Na Elizabeth Mayemba
TIMU ya soka ya Simba, imepata pigo kwa beki wake wa kutumainiwa Joseph Owino ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa michezo iliyobaki ya Ligi Kuu bara, na
ikiwemo mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Cliford Ndimbo alisema baada ya daktari kumfanyia uchunguzi amegundua kwamba ameumia vibaya goti lake na hivyo anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
"Owino atakuwa nje mzunguko wote wa pili ikiwemo na mechi yetu ya klabu bingwa dhidi ya TP Mazembe,na muda wowote kuanzia sasa atafanyiwa upasuaji wa goti lake," alisema Ndimbo.
Alisema beki huyo aliumia sana goti na ndiyo maana hata alipopangwa katika mechi yao na Mtibwa Sugar, alijitonesha na hivyo kumsababishia maumivu makali.
Mbali ya mchezaji huyo, pia mchezaji Hilary Echessa naye anasubiri vipimo kutoka kwa daktari wao, ambapo ripoti yake inatarajiwa kutoka Jumamosi ijayo.
Wakati huohuo, timu ya Simba inashuka uwanjani leo kucheza na Ruvu Shooting mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kikosi cha timu ya Simba kiliondoka jijini Dar es Salaam juzi kwenda Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 38,huku vinara wa ligi hiyo, Yanga ambao wana pointi 39 na Ruvu shooting ipo nafasi ya sita baada ya kujikusanyia pointi 22.
Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri, alisema lengo lao ni kuondoka na pointi tatu ili waweze kushikilia usukani wa ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment