18 March 2011

Maiti za wagonjwa wa Babu zatupwa porini

*Ni baada ya gari kupata ajali, wenye nalo kukimbia

Na Peter Saramba, Arusha

IMEBAINIKA kuwa Mzee Piniel Kingori aliyepotea baada ya kupata tiba Loliondo na mwili wake kukutwa umezikwa poririni katika Kijiji cha Ngaresero wilayani
Ngorongoro alikufa kwa ajali ya gari na mwili wake kutupwa porini na wafanyakazi wa gari alilokuwa akisafiria.

Mmoja wa ndugu waliokwenda Loliondo kumtafuta mzee huyo na kufanikiwa kupata mwili wake uliozikwa na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro baada ya kutotambulika maeneo yote ya karibu, alisema ilibainika kuwa marehemu alikuwa amevunjika mkono na majeraha kichwani katika ajali iliyohusisha gari aina ya Landcruiser ambalo halikutambulika.

Ndugu huyo Bw. Richard Njavai alisema kwa mujibu wa maelezo waliyopata kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo ambalo ni katikati ya pori, pamoja na marehemu kuna watu wengine wawili waliokufa katika ajali hiyo na miili yao kutelekezwa porini na wenye gari pamoja na abiria wengine baada ya kutotambulika.

Katika ajali hiyo walikufa watu watatu ambao ni Mzee King'ori, mama mmoja mwenyeji wa Kilimanjaro ambaye ndugu zake walichukua mwili wake na mtu mwingine aliyedaiwa kuwa ni Mzanzibari ambaye mabaki yake yalichukuliwa na ndugu kwenda kuyazika baada ya kuliwa na wanyama, alisema Bw. Njavai.

Alisema ajali hiyo ilitokea Saa 3 usiku Machi 4, mwaka huu, siku ambayo marehemu King'ori na mwenzake walifika Loliondo na kukutana na foleni kubwa ya kwenda kunywa dawa, hali iliyomlazimu mzee kujipenyeza na kufanikiwa kunywa dawa na kuwaacha wenzake aliokwenda nao, kisha akapanda gari lingine lisilojulikana kurudi Arusha.

 Alisema kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Bw. Elias WawaLali, baada ya taarifa za kuwepo miili ya watu waliokufa kupatikana, mwili wa marehemu ulipigwa picha na kusambazwa vijiji jirani ili wananchi wamtambue lakini njia hiyo haikufua dafu ndipo ulipoamuliwa uzikwe Jumatano iliyopita, siku tano baada ya ajali.

Jambo la kusikitisha ambalo ni la kinyama kufanywa na binadamu kwa mwenzake ni kwamba abiria anakufa kwenye ajali na mwili wake unatupwa porini, alisema Bw. Njavai akifuta machozi.

Alishauri serikali iandae utaratibu utakaowezesha abiria wote wanaosafiri kwenda na kutoka Loliondo majina yao kuandikwa ili kudhibiti unyama wa aina hiyo kuendelea kufanyika kwa watu wengine.

Mzee Kingori alizikwa rasmi jana kwa heshima zote katika makaburi ya familia eneo la Kijiji cha Sekei wilayani Arumeru baada ya mwili wake kuletwa usiku wa kuamkia juzi baada ya kufukuliwa na ndugu zake chini ya usimamizi na uratibu wa uongozi wa wilaya ya Ngorongoro na Jeshi la Polisi.

Juhudi za kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Wawa Lali kuzungumzia tukio hilo kwa undani hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana.

12 comments:

  1. Inasikitisha sana kusikia unyama kama huu.

    ReplyDelete
  2. Gari lililo tupa maiti hizo ni cruiser inayo safirisha watalii japo sina namba zake. Walikufa 5 hapo hapo na wengine kujeruhiwa. Dereva halali wa gari hilo alimpatia rafiki yake kuwapeleka watu kwenda kunywa dawa ya Babu, njiani walipata ajali, dereva huyo bandia alikimbia lakini alimuarifu dereva halali aliye muazima gari juu ya huo mkasa wa ajali. Dereva halali aliamua kukimbilia kwao milimani, Usangi. alipanda gari mjini Arusha saa 9.00 tulikaa kiti kimoja akiwa amechanganyikiwa, nilimdadisi sana akanieleza mkasa mzima wa watu 5 kufariki na mwenzie kukimbia na hiyo na yeye alikuwa anakimbia ili mwenye gari akajibu mashitaka. Nilimripoti kwenye polisi doria wa King'ori ambao walimuweka chini ya ulinzi, ushahidi ninao, yaelekea hao polisi walipewa hongo na kumuachia, walichukua namba yangu ya simu na sijasikia lolote toka kwao kwani niliwaeleza kisa cha huyo jamaa kuazima gari, gari kuua, na yeye na mwenzie kukimbia mkono wa sheria kwa kwenda kujificha. Polisi walio kuwa barabarani doria king'ori tarehe 12/03/2011 saa 10.00
    wanajua walifanya nini na mtu huyu aliye telekeza maiti za watu porini nahisi wengine waliliwa na wanyama kama fisi na simba marara wa eneo husika. Huu ni unyama na kama hao polisi walinyamaza mimi niko tayari kuwatambua mahakamani kwa kumuachia huyo muuaji.

    ReplyDelete
  3. Ndugu ninakupa pole kwa msiba uliokupata.Ninaomba umshukuru mungu kwa tukio hilo,ninachokuomba mwachie mungu kwa muuaji huyo muuaji atapata malipo yake muda sio mrefu kuanzia hivi.Wala usihangaike kwenda Polisi wala kwa mkuu wa Wilaya.Kisasi ni juu ya Bwana.

    ReplyDelete
  4. Du....!!!!!!!!!! jamani, sipati picha...!Eee Mungu aturehemu

    ReplyDelete
  5. Watu wanamlaumu babu kwa lipi hapa. Waliosababisha ajali awausiani na babu. Babu anaingiaje hapa. Let us be objective.

    ReplyDelete
  6. MWANDISHI UNAVURUGA mada. maiti zimezikwa kijijini baada yakukosa ndugu na kuanza haribika au zimetupwa???

    ReplyDelete
  7. kwani babu kalaumiwa?na waliohusika wote wachukuliwe hatua pamoja na hao askari wa king~ori

    ReplyDelete
  8. Natoa shukurani nyingi kwa ndugu aliye toa habari kwa Polisi wa King'ori na kumripoti huyo dereva halali aliyetoroka. Mungu akuzidishie kila la kheri na uwe na utu daima. Jambo kama hili sio la kunyamazia au kupuuzia kwani iwapo Roho yako itakupa upuuzie jambo la kinyama kutendeka kwa Binadamu mwenzio maana yake pia wewe una Roho ya kinyama isio na huruma.

    ReplyDelete
  9. Mungu anaanza kutulipa malipo kwa kumsingizia ametuletea dawa ya ukimwi! Tunahamasisha ufuska kwa vijana kwa imani kuwa dawa ipo kwa babu! Tutasikia mengi wee ngoja tu muda ndio mwalimu wa kweli!

    ReplyDelete
  10. Kwa faida ya mchangiaji wa tarehe 18 march 6:
    20 am, mwandishi hajakosea, maiti walitupwa na wenye gari ndio huyo mzee akazikwa na kijiji wakati mwingine kaliwa na wanyama

    ReplyDelete
  11. nawapa pole sana wote waliofikwa na hili. lakini kuna mengi yakujiuliza hapa. mwandishi anasema walitupa maiti na wahusika wa gari kukimbia, je gari husika liko wapi? mmiliki wa gari hajajulikana kumtambua dereva halali? hao viongozi walioshughulika na utambuzi mpk kuzika maiti kijijini walifanya juhudi za kupeleka hzo picha kwa babu? bila shaka hapo kuna watu wangeweza kutoa msaada hata wa utambuzi wa gari husika na mengineyo.
    polisi nao waliopewa taarifa na mtoa maoni hapo juu siwanajulikana? kwa nn wasihojiwe watueleze nn kilitokea?

    ReplyDelete
  12. mungu ndiye anaewapa watu uwezo wa kuponyesha popote ulipo na hatutakiwi kumuamini mtu na kumpa sifa za mungu ndo maana wanaoenda loliondo wengi wapata maafa lakini hawafikirii watu wapumbaza kwa taarifa za uongo zinazosambazwa za babu kuponyesha.

    ReplyDelete