08 March 2011

Pinda ataka Biharamulo ibaini vyanzo vya mapato

Na Mwandishi Wetu, Kagera

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya utendaji kazi katika wilaya ya Biharamulo ambayo iliwasilishwa kwake leo
asubuhi mara baada ya kuwasili
wilayani hapa akitokea Chato.

Waziri Mkuu alitoa maelezo hayo ya kutoridhishwa jana wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera mara baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya,Bw. Ernest Kahindi.

“Taarifa ya Wilaya haijibu maswali ambayo nilitaka nipate majibu yake ... ukiipitia kutaka kujua mmepata pembejeo zipi au matumizi ya mbolea katika wilaya hii yakoje,vyote huvioni,” alihoji.

Waziri Mkuu alisema Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wanapaswa kujiuliza ni kwa nini waliteuliwa na kupelekwa Biharamulo kufanya kazi hiyo lakini pia alitaka wajiulize katika eneo walilokabidhiwa kuongoza, kuna watu na ardhi ambayo ni rasilmali zinazohitaji kusimamiwa.

“Jiulize watu niliokabidhiwa ni wangapi, nilipokabidhiwa niliwakuta wana hali gani? Je wanajishughulisha
na kazi zipi? Na wewe una mpango gani wa kuwaendeleza? Je kuna fursa zipi za kuwaendeleza? Umefanya nini ili kuwawezesha? Na kuna vikwazo gani unakumbana navyo katika kumsaidia mwana-Biharamulo?,” alisema Waziri Mkuu. 

“Taarifa hii haioneshi DC, Mkurugenzi na timu yenu mmejipanga vipi kumsaidia mwananchi wa wilaya hii,” alisema.

Alipoulizwa ni upi wastani wa pato la mwananchi wa Biharamulo kwa mwaka, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Zuberi Mbyana alijibu kuwa hana uhakika bali anakisia kuwa ni sh. 100,000 ndipo Waziri Mkuu aliposema hataki makisio na kumwita Ofisa Mipango wa Wilaya aliyejibu kuwa ni sh. 420,000 kwa mwaka.

“Kwa kiwango hiki wastani wa pato la mtu kwa mwezi ni sh. 35,000 sawa na sh.1.167 kwa siku... utaakaje na kusema unaongoza watu wakati pato lao liko chini hivyo nawapa kazi DC, Mkurugenzi na timu yenu kaeni chini na mbungue bongo na kuangalia vigezo vyote nilivyovianisha,” alisisitiza.

Akiwaeleza kasoro nyingine katika taarifa yao, Waziri Mkuu alisema hawakutoa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi licha ya kuwa wameonesha idadi ya wakazi wa wilaya.

“Kutojua idadi ya nguvu kazi uliyonayo ni tatizo katika kupanga mipango ya maendeleo ya wilaya yako...” alisema.

Matatizo mengine aliyabaini katika majedwali ambako mapato ya Halmashauri yanaonesha hadi kufikia Januari 31, 2011 wamekusanya asilimia 30 tu ya lengo walilojiwekea.

“Mapato yenu hadi Januari mwaka huu ni sh. milioni 939.9 na ninyi hadi sasa mmeshakusanya sh. milioni 294.8 katika miezi mitatu iliyobaki mtafikisha lengo kweli? Mna muujiza gani?” alihoji.

Alipoulizwa wana mkakati wa kutimiza lengo na siku zilizobakia ni chache, Mkurugenzi huyo
alijibu kuwa wanasubiri kiasi cha sh. milioni 260 ambazo ushuru kutoka kwenye mgodi wa Tulawaka na kiasi kingine kitatokana na misako ya wanaovuna mali za
misitu kinyemela.

Waziri Mkuu aliwataka waangalie makusanyo kutoka katika vyanzo vya mapato halisia ambavyo vinatokana na uzalishaji kuliko kutegemea ushuru au faini za watu wanaovuna
mazao ya misitu kinyemelea.

“Watu wasipoenda msituni mtapata wapi hizo hela au mkituma maofisa wenu, wakakamatwa na wahalifu na hizo hela wakazitia mfukoni, nyie Halmashauri mtazipataje?,” alihoji.

Kutokana na hali hiyo, aliwashauri wakae na kuangalia vyanzo vyao vya mapato katika miaka ya nyuma vilikuwa ni vipi na wajiulize kwa nini wameacha kuvitumia ili kubaini mapungufu yaliyochangia hali hiyo ya kushindwa kukusanya mapato kama walivyopanga.

3 comments:

  1. Tunamshukuru waziri mkuu kwa kuliona hili linalotokea kwa wana Biharamulo. Ukweli ni kwamba viongozi waliokabidhiwa wilaya ili walete mwanga na suluhisho kwa matatizo yaliyopo, wamekiuka mkataba wao kwa kutenda hayo, na badala yake wamekuwa wakishughulikia yale yanayogusa maslahi yao! matokeo yake wananchi wamepoteza matumaini na kukata tamaa. Kama watajirudi, ujio wa waziri mkuu utakuwa umeleta suluhisho.

    ReplyDelete
  2. MIMI NINACHOKIONA NI WAZIRI MKUU KUWA MULALAMISHI BADALA YA KUWACHUKULIA HATUA KWA KUSHINDWA KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI.KAMA PM ANALALAMIKA JE SISI WANANCHI TUTAFANYAJE? JIBU NI KWENDA KULALAMIKA KWA CHADEMA WATUSEMEE KWA KAULI YA PEOPLES POWERRRRRRRRRRRRRRRRRRRR!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  3. waziri, maswala ya janga la kitaifa ambayo inabidi kuyamaliza selikari kuu yanasababisha kuzorota na bila kuwatia hofu wa ngazi za chini kupanga vizuri mikakati nao wakijinyakulia kilichokuwepo ili watakapong'oka wawe na chao; kama vile umeme, kuingia mikataba mibovu kwa manufaa ya vigogo na mabomu kulipuka ovyo, hii inaonyesha kusipo usiliasi kuanzia huko juu na baadaye kumkamata mwizi wa kuku na kumsalimisha kigogo wa mabilion ya kuwatosha wananchi wote na wakawa na maisha mazuri.

    ReplyDelete