Na Rabia Bakari, Kondoa
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Bw. Mustafa Sabodo amefadhili uchimbaji wa visima 10 vya maji safi katika wilaya ya Kondoa ili kutatua tatizo la maji ambalo ni
tatizo sugu wilayani humo.
Msaada huo wa visima unahusisha uchimbaji, pamoja na ufungaji wa pampu za maji ambao umegharimu zaidi ya sh. milioni 200, sanjali na kulipa wataalamu kutoka Wizara ya Maji ili kufanikisha mradi huo kitaalamu zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa katika ziara ya kutembelea uchimbaji wa visima hivyo, Mbunge wa Kondoa Kusini Bw. Juma Nkamia alisema kuwa visima hivyo vitakamilika ndani ya mwezi mmoja, na ni moja ya mikakati ya kuondoa tatizo la maji kwa asilimia 70 mpaka ifikapo 2015.
"Baada ya kupata msaada wa visima kutoka kwa Bw. Sabodo, sikuwa mchoyo, visima viwili nilipeleka katika Jimbo la Kondoa Kaskazini kwa sababu ninatambua kuwa, maji ni tatizo kubwa kuliko matatizo yote yanayoikabili Kondoa nzima.
"Namshukuru sana Bw. Sabodo, kwa sababu hata wakati naingia bungeni niligawa mikakati ya kiutendaji kwa makundi, na kundi la kwanza kulifanyia kazi lilikuwa ni maji, kwa hiyo kazi ndo inaanza, na mpaka ifikapo 2015 nitahakikisha tatizo hilo lipo robo yakumalizika,” alisema Bw. Nkamia.
Baadhi ya vijiji ambavyo vimepata ufadhili wa kuchimbiwa visima na Bw. Sabodo, ni Chemba, Ombiri, Lyori, Chang’ombe, Itolwa, Mlongia, Jangalo, Mapango, Kimkima na Gonga.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Isdori Mwalongo alisema kuwa kampuni iliyopewa tenda ya kuchimba visima hivyo ya Aqua Well Drilling imetoa msaada wa kuchimba kisima kimoja na hivyo kufanya idadi ya visima kuwa 11.
”Tatizo la maji hapa Kondoa ni tatizo kubwa sana, kwani mpaka ni asilimia 34 tu ya wakazi ndio wanaopata maji safi, ambapo kwa hali hiyo tunakuwa nyuma sana ya Malengo ya Milenia ya kuwafikia watu asilimia 65 hadi 70.
”Juhudi za wabunge kama Bw. Nkamia, kuomba wafadhili kutoka sehemu mbalimbali ni moja ya mikakati ya kumaliza tatizo la maji katika wilaya yetu, ikiwemo bajeti ya halmashauri, mfuko wa jimbo, wafadhili kama TASAF, na wengineo sambamba na miradi ya maji vijijini ni fursa tunayotaka kuitumia vizuri sana,”aliongeza Mkurugenzi huyo.
Mhandisi wa maji wilayani hapo Bw. Robert Mganga alisema uhaba wa maji unasababishwa na hali ya ardhi ya ukame Kondoa, na maji kuwa kina kirefu sana kutoka chini na hivyo kufanya upatikanaji wake kuwa shida.
No comments:
Post a Comment