04 March 2011

Tunadhibiti ubora wa vyeti UDOM-Prof Kikula

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), umetupili mbali madai ya wahitimu wa kozi mbalimbali kuwa vyeti vyao vimecheleweshwa tangu walipohitimu
Novemba mwaka jana, ukidai kuwa hatua hiyo ni muhimu kudhibiti wa ubora wa nyaraka hizo.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema chuo hicho kimeweka utaratibu kuhakikisha vyeti vyake vinakuwa bora zaidi kiasi cha kushindwa kugushiwa na wajanja.

Prof. Kikula alikuwa akijibu swali la gazeti hili kuhusu malalamiko ya baadhi ya wahitimu wa shahada za awali na zile za uzamili kucheleweshewa vyeti hadi sasa.

"Jamani UDOM ni moja kati ya vyuo vikuu vinavyotoa vyeti kwa wakati, kinachofanyika ni kusimamia ubora wake, vyeti vyetu si rahisi kugushi ndio maana tunachapa nje ya nchi na hatuwezi kusema ni wapi maana ni siri yetu," alisema Profesa Kikula.

Hata hivyo Prof. Kikula aliwataka Watanzania hususan wasomi kujenga tabia ya kujiamini na kuwa wadadisi kutafuta taarifa sahihi maeneo husika na kuacha tabia ya kulalamika.

"Jamani tunataka tujenge taifa ya aina gani! Tusiwe walalamikaji tu kwa kila kitu, ni aibu kwa mwanachuo kuhitimu bila kujua taratibu za vyuo vikuu," alisema Prof. Kikula.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Utafiti na Taaluma Profesa Ludovick Kinabo, alisema vyeti vya wahitimu wa Chuo hicho vililetwa hata kabla ya mahafali ya kwanza mwaka jana.

"Vyeti vya wahitimu vililetwa mapema, wapo wachache ambao kulikuwa na dosari ndogondogo tulishavipokea jana (juzi Machi 2) kwa DHL," alisema Profesa Kinabo.

Alisema kwa kawaida vyeti vya taaluma vinavyoonesha alama na maendeleo ya taaluma kwa kila mwanafunzi huchelewa kidogo kutokana na uhakiki ili kuepuka makosa yasiyo ya lazima.

Hata hivyo alisema vyeti hivyo pia vitawasili nchini ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

5 comments:

  1. Acheni visingizio hivyo, toeni vyeti watu wakahangaikie kazi/kujiendeleza. Kwani miaka yote hiyo mlikuwa hamlitambui hilo mkajipanga? Watu wanafoji noti itakuwa vyeti? Toeni wahitimu bora na siyo vyeti bora.

    ReplyDelete
  2. Ubora wa elimu ni muhimu zaidi ya karatasi (cheti). Makamu Mkuu wa Chuo, tembelea madarasani uone wanafunzi wanavyofundishwa, kwani watu wenye degree moja na mbili ndio wanakabidhiwa course kufundisha.Wanafunzi wana kaa zaidi ya 3000 katika chumba chenye uwezo wa kuchukua watu 300, AC mbovu, hewa hakuna. Hakuna maabara ya komputer, internet,vitabu hakuna: elimu mnafanya siasa. Mnatangaza majengo ya kichina ambayo yanavuja, na kupata ufa kila kukicha (subirini yaje yaanguke watu wafe ndo mtafurahi)mhitimu wa udom si bora hata kidogo. hawezi hata kutumia computa.tafadhali zingatieni ubora wa elimu, acheni siasa.....
    College of education ndo balaa: mbona uliweza ulipokuwa uclas, sasa kinakushinda nini?
    Walimu mnaoajiri wenye gpa zaidi ya 3.8 si wote ni bora, punguzeni kiwango hiki kulingana na tcu 3.5 mtapata walimu wengi tena bora kuliko hao mnaofikiria ni wazuri, tumesoma nao...tunawafahamu hawana lolote zaidi ya kuiba kazi za watu.

    ReplyDelete
  3. Jamani tusi lalamike sana UDOM ni chuo cha kata kama zilivyo sekondari za kata;hapa cc hakuna ubora wa elimu,kinacho jaliwa zaidi ni wingi wa wanafunzi

    ReplyDelete
  4. Watanzania tumezoea kudanganywa. Anachokisema Prof. hata yeye anajua sio cha kweli. Wahitimu hao watasubiri sana labda wajiorganize wagome ndo watapata hivyo vyeti. UDOM hawana jipya kuliko vyuo vingine!

    ReplyDelete
  5. Mimi binafsi sikubaliani na hilo hivi kuna logic gani toka 2010 hadi leo 2012 wanafunzi hawajapewa vyeti kila ukiuliza uingereza uingereza jamani hili siyo sahihi naomba tusaidiwe kuuliza wanafunzi wa BBA evening 2007/2010 hawajapewa transcript wala chochote hadi hivi leo, nadhani chuo hakikujipanga kuanzisha evening program na ndo maana wameshindwa Kikula unafamu hilo ? kuna watu hawana cheti hadi leo ? ?

    ReplyDelete