Na Zahoro Mlanzi
Tambo na majivuno ya mashabiki wa timu za Yanga na Simba, zilifikia tamati juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kupigwa mchezo wa marudiano
wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Katika mchezo huo, timu hizo hazikuweza kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 huku bao la kusawazisha la Simba lililofungwa na Mussa Hassan 'Mgosi' dakika ya 73 likileta mtafaruku uwanjani hapo.
Bao hilo ni moja kati ya matukio matano ya kusisimua katika mchezo huo, ambao ulihudhuriwa na mashabiki lukuki wengine kutoka mikoa ya jirani hapa nchini.
Mchezo huo ni wa nne kwa timu hizo kukutana katika msimu wa 2010/2011 ambapo, Yanga inaonekana kuongoza katika msimu huu kwa kuifunga Simba mara mbili katika ligi na mara moja kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.
Yanga iliifunga Simba mara ya kwanza jijini Mwanza katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, kwa 1-0 na pia zilikutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulifanyika kabla ya ligi kuanza, ambapo wana-Jangwani hao walishinda kwa changamoto ya penalti 3-1.
Simba ilifuta uteja huo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga mabao 2-0 na wa mwisho ndiyo wa juzi ambapo zilifungana bao 1-1.
Yafuatayo ni matukio muhimu ya kukumbukwa katika mchezo huo:
Davies Mwape vs Juma Nyosso,
hakika kwa yeyote aliyekuwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo, sina shaka wachezaji hawa wawili utaona ni jinsi gani walivyokuwa wakichezeana ubabe.
Mwape alikuwa na kazi moja tu kuhakikisha anaifungia Yanga mabao na kwa hakika alifanikiwa kwa asilimia 57, kwani kama si juhudi binafsi za kutumia nguvu na akili asingeweza kusababisha penalti iliyofungwa na Stephane Mwasika.
Nyosso naye hakutaka mchezo alikuwa na kazi moja tu ya kumficha Mwape, ili ajihakikishie namba katika kikosi cha kwanza.
Wachezaji hawa wote wanatumia nguvu nyingi na ndicho kitu kilicholeta picha tofauti katika mchezo huo.
Jeryson Tegete vs Kelvin Yondani,
kiukweli wachezaji hawa unaweza ukaona hakuna walichofanya katika mchezo huo, kwani hawakuonekana kabisa kutokana na kazi zilizofanywa na Nyosso na Mwape.
Tegete alishindwa kuonesha cheche zake kabisa zaidi ya shuti moja, alilopiga kipindi cha pili nje ya eneo la hatari na kupanguliwa na kipa Juma Kaseja.
Yondani anayejulikana zaidi kwa jina la Vidic, hakuwa na makuu zaidi ya kuharibu mipira yote aliyopigiwa Tegete, hakucheza kibabe kama alivyotarajiwa.
Nadir Haroub 'Canavaro' vs Mbwana Samatta nao
tukio lingine la kusisimua ambalo lilikuwa kati ya wachezaji hao, ambapo kama si ubabe na akili za Canavaro, basi wana-Jangwani hao wangekuwa na simanzi kubwa siku ya juzi.
Samatta hakupewa nafasi kabisa ya kuchezea mpira kwani kila alipogusa, Canavaro alifika miguuni na kutibua mipango na alipata nafasi tatu, zikiwepo kichwa kilichopaa juu na mashuti mawili yaliyotoka nje.
Mshambuliaji huyo chipukizi wa Simba, kila wakati aliomba huruma ya mwamuzi ili amsaidie kutokana na shughuli nzito ya Canavaro na si yeye tu, hata wachezaji wenzake walikuwa wakimuombea huruma ya mwamuzi.
Juma Seif 'Kijiko' vs Jerry Santo
nathubutu kusema viungo hawa katika mchezo huo, ndiyo waliong'ara kutokana na uhodari wao wa kupiga pasi ndefu na kufungua kuomba pasi, huku wakiwa hawajapoteza pasi.
Kijiko ambaye alicheza kama kiungo mkabaji alionekana kutawala eneo la kati na kupandisha timu, huku akipiga pasi zenye uhakika kitu kilichomfanya azibe pengo la Ernest Boakhye.
Santo naye kama Kijiko huwa hana mambo mengi uwanjani zaidi ya kukaba na kushambulia na kuna wakati alipandisha timu na kupewa pasi, lakini shuti alilopiga lilitoka nje, ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi kwa upande wa Simba.
Kigi Makasi vs Haruna Shamte
kama si kuwa makini katika kuangalia wachezaji hawa walivyokuwa wakicheza, unaweza kusema hawakuwa na kazi kubwa uwanjani.
Ukiangalia kwa makini mashambuliz mengi ya Yanga yalipelekwa upande wake wakiamini kuwa kasi na uwezo wa kumiliki mpira ungeleta madhara kwa Simba.
Lakini haikuwa rahisi kwa Shamte ambaye kila wakati alifika miguuni kwa Kigi na kuondosha hatari kama si akili za ziada na nguvu alizonazo, hakika mashabiki wa Simba wangekuwa wakizungumza mengine.
No comments:
Post a Comment