Na John Gagarini, Kibaha
WACHEZAJI wa Simba, wametakiwa kujiamini ili wapate ushindi kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) utakaopigwa
Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini juzi hapa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka alisema Simba wana uwezo kabisa wa kushinda mchezo huo kama watajiamini na kuondoa uoga kuwa wanacheza na timu kubwa Afrika.
Koka alisema kiwango cha Simba kiko juu na uwezo wa kufanya hivyo wanao kwani TP Mazembe, pamoja na kuonesha kuwa inaweza mpira, lakini inafungika bila ya wasiwasi na viongozi wawajenge kisaikolojia kwa kuwa uwezo wa kucheza soka la hali ya juu wanao, hivyo wasiingie uwanjani kinyonge.
“Wachezaji wa Simba wanapaswa kujiamini na kujituma, kwani mchezo waliouonesha kule Lubumbashi ulikuwa mzuri na kama wachezaji wangejiamini, basi hata kama wangefungwa ni idadi ndogo ya magoli, tofauti na magoli matatu waliyofungwa na wao kupata moja walionesha kuwa wanaweza,” alisema Koka.
Mbunge huyo alisema katika mpira, chochote kinaweza kutokea kwa kuweka mbinu mbalimbali za ushindi kwani miaka michache iliyopita, Simba iliweza kuitoa timu ngumu ya Misri ya zamalek jambo ambalo watu wengi waliona haliwezekani.
“Mpira unadunda kama, wao waliweza kutufunga kwao hata sisi hatushindwi kuwafunga kwetu kwani tutakuwa tukijivunia uwanja wa nyumbani na mashabiki wetu watumie nguvu na jitihada zao binafsi na kwa kutumia mafunzo ya Kocha Patrick Phiri, ambaye ana uwezo mkubwa,” alisema Koka.
Simba inapaswa kupata ushindi wa magoli 2-0 na kuendelea baada ya kufungwa magoli 3-1 kwenye mchezo wa awali uliochezwa wiki mbili zilizopita.
Mimi ni mpenzi wa YANGA. Lakini Simba nawapenda hasa mechi za kimataifa. Ninaungana na wapenzi wote wa mpira na wapenda soka kuiombea SIMBA iendelee vema dhidi ya hao TP MAZEMBE.
ReplyDelete