28 March 2011

MAAFA LOLIONDO Babu azuia wagonjwa wapya

*Atoa wiki moja waliopo kwanza waishe
Na Said Njuki, Loliondo

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ambilikile Mwasapile amewataka wagonjwa wanaotarajia kwenda kwake kupata tiba kusitisha
safari zao hadi Aprili Mosi mwaka huu atakapomaliza kuwahudumia wagonjwa waliopo kijijini hapo kwa sasa ili kupunguza maafa na vifo vinavyotokea mara kwa mara.

Akitoa tamko hilo juzi, mchungaji huyo maarufu kwa jina la ‘Babu’ aliomba ushirikiano katika kuboresha tiba hiyo badala ya watu kufa kwa maafa kama yanayotokea huko Loliondo kutokana na msongamano wa watu.

"Pamoja na kuwashukuru kwa muitikio wenu, naomba mnisaidie ili kupunguza msongamano wa watu wanaokadiriwa kufikia 24,000, magari 4,000 yaliyo katika msururu unaofikia kilomita 55 kutoka nyumbani kwangu. Mbali na yaliyoharibika kama 100, najua inawachukua siku tatu hadi saba kupata tiba, hali si nzuri na inahitaji hatua za haraka kuchukuliwa,” alisema Babu huku akisisitiza kuwa bado anazo nguvu za kutoa tiba hiyo.

Awali, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Arusha zikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Bw. William Lukuvi ziliketi Arusha kutafuta mustakabali wa tiba hiyo kutoka na idadi kubwa ya wagonjwa bila mafanikio hadi walipoomba msaada wa mchungaji huyo.

Katika jitihada za kutafuta suluhisho hilo, ilibidi Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumfuata Mchungaji Masapila kwa ushauri zaidi ndipo mchungaji huyo naye akakubali kutoa tamko hilo juzi nyumbani kwake Samunge, huku akionekana kuwa na huruma kwa wagonjwa hao, hususan wale wanaokufa wakifuata tiba kwake.

Alitoa mapendekezo kadhaa, muhimu likiwa ni kwa wale wanaotarajia kwenda kwake kusubiri kwa wiki moja ili apate nafasi ya kuwaondoa walioko huko, ambao wanaishi katika mashaka makubwa, huku watu wakizidi kuzidiwa na wengine kufa wakiwa njiani.

Pia Babu aliwataka wasafirishaji kutumia magari mazima badala ya malori mabovu, huku akisisitiza wagonjwa mahututi wanaokimbizwa mahospitalini wasikipelekwe kwake na iwapo wagonjwa wanaenda kupata tiba kwake waendelee kutumia dawa zao za hospitali kabla hawajapata kikombe chake.

Mchungaji huyo alikubaliana na ushauri wa serikali wa kutoza sh 5,000 kwa kila gari na sh 150,000 kwa kila helkopta itakayotua huko ili pesa zinazopatikana zisaidie kuboresha mazingira na kuweka miundombinu mbalimbali ikiwemo vyoo na mahema kwa ajili ya kupunzikia wagonjwa kabla ya kupata tiba yake.

Babu pia aliiomba serikali katika kipindi hichi cha wiki moja kukarabati barabara na kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha wagonjwa 2,000 kupata tiba kila siku, kusafisha mazingira, kujenga vyoo, kuweka miundombinu mizuri ya maji na kutengeneza eneo la kupumzikia wagonjwa kabla ya kupata tiba.

Maafa ya kutisha

Kutokana na ugumu wa kumfikia Babu Mwasapile, baadhi ya wagonjwa wamekufa njiani na miili wao kutelekezwa vichakani kutokana na wasafirishaji kushindwa ama kurudisha miili hiyo walipoitoa au kusogea nayo mbele kwenye foleni ya kuelekea kijijini Samunge.

Juzi zaidi ya maiti tano zilikuwepo maeneo ya nyumbani kwa mchungaji huyo baadhi zikiwa zimetupwa katika kingo cha barabara na kufunikwa majani. Maiti mojawapo ndugu zake kutoka Tabora walitoa ruhusa ya kuzikwa huko huko Samunge na nyingine ilikuwa ikisubiri gari kupelekwa nyumbani.

“Nawatafuta viongozi wa serikali ya kijiji ili wanipe ruhusa mini na vijana wangu tuzike mwili huu badala ya kuteseka hapa kwa zaidi ya siku tatu, na umeaanza kunuka. Nitatoa gharama zote za mazishi ya ndugu yetu, huu ni unyama usiomithilika,” alisema Bw. Hussein Ally ‘Befee’ kutoka Singida.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Erasto Mjaledi alisema yeye alifika hapo siku tisa zilizopita na baba yake Mzee Mjaledi Mwinuka wa Makete ambaye alikufa Machi 23, mwaka huu na hadi juzi walishindwa kuondoka baada ya basi walilokwenda nalo kukosa mafuta lita 40 za kufikia Mto wa Mbu.

Kulikuwapo madai kuwa maiti zaidi ya 15 zilikuwa katika magari ambayo hayajafika kwa Babu, na hivyo kuiomba serikali kukagua magari yote yaliyo katika foleni na maiti zinapobainika zipatiwe msaada wa kupelekwa kuzikwa popote inavyowezekana badala ya kuacha maiti hizo zikitupwa ovyo.

Vigogo na kikombe cha Babu

Juzi mchana ilikuwa ni zamu ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Terezya Huvisa waliongia mchana nyumbani kwa Babu na baada ya mchungaji huyo kuzungumza na waandishi na mawaziri hao aliendelea kutoa tiba na wao kupata kikombe chao.

Babu kama kawaida yake aliagiza wasaidizi wake kuleta vikombe na ndoo ya dawa tayari kutoa tiba hiyo, licha ya wananchi waliokuwa wakisubiri kuanza kupiga kelele kuwa wanacheleweshwa na vigogo hao, lakini wasaidizi wake waliwaomba radhi wananchi hao kusubiri kwa muda kidogo.

Baada ya kupata dawa, mawaziri hao walichangia sh 700,000
kwa ajili ya kuongeza masufuria ya kuchemshia dawa na vikombe kwa ajili ya kupunguza uhaba wa vifaa hivyo na babu akawashukuru kwa msaada huo.

Mchungaji EAGT ataka Babu akamatwe

Naye Zuhura Semkucha anaripoti kutoka Shinyanga kuwa, Mchungaji wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God (EAGT) Lubaga Mkoani Shinyanga Obedi Jilala amesema kuwa huduma inayotolewa na Babu ni pepo kubwa na anafanya uhalibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti anayotumia kama dawa.

Hayo ameyasema jana wakati alipokuwa anaongoza sara ya Jumapili kwa waumini wake ambapo aliwataka waumini wake na watu wengine waachane na imani kuwa dawa hizo zinatiba magonjwa sugu.

Alisema kuwa suala la kunywa kikombe kwa babu ni ukosefu wa imani kubwa hata kwenye biblia hakuna andiko kuwa ipo siku kuna mtu atajitikeza kutoa huduma ya kikombe.

Pia alisema kuwa hana imani na dawa hiyo inayotolewa na babu huyo kwa sababu iwapo ingekuwa dawa ya kweli ingeweza kutolewa hata nje ya eneo hilo la Loliondo hata kwa wagonjwa waliopo nje ya eneo hilo.

"Kama kweli ni dawa inatibu kwa nini itolewe eneo hilo tu, ebu oneni watu wanavyokufa, angekuwa anatoa hata kwa ndugu wa wagonjwa ambao wanapenda kuwapelekea nyumbani ndio ningeamini, lakini suala la mpaka yeye ndio akupe hilo ni pepo," alisema.

2 comments:

  1. Gazeni La Majira naomba mfanye Uchunguzi mdogo wasomaji wenu tujua NANI ANALIPA GHARAMA ZA VIONGOZI WANAOENDA KWA BABU...MAANA NINA MASHAKA NA HILI SANA.

    ReplyDelete
  2. Mchungaji huna sfa ya kuitwa mchungaji kama unapingana na babu anayesaidia watu huo ni wivu mmejianzishia vikanisa vya kuibia watu huku mkitoza sadaka kubwa .Hakuna pepo linalotibu hata YESU alizushiwa anatibu kwa Belizabuli UMESOMA KIWANGO GANI MPAKA UITWE MCHUNGAJI au umejipachika tu . ACHA kukemea mambo mazuri MATENDO MAKUU YA MUNGU .

    ReplyDelete