09 March 2011

Kaseba atamba Maugo katolewa kafara

Na Amina Athumani

BINGWA wa Dunia wa kickboxing Japhet Kaseba, ameibuka na kusema bondia Mada Maugo amenunua  ugomvi ambao si wa kwake na kwamba ametolewa
chambo katika pambano lao litakalofanyika April 16, mwaka huu.

Kaseba alisema endapo atapigwa na Maugo katika pambano hilo basi ataamua kuachana na mchezo wa ngumi kwakuwa itakuwa umri wake wa kucheza mchezo huo umekwisha na kuwahakikishia mashabiki wake kuwa atamtwanga Maugo kwa KO ili akaondoe ubishi kwa Cheka.

Pambano hilo la raundi nane litafanyika katika Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam ambapo mshindi kati ya Maugo na Kaseba atapambana na Francis Cheka katika pambano lisilo la ubingwa litakalofanyika mwezi Julai, mwaka huu.

Akitambulisha rasmi pambano hilo Dar es Salaam jana, promota wa ngumi za kulipwa, Halifa Kipao alisema  tayari mabondia hao wamesaini mkataba kwa ajili ya pambano hilo ambalo litafunguliwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania, IGP Saidi Mwema.

Alisema mbali na pambano hilo pia yatachezwa mapambano saba ya utangulizi huku pambano kati ya Yohana Robert na Saidi Zungu likiwa la kuwania ubingwa wa TPBO.
Mapambano mengine yatakuwa kati ya Fadhili Awadh na Bakari Dunda, Hasan Mandula atacheza na Uwesu Saidi, Joseph Martine atacheza na George Dimoso, Mohamed Matumla atacheza na Sadiki Momba, Deo Njiku atacheza na Issa Sewa na Kanda Kabongo atachuana na Maneno Osward.

Kipao amewataka wadhamini mbalimbali kujitokeza katika kudhamini pambano hilo ili kukuza viwango vya mabondia nchini ikiwa ni pamoja na kutoa udhamini wa kuwezesha mabondia wa Tanzania kupata mapambano nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment