04 March 2011

India kusaidia kuongeza idadi ya watalii

Na Grace Michael

WAKALA wa Kampuni ya Sun Phamaceutical Ltd imekubali kuleta  wafanyakazi wake 1,000 kwa ajili ya utalii hapa nchini hatua itakayoisadia nchi kuongeza idadi ya watalii na
pato kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Utalii na Maliasili, Bw. Ezekiel Maige kuhusu ziara aliyoifanya nchini India iliyokuwa na lengo la kuhamasisha utalii, alisema kuwa kampuni hiyo imekubali kufanya utalii hapa nchini mwezi Julai ambapo jumla ya wafanyakazi 1,000 watashiriki utalii huo.
Kutokana na makubaliano hayo, alisema kuwa wanatarajia kuunda kamati itakayoangalia namna ya kuwezesha idadi hiyo kuja kutalii hapa nchini bila ya kukutana na kikwazo chochote.

Alisema kuwa kutokana na mkakati wa Wizara wa kutangaza nchi ya Tanzania hasa kwa sekta ya utalii yenye lengo la kutafuta masoko mapya ya utalii imefanya mazungumzo na watu mbalimbali nchini India kwa lengo la kuhamasisha utalii kwenye maeneo ya picha, mikutano, kujitangaza kwa njia ya usafiri na utalii wa matibabu.
Alisema kuwa katika mazungumzo hayo ilibainika kuwa kinachokwamisha utalii wa wananchi wa India hapa nchini ni kukosekana usafiri wa moja kwa moja hatua iliyowafanya wafikie hatua ya kufanya mazungumzo na Kampuni ya ndege ya JET ambayo imekubali kufanya safari za hapa nchini.

“Wenzetu tulizungumza nao na wakawa tayari kufanya hivyo, ila walichotuomba tusaidia katika upatikanaji wa kibali cha ndege za kampuni hiyo kutua Dar es Salaam na suala hili waliomba lifanyike hata ndani ya miezi sita,” alisema Bw. Maige.

 Mbali na hao, alisema kuwa alifanya mazungumzo na Hospitali ya Fortis ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini India ambayo kupitia ubalozi wa Tanzania nchini India itaandika barua rasmi ya kuomba kuweka kituo chake cha uchunguzi wa magonjwa jijini Dar es Salaam hatua itakayochangia ukuaji wa utalii hapa nchini.
Akizungumzia changamoto ya kukosekana kwa hotel za kukidhi mahitaji ya watalii wengi, alisema kuwa mpaka sasa kuna vyumba 27,000 vyenye sifa na endapo lengo la kupata watalii milioni moja litafikiwa basi kutakuwa na upungufu wa vyumba 3,000 hivyo akasisitiza Halmashauri mbalimbali kubaini na kutenga maeneo ya uwekezaji wa Hotel ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Kwa upande wetu hapa wizarani tunaendelea na kazi ya kubaini maeneo ya kuwekeza hivyo itafika mahali tutaondokana na tatizo hili,” alisema Bw. Maige.

No comments:

Post a Comment