04 March 2011

CHADEMA wamchangia mlemavu mil. 6/-

Na Suleiman Abeid, Bukoba

VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameomba wanancvhi kutowanyanyapaa na kuwabagua watu wenye
ulemavu nchini na badala yake wajenge utamaduni wa kuwasaidia kila pale inapowezekana.

Ombi hilo limetolewa jana na mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alipokuwa akikabidhi msaada kwa mlemavu wa miguu, Bi. Edna Katinga (20) mkazi wa Kijiji cha Kitendaguro Manispaa ya Bukoba  ambaye pamoja na mwanawe, Joanes George (5) ni walemavu wa miguu na hutembea kwa kutambaa chini.

Bw. Mbowe alimkabidhi Bi. Katinga sh. 6,393,000 ambazo zilichangwa na viongozi na wanachama wa CHADEMA wa mkoani Kagera katika hafla fupi ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na uongozi wa CHADEMA mkoani humo juzi usiku.

Katika kiasi hicho, Bw. Mbowe binafsi alichanga sh. 2,000,000 taslimu ambapo mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CHADEMA kutoka mkoa wa Morogoro, Bi. Regia Mtema alijitolea kumchangia mlemavu huyo shilingi 100,000 kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia hiyo juzi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa alijitolea kumpeleka mtoto Joanes katika hospitali maalumu ya watu wenye ulemavu wa viungo ya CCRBT iliyoko Dar es Salaam ambako atafanyiwa uchunguzi wa kitalaamu ili kuangalia uwezekano wa kumwezesha kutembea kawaida.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi msaada huo jana asubuhi, Bw. Mbowe alisema upo umuhimu mkubwa kwa jamii hasa kwa wana CHADEMA kujenga tabia ya kuwasaidia watu wenye ulemavu ili kuwawezesha wajione kwamba ni binadamu kama wengine.

Wakati huo huo, chama hicho kimesema hakina muda wa kumjibu waziri wa Uhusiano na uratibu Ofisi ya Rais, Bw. Steven Wassira kutokana na matamshi yake aliyoyatoa kuhusiana na maandamano ya CHADEMA kupitia kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1).

Akitoa tamko kuhusiana na kitendo hicho cha Bw. Wassira jana, mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema chama chake mbali ya kusikitishwa na kauli alizozitoa, hakitopoteza muda wa kujibishana naye kwa njia ya marumbano.

Alisema Bw. Wassira ameonesha jinsi gani yeye ni janga katika Taifa la Tanzania na kwamba kauli zake ndizo zinazoweza kuleta vurugu hapa nchini na siyo CHADEMA kama alivyodai.

Ndugu zangu Wassira ni janga la Taifa, kama Rais Kikwete anafikiria ana waziri, basi kuanzia leo afahamu kuwa hana waziri bali ana janga la Taifa, hakupaswa kutoa matamko aliyoyatoa jana (juzi). Yeye ni Waziri wa Mahusiano hapa nchini ni kiungo muhimu katika suala zima la amani na utulivu.

Leo kutoa matamko akidai maandamano yanayoendeshwa na CHADEMA huko katika mikoa ya kanda ya Ziwa yamelenga kuwachochea wananchi kukichukia Chama cha Mapinduzi (CCM) hakustahili kufanya hivyo, kutumia kejeli, dharau na vitisho hakujengi kitu, ni vyema angetumia busara zaidi iwapo aliona kuna tatizo, alieleza Bw. Mbowe.

Alisema viongozi wa CHADEMA wana akili na wanatumia busara katika kila jambo wanalolifanya hapa nchini na kwamba wanalipenda sana taifa kuliko kitu kingine chochote.

Tunasema hatuoni sababu ya kumjibu kwa maana siyo wa kiwango chetu, laiti kauli hiyo ingetolewa na Rais Jakaya Kikwete au Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda hapo tungekuwa na haki ya kutoa tamko rasmi la kuwajibu lakini siyo huyu Wassira.

Tunaomba asitufuate fuate, hatumuogopi isipokuwa tunamuheshimu, kwa kawaida penye tatizo watu husuluhishana kwa kutumia busara, siyo vitisho wala kejeli. Atuache asitulazimishe tuchukue maamuzi mazito, CHADEMA hatupendi tufike huko. Atuache kabisa, alisema Bw. Mbowe.

4 comments:

  1. safi sana chadema, safi sana mbowe! hii ndio aina ya chama tunachokihitaji..sio mavuvuzela ya sisiemu!! BAELEZEE BAELEWE! BAASIRA SIO BA SAIZI BETU!

    ReplyDelete
  2. ccm hapo mmechemsha! eti maandamano yatasababisha watu waichukie ccm! mbona imeshachukiwa hata kabla ya maandamano? rais unatakiwa kuchukua maamzi magumu juu ya wanachama wako a k a mafisadi. la cvyo unakiaribu kama c kukizika chama chako! kaza buti chadema mpaka kieleweke. tanzania bila ccm inawezekana.

    ReplyDelete
  3. keep it up mbowe !!
    Hii inaonyesha jinsi mlivyokomaa kisiasa na uwezo wakiongozi ambaye hutakiwa kutumia busara zaidi ya kuropoka fikiria kambla ya kujibu.

    ReplyDelete
  4. CCM hawana jipya la kuwaambia wananchi wa tanzania. tunahitaji chama kingine chenye watu maakini wanaoona matatizo ya wananchi na inchi kwa ujumla. Na daima mkumbuke amani tuliyokuwa nayo inaweze kutoweka tu kwa sababu ya ubabe wa CCM na si vinginevyo. kama Vitendo vya kubaka uchaguzi na matokeo yake. kuwanyima watu ya kweli n.k. CHADEMA big up mmeomyesha kuwajali hata ndugu zetu wenye ulemavu. Mungu awe nanyi daima. mnakopita hubirini pia kuondoa mgawanyiko wa kidini propaganda inayotuumiwa na CCM kutugawa watanzania.

    ReplyDelete