Na Mwandishi Wetu, Kagera
ASKARI mstaafu wa Jeshi la Polisi, Bw. Paulo Bundala ameiomba serikali iangalie uwezekano wa kuwatumia askari polisi waliostaafu ili wasaidie
kukabiliana na wimbi la ujambazi kwani baadhi yao bado wana nguvu.
Askari huyo alitoa ombi hilo mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Chato mkoani Kagera ambako Waziri Mkuu alitoa nafasi ya wananchi kuuliza maswali.
“Askari wastaafu tufikiriwe na kuitwa kwa mkataba ili tusaidie kuzuia uhalifu wa mipakani, mbona walimu wakishastaafu wanaitwa tena kazini kuziba upungufu? Hapa kuna mapori na ujambazi unatokea kila mara, tunaweza kusaidia kupunguza matukio hayo kwa sababu baadhi yetu bado tuna nguvu,” alisema.
Bw. Bundala pia aliomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia wakazi wa Chato umeme wa kuvuta kutoka Geita badala ya kuendelea kutegemea ule wa jenereta unaotoka Biharamulo ambao kila mara huwa unakatika.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema suala lake la kuajiriwa kwa mkataba halina tatizo kwani kwa kutumia sera ya ulinzi shirikishi, polisi waliostaafu wanaweza kusaidia kutumika kuimarisha ulinzi wa raia na kwamba uongozi wa mkoa pamoja na polisi waangalie uwezekano huo.
Kuhusu umeme, Waziri Mkuu alikiri kwamba umeme unaotoka Biharamulo hautoshi kwa sababu jenereta iliyopelekwa huko haikuwa mpya. “Dawa ni Chato kuwa na jenereta yake kwa sababu jenereta iliyopo Biharamulo siyo mpya, kwa hiyo siyo rahisi kutoa umeme wa kutosha,” alisema.
Akijibu swali la mkazi mwingine wa Chato, Bw. Marko Manyaga aliyetaka kujua ni kwa nini wana kero ya maji wakati ziwa liko karibu na mji wa Chato, Waziri Mkuu alisema anatambua kuwa maji bado ni tatizo lakini ni lazima watambue kuwa maji siyo suala la kuchota tu ziwani na kuleta watu wanywe.
“Maji ni lazima yasafishwe kwa madawa ili mtumiaji asipate shida... ahadi ya kuleta maji safi ipo, itachukua muda lakini mwishoni mtapata maji safi na salama kwani upo mradi mkubwa wa maji wa sh. bilioni tatu... tulilenga kukamilisha kwanza ule wa Shinyanga kabla ya kuanza mradi mwingine mpya,” alisema.
No comments:
Post a Comment