07 March 2011

Wakurugenzi kujibu maswali papo kwa papo

Na Theonestina Juma, Muleba

WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutenga muda takribani nusu saa hadi saa moja kabla ya kuanza kwa Baraza la
Madiwani kuwaruhusu kuuliza maswali ya papo kwa papo.

Bw. Pinda alisema hayo jana wakati akipokea taarifa ya Wilaya ya Muleba, iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Angelina Mabula katika Shule ya Sekondari ya Nyailigambwa Kata ya Muhutwe wilayani humo.

Alisema iwapo wakurugenzi watapanga muda maalumu kwa madiwani kuuliza maswali kabla ya kuanza vikao vya Baraza la Madiwani, yatawawezesha madiwani hao kujua mambo yanayoendelea katika halmashauri zao.

Alisema si lazima kuzama zaidi kwenye kanuni hata katika masuala ambayo ni ya muhimu.

Alitoa mfano wa bungeni kupitia kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, yameonesha ni jinsi gani serikali ilivyojipanga katika kutatua matatizo ya wananchi.

Alisema mfano kama masuala ya barabara fulani iliyoko katika kata yake ama sehemu fulani diwani akiuliza katika maswali ya papo kwa popo huweza kumfanya mkurugenzi kutoa majibu ya uhakika tofauti na pale ambapo diwani angemfuata na kuanza kumpa majibu yasiyostahili, kama 'tuko mbioni kuijenga'.

Alisema lengo la kusema hivyo ni kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia wananchi katika harakati za kujiletea maendeleo.

Hata hivyo, Bw. Pinda alisema madiwani wanatakiwa kumpelekea mkurugenzi maswali mwezi mmoja kabla ya kikao cha Baraza la Madiwani kufanyika ili kumwezesha kuyatatafutia majibu mapema na ikibidi wawabane kwenye kikao ili kutoa majibu ya uhakika.

No comments:

Post a Comment