Na Peter Mwenda
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Bw. Leonidas Gama amesisitiza kuwa serikali haitalipa fidia ya fedha taslimu kwa waathirika wa mabomu ya Gongolamboto badala yake
itawajengea nyumba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bw. Gama alisema waathirika wakilipwa fidia wengi wao hawataitumia ipasavyo na kuwanufaisha wengine ambao hawastahili malipo hayo.
"Tumejifunza fidia ya mabomu ya Mbagala ambako watu wamelipwa fedha ambazo si zao na kuwaacha waathirika, wengine walilipwa fidia zao lakini bado mpaka sasa wanaishi katika mahema," alisema Bw. Gama.
Waathirika wa mabomu ya Gongolamboto katika mkutano na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam juzi waligoma serikali kuwajengea nyumba kupitia kampuni ya Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT).
Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya alisema kazi ya ukarabati wa shule na zahanati umeanza ambako Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inaanza ukarabati wa Zahanati ya Kivule iliyopigwa bomu na kuharibu chumba cha wazazi.
Bw. Gama alisema TBL ukarabati huo unafanyika ili kurejesha huduma za uzazi katika zahanati hiyo ambayo ilisimamisha kutoa huduma.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivule, Bw. Joseph Gassaya alisema huduma za uzazi zilisimama baada ya bomu kupasua mabati na kuvunja chumba cha wazazi na kusababisha nyufa.
Mmoja wa waathirika wa mabomu hayo, Bw. Arthur Lyatuu mkazi wa Kinyerezi alisema nyumba yake haikuteketea kama waathirika wengine lakini akisubiri mpaka serikali imjengee ataingia hasara kubwa kwa sababu mvua zikianza maji yataingia ndani na kuozesha mbao na vifaa vingine.
Alishauri serikali ithamini nyumba zilizopata madhara kidogo na kuruhusu wahusika wajenge kwa gharama zao na baadaye serikali iwalipe.
WANAOKATAA WANA ZAO HILA ZA KUWADHULUMU WENGINE HAPO MUHIMU SUMA JKT WAJENGE KWA UADILFU NA UMADHUBUTI WASILIPUWE HIYO ITAKUWA NJIA SAHIHI TENA NASHANGAA MPK SASA NILITEGEMEA ANGALAU NYUMBA ZAIDI YA 15 ZIWE ZIMESHAKARABATIWA AU KUJENGWA KABISA WAFANYE HARAKA SANA MAANA MVUA ZIKO KARIBU KABISA KUPOROMOKA MAANA ZIMESHAANZA
ReplyDelete