LONDON, Uingereza
MSHAMBULIAJI Mario Balotelli, anajindaa kupata adhabu nyingine kwa kutozwa faini katika mshahara wake wa pauni 100,000 na ameonywa na wakuu wa
Manchester City kutokana na tabia yake na sasa mchezaji huyo anaonekana kuwatokea puani mabosi wake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20, anakatwa fedha za faini kwenye mshahara wake kutokana na kuwamwagia vumbi wachezaji wa timu ya vijana waliokuwa kwenye uwanja wa mazoezi, kutoka kwenye chumba chake kilichopo ghorofani.
Adhabu hiyo itakuja huku wiki mbili zilizopita, akiwa amepewa adhabu kwa kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi ya Ligi ya Europa kwenye mechi dhidi ya Dynamo Kiev.
Sasa atawekwa kiti moto na kocha, Roberto Mancini na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo kuhusu tabia yake isiyokubalika.
Maofisa wa City awali walikuwa na furaha naye wakieleza kuwa ni kijana, anakomaa na amekuwa akijaribu kuzoea soka ya England baada ya kuhama Italia.
Lakini tukio alilofanya hivi karibuni limewakasirisha mabosi wa City, ambao wameanza kuhisi kuwa ilikuwa ni makosa kwao kumsaini kwa pauni milioni 24 kutoka Inter Milan.
Matendo ya Balotelli, yanadhihirisha kuwa ilikuwa ghari kutokana na faini alizotozwa ambazo zinafikia pauni
300,000.
Balotelli amefunga magoli 10 katika klabu yake, tangu ahamie na anaonekana kuiletea matatizo City. Kabla ya kuanza kuichezea alikuwa majeruhi na alikaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu, kisha alipata kadi nyekundu katika mechi zake mbili za mwanzo.
Aliwahi kugombana mazoezini na Jerome Boateng na kukasirika baada ya kutolewa katika mechi dhidi ya West Ham na Notts County.
Moja ya vituko alivyofanya wakati akiwa majeruhi italia ni kuingia katika geti la gereza la wanawake, akieleza kuwa alitaka tu kuona ndani kukoje.
Uwanjani ameshapata kadi za njano tisa na mbili nyekundu.
Hakuna mtu alikuwa majeruhi kwa siku za karibuni. Lakini kurusha vumbi kunaonekana kunaweza kufanya akachukuliwa hatua za kinidhamu.
No comments:
Post a Comment