07 March 2011

Simba, Yanga zaingiza mil. 240/-

Na Zahoro Mlanzi

MECHI ya watani wa jadi, Yanga na Simba uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi umeingiza sh. 243,017,000 kutokana na watazamaji 46,539 waliokata
tiketi kuishuhudia.

Kutokana na mapato hayo kila timu imepata sh. 51,194,793 baada ya makato mbalimbali ya gharama za mchezo kukatwa.

Timu hizo ziliumana juzi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1 ukiwa ni marudio baada ya mzunguko wa kwanza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba mapato hayo yametokana na kuuzwa kwa tiketi zote za viti vya kijani 19,648 na bluu 17,045.

"Maeneo ambayo tiketi hazikuuzwa zote ni viti rangi ya machungwa, Viti Maalum A (VIP A), VIP B na VIP C ambapo kati ya tiketi 748 sawa na viti 748, tiketi 309 ndizo zilizouzwa, hivyo ukichanganya mapato yote hayo unapata fedha hizo," ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya kuondoa gharama za mchezo na mgao wa uwanja, Kodi ya Ongezeko la Mapato (VAT), Chama cha Soka cha Mkoa (DRFA), TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) huku klabu zikipata sh. 51,194,793.

Katika mchezo huo viingilio vilikuwa ni sh. 3,000 (viti vya kijani), sh. 5,000 (viti vya bluu), sh. 7,000 (viti rangi ya machungwa), sh. 10,000 (VIP C), sh. 20,000 (VIP B) na sh. 30,000 kwa VIP A.

2 comments:

  1. INASHANGAZA MPK LINI TIMU ZA MPIRA BADO ZINANYONYWA? MAANA MAPATO MILLION 243,KILA TIMU MILL, 51 MAANA JUMLA 103 HIZO ZILIZOBAKI ETI GHARAMA ZA MCHEZO!! WAO SIO WALIOZIWEKA TIMU KAMBINI WALA POSHO ZAO SASA IWEJE WACHUKUWE PESA ZAIDI YA HIZO TIMU?HIYO ASILIMIA WANAYOIKATA WAPUNGUZE MAANA NI WIZI MTUPU

    ReplyDelete
  2. wabongo mnamatatizo mambo yenu ya siasa mnayaingiza kila sehem hiyo ni dalili ya kushindwa maisha na kuchanganyikiwa aliokuambia maendeleo ya timu au utajiri unatokana na mapato ya milangoni ni nani?ziambie tim zenu zilizo jaa na wanachama wenye uwezo mdogo nani wasioweza hata kumsajili mchezaji mmoja?mkitaka mapato makubwa jengeni uwanja wenu wenyewe kilakitu mnategemea alafu kulalamika kwingi du acheni hizo

    ReplyDelete