibuka miaka minne iliyopita baada ya kuibuliwa kwa kashfa ya kampuni tata ya Richmond na hatimaye kujiuzulu kwa Bw. Edward Lowassa kutoka kwenye nafasi ya uwaziri mkuu, yaliyopachikwa majina ya 'watuhumiwa wa ufisadi' na lile la 'wapambanaji dhidi ya ufisadi' yalidhihirika wazi.

Akidhihirisha katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kuwa minyukano inayoendelea ndani ya chama hicho, hususan kupitia UVCCM, kuwa ni juu ya kile kilichojulikana kama 'vita dhidi ya ufisadi', kada huyo Bw. Paul Makonda alihoji iweje viongozi wa UVCCM wanakuwa wepesi 'kuwatukana' wazee wanaotoa ushauri lakini hawatumii ujasiri huo huo kuwasema 'mafisadi' wanaokiharibu chama kutokana na tuhuma zao.

Akisema kuwa 'kila mtu duniani anatumiwa, inategemea kwa wakati gani, unatumiwa na nani kwa ajili gani,' alidai kuwa hayo yote yanatokana na kuwa kuna vijana ndani ya UVCCM wamekubali kutumiwa kwa maslahi binafsi ya kikundi cha watuhumiwa wa ufisadi, wenye mikakati ya kuwania urais wa mwaka 2015, ili kuwashambulia makada wengine ambao wanahisiwa kuwa wanaweza kuchukua fomu za kugombea, hivyo kuwa kikwazo kwa lile kundi la kwanza.

Alisema kuwa anashangaa viongozi wa UVCCM wanapata wapi mamlaka ya kukiuka katiba ya chama hicho, na kanuni za UVCCM, na kuwadhalilisha viongozi wastaafu (akitolea mfano wa Fredrick Sumaye, Jaji Warioba), ambao alisema wametumikia nchi kwa uadilifu, kwani ni sawa na kukidhalilisha chama hicho na kusababisha usumbufu, rabsha na msuguano miongoni mwa viongozi wa chama na serikali.

Alisema kikatiba UVCCM haina uwezo wala mamlaka ya kile ambacho viongozi wao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakifanya, kama vile kutaka 'kuiumba upya' jumuiya hiyo kwa kuifanyia mabadiliko akisema kuwa hilo haliwezekani kwani ni tawi la chama, hivyo UVCCM inaweza kurekebishwa pale chama chenyewe kitakapoamua kujifanyia mabadiliko yatakayozigusa jumuiya zake zote.

Alisema uongozi wa UVCCM ngazi ya taifa umekiuka kanuni kadhaa, ikiwemo sehemu ya 7 (i-v), ya 8 (i), akisema jumuiya hiyo inatakiwa kupokea maelekezo, maagizo, ushauri kutoka CCM, si kama inavyofanyika sasa, ambapo UVCCM ndiyo wanaotoa maagizo na kuishinikiza serikali na chama kufanya yale wanayodhani yana faida kwao "hii kamwe haikubaliki ndani ya CCM na serikalini," alisema Bw. Makonda.

UVCCM upinzani ndani ya CCM

Bw. Makonda ambaye alijitambulisha kama mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Moshi Vijijini, akiwa amekitumikia chama hicho katika kazi mbalimbali ikiwemo kuhesabu kura za urais mwaka jana wakati wa mkutano mkuu wa CCM, alisema vijana wengi nchini, wamepoteza imani na UVCCM, kwani imegeuka kuwa ya vijana wachache walioko katika nafasi za taifani, lakini ngazi ya chini hakuna matumaini yoyote ya uhai wa jumuiya hiyo.

"Mambo yanavyokwenda si sahihi, UVCCM hii ya akina Beno Malisa na Shigela imepoteza sifa ya kuwa jumuiya...hiki ni chama cha upinzani ndani ya CCM...eti sasa hivi wanasema tuandamane nchi nzima, tutawapata wapi vijana hao wa kuandamana, hatuna vijana huko chini, wale wa mwaka jana walikuwa ni wahuni tu waliochukuliwa mitaani, wakawa wanafanya fujo...hawakijui chama, hawajui itikadi...hii sasa si jumuiya ile ambayo akina Mzee Kawawa (Rashid) waliilea.

"Inapata wapi nguvu na mamlaka ya kutoa matamko na kuiagiza serikali, kama kuvunja bodi, kuwa eti usalama wa taifa umeshindwa kazi haumsaidii rais, gavana anamwacha rais anatoa matamko ya ajabu juu ya uchumi, wanataka sekretarieti iondoke, wanawasema wazee wastaafu wamekosa adabu, wanapata wapi uwezo huo...hizi ni kauli za uchonganishi...wanajua majukumu ya usalama wa taifa mpaka waseme wameshindwa kazi, wanajua majukumu ya gavana...hii si jumuiya ya kujisifia tena;

"Hawa viongozi wa UVCCM hii...hiki kitimu cha akina Malisa na Shigela kimeamua kuwa wasaidizi wa mafisadi, vibaraka wa mafisadi, hivyo kuwaita mafisadi si dhambi, unajua ukipokea rushwa uwezo wako wa kufikiri unakufa...sasa imefikia mahala UVCCM ina vijana wanawaza zamu yao ya kula badala ya kuwatumikia wananchi...hawa ni wezi," alisema Bw. Makonda.

Akizungumzia suala hilo, Bw. Shigela alisema wenyewe wanashughulika na mtu yeyote anayevunja maadili, awe fisadi, awe anatuhumiwa au anatuhumu, anazungumza nje ya vikao au anayeelekea kuwa fisadi.

Alisema UVCCM haiwezi kuwa wakala wa mafisadi bali aliyesema ndiye wakala wa mafisadi, hajui mawahusiano ya jumuiya na chama, na wanachofanya ndiyo kazi yao.

"Kama anaona tumevunja katiba siku saba ni nyingi mno, ashtaki kwenye jumuiya au kwenye chama, na akiona huko hapati haki akimbilie mahakamani kesho,' alisema na kuongeza: Huyo tunamjua ametumwa, mtu aliyenunuliwa utamjua tu. watu wa Kilimanjaro alikosema yeye ni kiongozi wamemkana na wamesema watampeleka mahakamani.Alisema hao mafisadi walikuwa wanamsomesha shule, na shule amefukuzwa kwa kushindwa masomo, ndio maana yuko mjini.

Uraia wa Hussein Bashe

Bw. Makonda aliibua upya madai ya hoja ya uraia wa Bw. Hussein Bashe akisema hapaswi kujihusisha na masuala ya jumuiya hiyo, kwani si raia, kama ambavyo iliwahi kutamkwa na uongozi wa chama hicho katika vikao halali, chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, kisha kusisitizwa na viongozi wa CCM, kama Katibu Mkuu, Yusuf Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Bw. John Chiligati, "iweje Bashe apewe jukumu zito la kukusanya maoni ya muundo bora wa UVCCM wakati mwenyewe ni tatizo," alisema;

"Hakuna tamko lingine mbadala limewahi kutolewa kuthibitisha uraia wake baada ya lile la mwanzo ambalo lilitolewa na Halmashauri Kuu ya chama katika kikao halali chini ya mwenyekiti ambaye pia ni rais...ambaye ana taarifa zote za polisi, uhamiaji, usalama... iweje mtu ambaye si raia apewe kazi ambayo mstakabali wake una athari kwa vijana raia wa taifa hili...huu ndiyo sasa ufisadi wa hali ya juu kabisa kuingia kwenye kumbukumbu za taifa hili.

Alitumia fursa hiyo kuitaka sekretarieti yote ya UVCCM kuitisha mkutano na waandishi wa habari ili kuwaomba radhi Watanzania kwa matusi yao kwa viongozi wastaafu na wengine walioko serikalini, yaliyosababisha chama kudharauliwa, kisha iachie ngazi. Pia kamati ya utekelezaji nayo iachie ngazi, huku Baraza Kuu likitakiwa kujivunja.

Pia aliomba radhi kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, akisema "kwa niaba yangu mwenyewe na vijana wenye mtazamo kama wangu, vijana wote wa UVCCM wasiokubaliana na maamuzi ya kijinga ya viongozi wao wa ngazi ya taifa, Watanzania wote waliochukia kauli ya baraza la Mkoa wa Pwani na baraza kuu kule Dodoma na kwa niaba ya chama ili kisione kuwa wote tumekengeuka, tupo wenye mapenzi mema na chama hata kama uongozi wa UVCCM unatusukumia CHADEMA."

Wapinzani wamtetea Sumaye

Kitendo cha Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Pwani kumtolea maneno ya kejeli Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Fredrick Sumaye hadharani kimedaiwa kuwa ukosefu wa utovu wa nidhamu na maadili  kwa sababu ni sawa na baba yao mzazi.

Mbali na hilo, kauli yao nyingine kuwa jina la mgombea urais lipo mezani kwa Rais Jakaya Kikwete inaonesha kwamba ni udhahifu na hivyo rais anapaswa kuwachukulia hatua.

Kauli hizo zimetolewa jana na vyama vya upinzani visivyokuwa na wabunge bungeni katika Viwanja vya Jangwani wakati walipokuwa wakizungumzia amani na utulivu wa nchi.

Akihutubia katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa TADEA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Ushauriano la vyama vya siasa, Bw. Juma Khatib alisema kuwa maneno ya kebehi ambayo UVCCM waliyomtolea Bw. Sumaye ni kashfa, hivyo ni vizuri wakaheshimu wazee.

"Sumaye pamoja na kwamba ni Waziri Mstaafu, vile vile yule ni sawa na baba zao waliowazaa," alisema.

Alisema kuwa Bw. Sumaye aliongoza taifa kwa matatizo makubwa na aliweza kuwafikisha Watanzania hapa walipo sasa, hivyo UVCCM walipaswa kumshukuru na siyo kumtolea 'kauli za utumbo'.

Bw. Khatib alisema kuwa Bw. Sumaye alikuwa kiongozi mkubwa wa nchi kwa muda wa miaka kumi na ameweka historia kubwa na kusisitiza kwamba matamshi ya UVCCM hayakuwa sahihi.

"Kwanza UVCCM siyo chama cha siasa ni taasisi, hivyo hawakupaswa kuzungumzia mambo hayo hadharani. Tuliwaeleza CCM siku moja kwamba UVCCM inatakiwa kuwa ndani ya chama hicho na siyo nje.

"Siyo tabia nzuri UVCCM kuwaumbua mawaziri wakuu wastaafu na viongozi, kwani wanapofanya hivyo wanakipaka matope chama chao ikiwa ni pamoja na kupotosha maadili ya Tanzania.

UVCCM vya vipindi vilivyopita hawakuwa na utamaduni wa kuwaumbua viongozi wao hadharani, kiongozi yoyote ni lazima apewe heshima yake," alisema.

Naye Mwenyekiti wa Taifa SAU, Dkt. Paul Kyara alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa vurugu kidogo za hapa na pale ni hatua nzuri ingawa sheria na taratibu nyingi inabidi zirekebishwe ili kuwa na uwanja sawia katika tasnia ya kisiasa, hususan siasa za vyama vingi.

"Wakati wa uchaguzi sasa umekwisha na wagombea waliahidi mambo mengi, lakini inashangaza wanapotembelea magari ya gharama na kuishi kwenye mahoteli ya kisasa badala ya kutekeleza majukumu yao," alisema.

CCM ichukue hatua
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshauriwa kuchukua hatua madhubuti ili kudhibiti tabia ya malumbano ya kurushiana maneno makali kati ya wana CCM wenyewe kwa wenyewe ambayo inaelekea kukithiri katika siku za hivi karibuni.
 
Ushauri huo ulitolewa jana mjini Shinyanga na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Bw. Hamisi Mgeja alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake waliotaka kufahamu msimamo wake juu ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na UVCCM dhidi ya viongozi wastaafu nchini.
 
Bw. Mgeja ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, alisema malumbano yanayoendelea hivi sasa yanaweza kuhatarisha uhai wa chama na kwamba ni vizuri sasa uongozi wa CCM Taifa ukachukua maamuzi mazito kwa kuzuia mara moja malumbano hayo.
 
Alisema kwa kawaida chama hakijengwi na malumbano ya kurushiana maneno bali tatizo lolote linalojitokeza linafaa likajadiliwa ndani ya vikao halali vya chama na kutatuliwa badala ya kulitoa nje huku wana CCM wakishughulikiana wenyewe kwa wenyewe.

“Kwa kweli binafsi yangu nasikitishwa na hali inavyokwenda hivi sasa ndani ya chama chetu, katika hali ya kusikitisha tumeacha kutekeleza ilani ya uchaguzi kama tulivyokuwa tumewaahidi wananchi na badala yake tumeanza kushughulikiana sisi wenyewe kwa wenyewe.
 
“CCM kama chama tawala tunapaswa tuelewe kuwa ni tegemeo la Watanzania wengi ambao wanategemea kuona mambo makubwa itakayoyafanya kwa ajili ya kuwaletea wananchi mageuzi makubwa katika maendeleo yao, wanaamini kuwa CCM ndiyo yenye majibu yote ya matatizo yao.

Imeandaliwa na Tumaini Makene na Gladness Mboma, Dar; na Suleiman Abeid, Shinyanga

15 comments:

  1. Huyu Shigela nimemfuatilia hotuba na statement zake mbali mbali na kugundua kuwa ni mtu asiye na upeo kabisa,ni aibu kwa Sumaye kuendelea kubishana na mtu kama shigela,people will not notice the difference,ushauri kwa Sumaye akae kimya aachane na huyu Shigela,We know what shigela is doing is purely political suicide,hana future kwenye politics,after all Shigella sio kijana sijui anafanya nini kwenye umoja huo ambao kwa sasa umekosa muelekeo kabisa,kila mkoa UVCCM ina mitazamo yake,sio siri viongozi wa kitaifa wa UVCCM wamenasa sawasawa kwenye ndoano ya mafisadi,hakuna ujanja.SiKWAMBA NAMSAPOTI SUMAYE,NO NO, Sumaye ni kiongozi hafai kabisa kfikiriwa acha kupewa nchi,muda aliotumikia unatosha,aliyoyafanya tunayajua,hana mpya.Tunajua alienda kusoma digrii ili aqualify kuwa candidate wa uraisi kwani wakati ni waziri mkuu alikuwa ana diploma ya ukiriguru ya kilimo.Alionyesha uwezo mdogo sana akiwa waziri mkuu,alinyanyasa watu kibao na ni dictator ,mbabe na asiye na maono,comperatively nafuu ya mzee lowassa japo naye amechafuka hawezi kuwa raisi mzuri na obviously CCM wakileta jina lake hatutampa kura.

    ReplyDelete
  2. Wananchi wenzangu, acha tuyaone ya Musa baada ya kushangaa ya Firauni. CCM imechafuka kikwelikweli, sasa viongozi wakuu wanatumia UVCCM kuwamaliza makada wanaonekana watakwamisha jina la mtu ambaye tayari Rais ameshamchagua kama pendekezo lake la mtu wa kumrithi kupitia CCM. Cha kushangaza na kujiuliza ni kama hawa UVCCM wana hakika gani ya mtu wa JK kupita katika uchaguzi? Au mbinu ni zile zile za kuwazuia mawakala na waangalizi wa uchaguzi kutoshuhudia idadi ya kura za urais kama Tume ilivyofanya uchaguzi wa 2010.

    Jamani someni ripoti ya waangalizi kutoa nchi za Ulaya ili muone ni jinsi gani JK hakushinda katika uchaguzi huo. Tume ilimpitisha ili kumnusuru.

    Acheni UVCCM na baba yao CCM wanyukane ili wananchi waamue mapema mustakabali wa uongozi wa nchi hii.

    ReplyDelete
  3. LAZIMA MZOZO UTOKEE WEWE UNAMUONA MAKAMBA NA UZEE WAKE ANAJIITA NI MMOJA KATI YA UMOJA WA VIJANA CCM, WAPI NA WAPI, ZEE ZIMA LINAJIITA KIJANA, KUTOACHIA MADARAKA NDANI YA CCM NI UFISADI WENU. MMEJAWA NA UROHO WA MADARAKA HATA MNASHINDWA KUPUMUA, MMEZEEKA LAKINI BADO CHOKOCHOKO NI MBICHI. CCM KAMA ITAKUFA ITAKUWA NEEMA KWA WATANZANIA. NA HATA MKITUMIA UFISADI WENU 2015 HAMTAPATA USHINDI, ANFDAENI SANA TUKOFIA NA KANGA NA TISHERTI ILI MHONGE WAPIGA KURA LAKINI CHAMOTO MAKIONA. TUMECHOSHWA NA CCM FISADI.

    ReplyDelete
  4. bado ktambo kdogo tutaizka ccm na chadema itaibuka. migogoro hii n ishara njema ya ukomboz wa nchi na wanyonge wote.chadema jiandaen kuchukua nchi

    ReplyDelete
  5. Vijana gani hawa wenye fikra zilizozeeka namna hii?

    ReplyDelete
  6. UKWELI USIOFICHIKA KUNA MPASUKO NDANI YA UVCCM MAANA TOKEA KUENGULIWA KWA MWENYEKITI KWA KUDANGANYA UMRI WAKE HAWA VIJANA WAMEKOSA MWELEKEO, SIO WOTE ILA BAADHI YA HAO WANAOMFATA MAKAMBA KWANI HY MZEE MAKAMBA AMEZEEKA MPK AKILI YAKE IMEZEEKA,NI VEMA HAYA YAMEJITOKEZA MAPEMA KUNA MUDA WA KUYAREKEBISHA,WANAOTEGEMEA KUMEGUKA AU CCM KUANGUKA!! HAYO YOTE YANAWEZA KUTOKEA LAKINI....,TUWE NA FIKRA NA KAZI YA ZIADA MAANA TUKUMBUKE KUWA DUA YA KUKU KWA MWEWE.INGAWA MNACHEKELEA TUKAE TUKIJUWA UKIONA MWENZIO ANATAKA KUNYOLEWA NAWE TIA MAJI,USISHANGILIE MPK ANYOLEWE MAANA WEMBE UNAWEZA UKAKOSA MAKALI UPANDE WA CCM UKANYOA KWAKO!!USICHEKE MAMBA KABLA HUJAVUKA MTO USITUKANE WAKUNGA WAKATI UZAZI UNGALIPO!!

    ReplyDelete
  7. CCM wako juu na watakuwa juu zaidi , ila kuwa hao Mazee yamekomaa mpk akili zao zinadata inabidi watimuliwe haraka sana tena sasa, ili chama kiwe na mwelekeo maana sasa hakina msemaji madhubuti kila mtu anaropoka hovyo,huyo kijana wa Pwani Ulega inabidi amulikwe aliyoyasema ni yake au katumwa maana hata mzee makamba alipohojiw kuhusu kauli ya huyo kijana ameonyesha kumuunga mkono,kuhusu Bashe mbona kauli ilishatoka kuwa ni Raia Wizara imethibitisha hayo lakini ni utashi wa kina makamba kumtosa kwa sababu zao binafsi CCM iko imara ila tatizo baadh yao ni tamaa na vinganganizi

    ReplyDelete
  8. Waoo nafarijika sana, Vita vya panzi furaha kwa.... Naomba hao vijana wazee waendelee kuzozana na baba zao kwani hata hivyo wengine ni wazee kama kina Sumaye. Sisi tunapenda ikiwezekana wazozane wote bila kujali ni vijana,kina mama au wazee na kina baba ili wapatikane kina uhuru kenyata wa TZ hso wote hawana busara wala fikra ndo maana wanafanya mambo kwa mtazamo wa kupata uongozi fulani. hakuna mtanzania anayetaabika kwa hali ya sasa atakaye wachagua tena labda wenye mawazo mgando kama yao. tena watuache tuhangaike na matatizo yetu au wakapate kikombe kwa babu ili watibu akili zao ndio watakumbuka matatizo na kusahau tamaa ya uongozi. Ras David Say'S

    ReplyDelete
  9. Baba wa taifa mwalimu nyerere alisema alipenda kuona CCM inagawanyika kuwa mbili! lakini kwa mtazamo wangu sasa kutakuwa na CCM tatu siku si nyingi, Yaani 1.CCM Uswahili-Mwenyekiti Jakaya Kikwete, katibu Makamba pamoja na wafuasi wake.
    Pia itakuja 2.CCM Mafisadi-mwenyekiti-Edward Lowasa, katibu wake Rostom Aziz na wafuasi wake, mwisho itabaki 3. CCM itikadi- mwenyekiti-pius msekwa, katibu wake joseph Butiku na wafuasi wake! ok kama wewe ni MwanaCCM bila shaka utajuwa wewe jiendae kwenda wapi!

    ReplyDelete
  10. TATIZO LA UVCCM NI UDUNI WA ELIMU DUNIA, HATA UKIONA MANENO WANAYOSEMA NIKAMA VILE MTU HAJAENDA SHULE!NAKAMA WALIMALIZA SHULE BASI WALIMALIZA KWA KUDRA YA MWENYEZI MUNGU MWENYE REHEMA ZOTE.
    KINACHO NISHANGAZA ZAIDI NI KWA NINI MWENYEKITI WA CCM AMEKAA KIMYA NA KURUHUSU HAYA MAJIBIZANO YAKIENDELEA? BILA SHAKA SASA TUNAWEZA KUONA UDHAIFU WA HUYU MWENYEKETI WA TAIFA WA CCM.

    ReplyDelete
  11. BARUA YA WAZI KWA WANA-CCM.
    Hivi haya maneno na malumbambano ya kila siku hamuoni kuwa badala ya kujenga chama chenu mnakibomoa chama hiki kikongwe? Hivi mwenyekiti wa chama hiki mheshimiwa J.kikwete yuko wapi? hivi kweli anafurahia hali hii ya malumbano yasiyo na tija? hivi mzee makamba kwa hekima ya uzee wake anaona busara kupayuka kila siku kwa mambo yale yale? Sumaye akisema kitu wanamjibu, lakini chadema wakirusha dongo la CCM wanakaa kimya kiasi kwamba wananchi wanafikiri ni kweli yale chadema wanayosema ni kweli! mbona kama katibu wa chama hujibu mapigo ya chadema? mie naona mzee makamba husitahili cheo hicho!ni muda wako mzuri wa kujiuzuru nafasi hii, hapo ulipofikisha chama inatosha!!! unajenge uswahili sana katika chama na sasa umemuambukiza mwenyeketi wa CCM mh. J kikwete uswahili huo.
    Ebu tukumbushane kama siyo mageuzi haya batiri ndani ya CCM ya sasa,enzi ya uwenyekiti wa baba wa taifa hali hii ya kutukanana kada wa CCM kwa kada wa CCM ingeweza kutokea? kwa mtazamo wangu chama cha CCM kimekosa mvuto tena na jinsi kinavyoendeshwa ni ibilisi tu ndiye anayejuwa chama kinatumia dira gani! NINI KINAFANYA KIKWETE KUKAA KIMYA??? bila shaka anahusika na kile kinachoendelea sasa hivi ndani ya chama chake, vinginevyo kikwete ameshindwa kuongoza chama ni bora aachie ngazi kama mwalimu nyerere alivyoachia ili chama hiki kirudiwe na hadhi na heshima kama ilivyokuwa mwanzo.

    ReplyDelete
  12. CCM INAKUFA. JK HAFAI KUWA KIONGOZI. CCM INAFIA MIKONONI MWAKE...

    ReplyDelete
  13. Hapa tatizo ni Mwenyekiti wao... watanzania tuliwaambia kuwa huyo jamaa hafai kua hata katibu kata. sembuse kuongoza chama na addiritura kuongoza nchi? Raisi gani, Chama gani, chenye kumtumia mtoto wake (Riziwani) kutumia mabilioni ya chama kuzunguka nchi kwa mlango wa kampeni za uchaguzi. Riziwani ni nani katika Chama. Na yule mototo mwingine wa Mwenyekiti aliyekuwa akitunza mfuko wa njuluku kwa ajili ya uchaguzi... Nyie UVCCM mlikuwa wapi wakati hayo yalipokuwa yakitendeka? Mlipanda ulaghai mbele ya sisi vijana wenzetu maskini wa tanzania na mkaamua kupigana upande wa wenye pesa, mkapoteza mvuto, na sasa mnavuna fedheha!

    ReplyDelete
  14. Duh CCM poleni mno! sijui mnajisikiaje? mmesoma walichoandika walionitangulia? Sipendi mambo ya siasa hata kamwe, ni kheri nafasi niliyo nayo hainiruhusu kujiunga na chama cha kisiasa! jaribuni kutafuta suluhu ila kweli chama chenu kitakufa!! chukueni hatua za makusudi kukinusuru chama!!!Ila nanyi mlijiaona miungu ndani ya Tanzania hii!! Ni adhabu kutoka kwa Mungu mnaipata!

    ReplyDelete
  15. Matokeo ya kupeana uongozi kwa kujuana. mtoto wa mjomba, shangazi, kada mzuri ndio hayo! Nani wa kumuadabisha mwenzie? Kila mtu ni mkubwa kwa mwenzie hata wazazi wao hawawaeshimu, ukiuliza baba katibu, mjomba waziri,shangazi mwenezi. Sasa huo msiba umefika na utawamaliza tu, mti umekuwa na umeimarisha mizizi, poleni sana lakini pia watanzania tunashukuru Mungu amewaweka wazi, tulisema sana siku za nyuma watu wakasema hakuna tatizo. Please vyama vingine kaeni chojo na jinamizi la undugunization (chadema, TLP, UDP, CUF)

    ReplyDelete