09 March 2011

Siku 20 kumpa 'ulaji' Ulimwengu TP Mazembe

Na Zahoro Mlanzi

MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 (Vijana Stars) na Kituo cha Michezo cha ABC cha Swiden, Thomas Ulimwengu atakwenda
 kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa siku 20.
Ulimwengu ambaye yupo chini ya Wakala anayetambulika na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Damas Ndumbaro anatarajia kuondoka nchini Machi 11, mwaka huu na kufanya majaribio mpaka April Mosi, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema Ulimwengu pia alishafanya majaribio katika timu ya Dalkurd ya Swiden kabla ya kujiunga na kituo cha ABC.
"Hata hivyo licha ya kwenda kufanya majaribio kwa muda huo, shirikisho litaandika barua kwa Mazembe kuiomba wakati Vijana Stars ikiumana na Cameroon Machi 27, mwaka huu, mchezaji huyo awepo kulisaidia taifa lake," alisema Wambura.

Alisema mchezo huo awali ulipangwa ufanyike Machi 26 lakini ukasogezwa mbele kwa siku moja, hivyo ni fursa pekee kwa mshambuliaji huyo kuonesha uwezo wake na ana amini Mazembe watamruhusu kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema mpanda baiskeli wa kike kutoka Hispania, Joan Menendez amekabidhi seti mbili za jezi na mipira 11 kwa timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kutokana na kuhamasika na timu hiyo ilivyoonesha kiwango katika michuano ya Afrika.

Alisema hafla ya kukabidhi vitu hivyo vilifanyika jana asubuhi ambapo alimkabidhi Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenela Mukangara.
Alisema mpanda baiskeli huyo aliendesha baiskeli kutoka Dar es Salaam mpaka Kilimanjaro kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kusema kwamba alivutiwa na Twiga Stars wakati wa fainali za Afrika kwa wanawake zilizofanyikia Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment