21 March 2011

CHADEMA: Hatukusudii kuipindua Serikali

Na Tumaini Makene

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hakina nia, ajenda wala lengo la kuipindua serikali iliyoko madarakani kwa njia ya
maandamano, bali hofu na woga alionao Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine inatokana na kushindwa kutekeleza ahadi na kuwajibika kwa wananchi.

Kimesema kuwa pamoja na kuenezwa propaganda hiyo ya kupindua serikali, na nyingine kama za kuvuruga amani ya nchi, ukabila, udini na kufadhiliwa, hakitaacha kufanya kazi yake ya siasa ya kuiwajibisha serikali, kwa kusimamia hoja za wananchi juu ya mwenendo wa nchi na viongozi wao.

Kimesema maandamano ya amani yanayotumika kuishinikiza serikali kuwajibika kwa wananchi si kuhatarisha amani ya taifa, "bali kwa viongozi wabovu wa CCM na serikali yake wanaohofia nguvu ya umma ya Watanzania wanaoanza kuamka, kuelimika na kuhoji juu ya mwenendo wa serikali na viongozi wao".

Kimesema pia kuwa kamwe hakitakubaliana na hila za aina yoyote zinazofanyika kulitia taifa aibu ikiwemo kutaka kubadilisha Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ili serikali inunue vifaa chakavu na kuingia biashara ya aina yoyote na kampuni tata ya Dowans.

CHADEMA kimesema kuwa kitaendelea kutumia 'majukwaa' yote mawili, ndani na nje ya bunge, kutetea maslahi ya Watanzania na nchi kwa ujumla, kikisema kuwa hayo ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote kile, hasa katika eneo la nishati ya umeme, ambako kimedai kuwa kuna miradi ya kitapeli inaibuliwa kila kukicha kwa faida ya 'wachache wanaotengeneza mabilioni ya bure.'

Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe alipokuwa akitoa tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA, ambapo alisema "kauli za Rais Kikwete kwamba maandamano haya yalilenga kuiondoa serikali iliyo madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia ni uzushi na uwongo."

Alisema kuwa amani wanayozungumzia viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Rais Kikwete kuwa itavurugwa, wakihofia kazi ya kisiasa inayofanywa na CHADEMA "ni amani ya CCM na viongozi wake ambao kwa miaka yote walizoea kuishi kana kwamba nchi ni mali yao, badala ya kujiona kuwa ni watumishi wa wananchi waliowachagua kuongoza".

Tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA lilisomwa na Bw. Mbowe akisaidiana na Katibu Mkuu wake, Dkt. Willibrod Slaa katika kujibu maswali ya waandishiwa habari, lilijikita katika maeneo kadhaa, ambayo ni kuhusu maandamano ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, maandalizi ya ziara na maandamano mengine katika mikoa mitano ya Nyanda za Juu Kusini na Uchaguzi wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA).

Maeneo mengine yalikuwa ni kuhusu vitisho vya kuuawa kwa Dkt. Slaa na viongozi wengine wa kisiasa nchini, suala la uchaguzi wa Meya Arusha, tatizo la umeme nchini, suala la mabomu ya Gongolamboto, janga la tsunami huko Japan, uamuzi wa serikali kuandaa mswada wa kubadili Sheria ya Manunuzi ya Serikali;

Pia azma ya serikali kuwekeza katika uchimbaji wa uranium, mikakati ya kukabiliana na janga la njaa linaloikabili nchi kwa sasa na suala la kupanda kwa deni la taifa kwa kiwango cha asilimia 18 ndani ya mwaka mmoja.

"Kamati Kuu imesisitiza kuwa CHADEMA ni chama cha kidemokrasia na kitaendelea kutafuta ridhaa ya wananchi ya kuunda serikali kwa njia ya kidemokrasia na kwa mujibu wa sheria za nchi na wala haina dhamira ya kuiondoa serikali kwa njia zisizo za kidemokrasia.

"Kamati Kuu ilipokea na kujadili kwa umakini tathmini ya maandamano yaliyofanyika kanda ya ziwa, pamoja na matamko yaliyotolewa na viongozi wa serikali na CCM, wakiwemo Rais Kikwete, mawaziri Bernard Membe, Stephen Wasira, Sophia Simba na John Chiligati...Kamati Kuu imesikitishwa na kauli zilizotolewa na viongozi hao wa serikali na CCM.

"...zinaashiria kuwa viongozi wa CCM hawajui maana na kazi za vyama vya upinzani...Kamati Kuu inapenda umma uelewe kuwa maandamano ya CHADEMA Kanda ya Ziwa yalifanyika kwa taratibu zote za nchi na yalikuwa ya amani tele. Kamati Kuu inapongeza Jeshi la Polisi pale ambapo halikuingilia maandamano hayo pasipo lazima. Malengo ya maandamano yaliainishwa waziwazi kabla, wakati na baada.

"Operesheni zote za kisiasa za CHADEMA hugharamiwa kwa njia ya michango ya viongozi na wanachama pamoja na ruzuku ambayo chama hupokea kutoka Serikali Kuu. CHADEMA haijawahi na wala haina mpango wa kupokea fedha kutoka mataifa ya nje kwa ajili ya maandamano...mbinu za kisiasa kama hizi ni chafu na haziwezi kuiponya CCM magonjwa inayougua.

Bw. Mbowe alisema kuwa CCM imechokwa na wananchi na kuondoka kwake madarakani ni suala linalosubiri muda uamue, akisema kuwa Kamati Kuu hiyo imetambua kuwa Rais Kikwete ameanza kutekeleza walau kwa 'maneno' madai ya msingi yaliyotolewa na chama hicho, ikiwemo kuchukua hatua za kushusha bei ya sukari na gharama za umeme.

"Rais Kikwete na serikali yake wasiwe wazito wala wasione aibu kutekeleza yale yote ambayo CHADEMA inawashauri yenye manufaa kwa nchi lakini wayatekeleze kwa ukamilifu na ufanisi badala ya kufanya kiini macho. Watanzania wana haki ya kudai maisha bora kwa kuwa wameahidiwa muda mrefu na serikali.

"Ni wajibu wa serikali kufanya hivyo kwa kuwa inawatoza kodi wananchi. Kodi ni lazima ziendane na huduma inayolingana, na rasilimali za taifa lazima kwanza ziwanufaishe wananchi wenyewe na si vinginevyo," alisema Bw. Mbowe.

Alisema pia kuwa kamati kuu ya chama hicho imepokea kwa tahadhari na maskitiko taarifa za kuwepo njama za mauaji dhidi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, pamoja na wanasiasa wengine nchini, zilizotolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Mbali ya kuitaka serikali kuharakisha kufanya uchunguzi wa taarifa hizo zilizotolewa na kiongozi mwandamizi serikalini, kisha kutoa tamko juu ya hilo, CHADEMA wamelitaka Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha usalama wa Dkt. Slaa pamoja na viongozi wengine waliotajwa, kama ambavyo linapaswa kulinda wananchi wote.

"Kamati Kuu imepokea taarifa juu ya uamuzi wa serikali wa kuandaa muswada mpya wa Sheria ya Manunuzi...imezingatia kuwa lengo kuu la muswada huo ni kuiwezesha serikali na taasisi zake kununua bidhaa zilizotumika...hiki kitakuwa kisima cha wizi, hatutaunga mkono mabadiliko ya sheria yanayotaka kukidhi mahitaji ya watu, ikiwemo kununua mitambo chakavu.

"Tunatambua sana kuwa kuna mikataba mingi ya nishati hapa nchini tunataka yote itathminiwe...sasa hivi serikali ina mpango wa kukodi mtambo wa megawati 260 kwa takribani dola milioni 260...huu ni utapeli mkubwa...kwa nini wasinunue mitambo yetu wenyewe...wala hatutaki waingie katika biashara yoyote kinyemela na kampuni ya Dowans.

"Kwa nini mitambo hiyo isitaifishwe kwa maslahi ya umma kwa sababu iliingizwa kwa rushwa, hatuwezi kukubali biashara ya kuingia mkataba na Dowans, itumike sheria kutaifisha mitambo hiyo."

Aliongeza kuwa kwa sasa ni hatari Tanzania kutaka kujikita katika uzalishaji wa uranium, wakati haina hata sera za uvunaji wa madini hayo, akisema 'kama nchi imeshindwa hata kuhimili mitambo ya umeme na milipuko ya mabomu, itakuwaje uranium. Tuwaulize wenzetu huko Japan au Marekani sasa hivi hawalali, si kitu cha kukimbilia.

Kwa upande wake Dkt. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete ametoa tamko kinyume na katiba ya nchi kwa kuitaka hazina ipunguze kodi katika baadhi ya maeneo, kwani hiyo ni kazi ya bunge na serikali ilipaswa kupeleka mswada bungeni ili hilo lifanyike.

27 comments:

  1. Chadema msijifanye kuwa nyinyi ni watawala wa Tanzania. Hamjapewa dhamana hiyo. Mnaongea kwa kiburi kama vile mmepewa ridhaa na wananchi. Halafu mmuogope Mungu tuliwasikia mkimpa Kikwete siku 9 atimize matakwa yenu la sivyo mlisema mtachochea ya Tuninisia, Libya, na Egypt, kutumia nguvu ya umma. kama huko si kutaka kuiondoa serikali madarakani ni nini? Mmeona public opinion haiko upande wenu sasa mnajifanya kubadili malengo. Vinyonga wakubwa nyie. Siku 9 mlizompa Kikwete zimeshapita, je, ametimiza yote mliyotaka? Na kama bado sasa mnafanyaje? Nyie ni wanafiki wakubwa na cha mtemakuni mtakipata 2015. People now know your true colors.

    ReplyDelete
  2. ha ha ha ha ha ukwel nmeamini kuwa Tanzania kuna mazuzu wengi yaan huyo zuzu aliyechangia,kwanza inaonekana hujui katiba ya nchi ndio maana unasema hivyo,kama watu wamejua true colors of CHADEMA mbona kwenye maandamano ni wengi,halaf inaonekana hufuatili mambo,JK altoa tamko kabla hata siku tisa hajaisha alionekana aktia huruma sana,halafu ww inaonekana hujahururia mikutanao ya CHADEMA,wanachokifanya n kutuelimisha,hivi ww huon maisha yalivyo,mafuta yamepanda TZ 33% toka mwaka jana,bei za vyakula juu,ACHA UJINGA,ssem ni chama ambacho kinakumbatia watu wanaovunja hak.

    ReplyDelete
  3. Kusingizia Huyo Slaa wenu anataka kuuawa,kwa nini auawe,ili mpate umaarufu zaidi.Ana nini zaidiya kuwa potential dikteta.Kila kukicha ufisadi is his chorus.Nini kingine alichonacho zaidi ya kupandikiza chukika kwa wananchi waichukie serikali yao halali.Angekuwa na maana kama atashauriana na serikali kuleta maendeleo badala ya kuleta fujo na kusababisha watu maskini kupoteza maisha.

    ReplyDelete
  4. pole sana kwa maoni yanayoshafanan na mtu aneye ishi machakani, wewe hakika ni m..nga

    ReplyDelete
  5. mchangiaji wa kwanza na wa tatu, nadhani vidole vyao viliwasha na wakaamua kuandika upupu humu ndani. Mchangiaji wa kwanza ameshajibiwa. Nitamjibu wa tatu.

    Slaa kuuwawa siyo singizio la Chadema, issue hii ilitoka ccm tena kwa kigogo wa serikali ambaye ni naibu waziri. Sasa ulitaka Chadema wakae kimya wakati kiongozi wao ametajwa kuuwawa. Na suala na mauaji Tz halijaanza leo, tuna mifano mingi sana ya watu waliouwawa. Hatwa wewe ukitishiwa kuuwawa katiba inakuruhusu kutoa taarifa, hata kuomba ulizi wa polisi ikiwezekana.

    Ufisadi hauwezi kuachwa mpaka hapo ufisadi utakapotokomea, wewe ulitaka aache wakati bado unaendelea? Kwa taarifa yako bila kelele za Cdm za kupinga ufisadi Dowans wangekuwa tayari wamelipwa.
    Anachokiongea ni kushindwa kwa serikali kuwapatia maisha bora watanzania. Kila kitu bei juu, jee ni sawa. hata sukari inayozaliwa hapa hapa bei juu. Sisi kwetu tunatumia ya Malawi kwani ni bei nzuri kidogo.
    Hawezi kushauriana naserikali kwani yeye siyo consultant wa serikali. Maconsultant watafanya kazi gani?
    Nadhani hujui kazi ya siasa, siasa mahali pake ni majukwaani ndugu. opposition party kazi yake ni kuikosoa serikali pale inapofanya makosa. Ulitaka ukosoaji huo uwe siri????

    watu gani waliopoteza maisha? Umeona maandamano ya kanda ya ziwa? Hata mende hakufa. Wanaouwa watu ni serikali na dola yake, na siyo vyama.

    Mwisho naomba utafute elimu kwa nguvu zako zote kwani itakusaidia kuchanganua mambo kwa kina zaidi, hasa kwa kufanya utafiti, na siyo mtiririko wa maneno yasiyokuwa na data

    ReplyDelete
  6. chadema na watanzania wengne wote wenye upeo tunatakiwa tuwaelimishe na kuwaamsha mambumbumbu na mazuzu wa ccm kama akina kikwete, malisa, chiligati, sophia simba,ngeleja na wengineo mkkikaa kimmya taifa litaangamia kwa kukosa maarifa.tukikaa kimya hata mawe yatatucheka. mungu ibark chadema na wanachama wake wote.

    ReplyDelete
  7. kama si juhud za chadfema taifa lingekuwa wap? angalia kla kitu kinafanywa kwa shinikzo za chama hk tukufu cha upnzan. wananena yenye mmanufaa kwa wananchi na mpaka sasa wananchi wanajua kashfa nnyng na za aibu kwa sababu ya juhud za cchadema.maslah ya nchi hii yapo mikonon mwa watu vwachache waadilfu nao n mashujaa wa chadema. haya shime watanzaniva tukiunge mkono kwa hali na mali ikl tuifaid nchi yet

    ReplyDelete
  8. wakat wa maut ya ccm umewadia na tusishangae tunapoona ikitapatapa. imeshhindwa kujal masslah ya umma na ss umma upo mbion kukikondoa. ole wako kikwete, makamba, lowasa, malisa, rostam,chiligati,, ngeleja, pinda na wengne.kwan sanda na majeneza yenu n tayar na tutawazka kisiasa sku s nyng

    ReplyDelete
  9. Hawa wachangiaji wengine Bwana! sijui wanatokea wapi.hivi kazi ya upinzani ni nini?Upinzani ni taasisi rasmi kabisa na wana forum halali ya kuzungumzia mambo ya nchi na kuinyooshea kidole serikali iliyopo madarakani.Hata siku moja Upinzani hauwezi kuwa rafiki wa serikali iliyopo.Tatizo ni usingizi watu walionao kwa ajili ya kuzoea chama kimoja.Akiongea mtu anaambiwa ni treasonable!NYIE VIPI? na hawa akina Sofia wanyamaze watu wapige siasa na sio kuleta midomo isiyokuwa na tija. Mtanzania wa Leo sio kama yule wa miaka ambayo akina Sophy walikuwa wakibebwa ili waingizwe kwenye siasa kwa mbeleko za wazazi wao.Sasa ni ku- struggle!

    ReplyDelete
  10. wanaitetea serkal ya kikwete wajiulze yafuatayo:kwa nn nchhi hii inaendelea kuddmia kwenye umaskn pamoja na raslimal nyng zilizopo?2.kwa nn pamoja na hal ngum ya maisha tulionayo viongoz na vgogo waccm wanaendelea kuponda mal kwa magar na majumba ya kukufuru? 3.kwaa nn matatzo ya umeme na milipuko ya mabom kama ya gongo na mbagala yanajirudiarudia kana kwamba taifa halina mipango na dra? 4. kwa nn sehemu nyng zenye rasilimal za madn na nyngne wat wake wanaendelea kuwa maskin kupinduka eg.shinyanga? 4. kwa nn inajb hoja za chadema kwa vtsho badala ya mantk na utekelezaji? jiulze kabla ya kushabkia

    ReplyDelete
  11. Wa Tz tuwe tayari kuwasikiliza manabii walioletwa na Mungu kupitia Chadema ili wahubiri ukweli kuhusu Nchi hii.Hao wanaosema Chadema wanachochea fujo na kusema wanataka kuondoa serikali iliyopo hawana tofauti na wale waliosema Bw Yesu alizaliwa ili awe Mfalme na achukue kiti cha Herode!Bila kufahamu kuwa ufalme wake haukuwa wa hapa duniani.Rais na serikali yake hawatakiwi kukiogopa Chadema. wao wachape kazi.ili wananchi wanufaike na ikiwa hivyo hata chadema hatasema.Tujiulize, mbona ulaya,India, SA, mkate ukipanda bei watu huandamana? in maana hao ni wajinga?wanaishi kwa mkate TUU?Serikali wajibikeni na wale wababaishaji waondoeni watawaponza!

    ReplyDelete
  12. mm ninafkiri huyo mchangiaji namba moja na namba tatu wametumwa tu ili kuchafua hali ya hewa, hvi bila chadema kupitia slaa nani angejua madudu yote yanayofanywa na serikali??? jaman watanzania tunataka malaika ashuke ndo atuambie ukweli kuhusu nini kinaendelea nchini??? leo hii mtu aliyejitoa maishaa yake bila kujali vitisho na kuwaeleza watanzania ukweli kuhusu yale wananayoyafanya viongozi wetu amegeuka kuwa adui??? kweli hii nchi ndo maana haiendelei na kila siku tutabaki kuwa maskin tu kwani wananchi wake pia ni maskin wa kufikiri.

    ReplyDelete
  13. sasa imebakia jambo moja tu. nalo ni ama kubak ccm na kuendelea kuangamia kwanjaa na umaskin huku raslimal zet zkitafunwa na wachache wa ccm au kukiunga mkono chadema chama pekee cha upnzan kinachoonyesha nia ya kuikomboa tz na wanyonge wote. tuamue kusuka au kunyoa

    ReplyDelete
  14. ni dhahr kuwa kikwete hafai kuongoza na n bahat mbaya watanzania weng hatujaamka kama misri tungefanya kwel na wala tusingesubr chadema kama mapmb wa ccm wanavyokisingzia.chadema juuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuu

    ReplyDelete
  15. aliyotabr nyerere yametmia.alitabr ccm itakufa kwa wao wenyewe kukaangana kutokana na kukosa mwelekeo na dra. tazama wao kwa wao wanaanza kukaangana. leo wamemgeuka lowasa fsad mwenzao aliyekijenga chama kwa hela ya ufsad. tena waadlfu ndan ya chama hcho wanaoonekana kukikosoa chama wamekuwa mwba nass wanapanga kuwaondoa na kupanga kuwaua. ole wenu mwsho wenu umewadia. tubun mfe kwa aman. chadema idumu milele. mbowe na slaa waish milele. wanachama wake wachanue milele

    ReplyDelete
  16. wachangiaji wa kwanza na watatu , hao wasiwaumize vichwa , kwani hao ni wamoja wa katika timu ya mafisadi, pia hawana elimu ya kutosha kuhusu siasa, wanadhani vyama vya upinzani ni kampuni ya kutengeneza chocolate. Ifuatayo nawapa shule kidogo hao no.1 na no.3. Vyama vya vitukufu vya upinzani kama chadema ,ukiacha mamuruki na vibaraka wa sisiemu, kazi yake ni kuangalia na kuikosoa serikari ya chama kilichoko madarakani, kuhakikisha kinaongoza nchi kulingana na misingi ya katiba ya nchi, na si vinginevyo kama mnavyo dhani, tatizo viongozi wa sisiemu wanaongoza kwa mazoea na wala si kwa misingi ya kisiasa.(civil societies are watch dogs to the ruling government). Hayati baba wa taifa(mungu amlaze mahali pema peponi amina!) wakati wa utawala wake , alikuwa na utaratibu wa kupeleka makada wake kupata japo shule ya awali ya siasa hapo kivukoni, ndio maana miiko ya uongozi ilikuwepo, leo hii mafisadi yanaigia ktk siasa bila hata ya kufujua siasa ni nini. Chadema, kukosoa ndiyo mtaji wao na ndio maana ya multipartisim. Acheni mazoea ya chama kimoja. Ndungu Mh. Mbowe , tatizo kubwa la nchi hii ni elimu, hebu endeleeni kuwaelimisha watanzania watoke huko waliko, na mungu atawatangulia.

    ReplyDelete
  17. Wewe uliechangia wa kwanza nadhani una mtindio wa ubongo na taahira ya akili inabidi upelekwe mirembe ukatibiwe ukichaa. CCM ni mafisadi wakubwa katika nchi hii. Serikali nzima from the top ni mafisadi na wezi wakubwa sasa sielewi hata unachokitetea. President Kikwete na yeye ni fisadi pia kwa vile anatetea marafiki zake mafisadi kama lowasa.

    ReplyDelete
  18. Tunaomba kwa sasa hivi hakuna kupoteza muda tena ikiwezekana tuangalie wabunge watakapo kuwa huko bugeni tulifurumushe huko mitaani mpaka kieleweke. Tumeshaambiwa kila mtanzania atakula kwa jasho lake. Ruksa ukiingia mtaani utakachokipata ni saizi yako si jasho lako bwana.

    Chadema ndio imekuwa ikiwatuliza wananchi kwa kugusa kila hali tuliyonayo na kutupa faraja kwamba itashinikiza serikali itatue haya matatizo sasa majibu tunayopewa kila mtu atakula kwa jasho lake duuu!!!!!. Nabado alisahau kila mtu atakula kutokana ua urefu wa kamba yake. Na anajua hiyo ni laana mungu aliyompa Adamu na Eva walipovunja masharti yake.

    Nyinyi viongozi na serikali ya Kikwete sisi watanzania tumewakosea nini? Au ni hizo kodi tunazolipa na huo utajiri wetu mungu ametupa mnataka kutufunga mdomo. Hapa tutabanana mpaka kieleweke hakuna kupumua. Kwa kujibu hii kauli siku moja mtatusikia pale jangwani ili serikali iweze kuzinduka na kuwakemea watu wenye tabia za kuwatukana watanzania wawe wanachukuliwa hatua hatuwezi kuwa na serikali za kihuni.

    Vijana wataiga nini sasa kama serikali itakuwa na kauli za majivuno. AU NDIO MAJIBU YA MIPASHO NA MAPIGO KWA CHADEMA.

    ReplyDelete
  19. Nimefarijika sana kwa tamko la CHADEMA kwa maswala msingi ya taifa letu la Tanzania. Maana ya upinzani ni kuiamsha serekali itimize wajibu wake ipasavyo kwa wananchi walioiweka madarakani, na kazi za kisiasa za CHADEMA zikiwemo maandamano ni haki za kikatiba(Constitutional Rights), ninapata shaka kusadiki uelewa wa katiba kwa viongozi walioko serekalini kulikoni? Sisi watanzania tulio wengi atufahamu katiba ata na nyie mnaotuongoza?!!!!!! Ndugu zangu mnaotuongoza chonde chonde dunia kwa ujumla inataka mabadiliko na kamwe haki aiombwi ila inadaiwa, watanzania wa leo sio wa miaka ya 1980, ni Tanzania mpya, yenye watu wapya, fikra mpya na mitazamo mipya ya nchi yao. Kuna matatizo lukuki na umasikini uliokithiri nchini mwetu na wanaotuongoza utafikiri wanaongoza taasisi ya watu tisini. Ninawasii viongozi wote wa serekali kwamba MUNGU NDIO ATAWAONDO MADARAKANI na mwenzako akinyolewa tia zako maji, kwani uvumilivu wa watanzania utafika mwisho na umekaribia

    ReplyDelete
  20. Nashukuru sana CHADEMA. Kimsingi, chama hiki kinatoa matamko ambayo yametafakuriwa kwa kina "well thought" na kimsingi yanaonekana kuwa yanatolewa na watu ambao wako serious na nchi yao. naungana na wote na pia bwana Deo kuwa tunaomba watu waliobakia wenye akili timamu tuelimishe umma, tufike wakati nchi yetu iongozwe na misingi na kanuni na sio waganga wa kienyeji...Wanaua mashirika, wanalalamikia wakoloni, wanauza mabenki wanalalamikia ukoloni, wanauwa vyama vya ushirika wanalalamikia ukoloni...wanakusanya malimbikizo aka areaas, wanazifuata kuziiba tena, wanatafuta mawakili, wanashirikiana kuiba....wanajiuzia mashamba na viwanda, wanatuuzia sukari bei juu.... hii ni nchi ya kiwenda wazimu! tonge lilokuwa lipitie Tanesco limebumba tu kwa sasa ila ulikuwa ni mwendo uliozoeleka wa miaka mingi wa hawa watawala wetu

    Namtukuza sana Mungu kwani inaonekana anatupendelea sana waTZ, kwenye maradhi katupa Babu wa Loliondo, kwenye hatima ya nchi yetu katupa CHADEMA!

    ReplyDelete
  21. Watanzania msipofanya kazi kwa bidii mkitegemea kuna kiongozi yeyote wa siasa atakae wasaidia mtaishia pabaya. Mimi naungana na wazo la Mkulo kua kila mtu atakula kwa jasho lake. Try to be aggressive in bringing development for you own country. Vijana acheni kushinda vijiweni mkidiscuss siasa. Nanyi wafanyakazi kwenye sector za umma, acheni kwenda ofisini asubuhi na kukaa tu bila kufanya chochote mkisubiri saa tisa na nusu hali ukijua mwisho wa mwezi utadai mshahara ambao hujaingiza chochote kwa taifa. Kwa tabia ya watanzania na uvivu wetu tutaishia kumuona kila mtu ni mbaya. Tufanye kazi kwa bidii tuache malumbano.

    ReplyDelete
  22. Namshukuru mchangiaji aliyenitangulia. Kila mtu atakula kwa jasho lake na kila mta atavuna alichopanda. Kwangu mimi ninaona siku hizi watu wengi wanajifanya kuwa wanasiasa na kujaribu kutulitumia jukwaa la siasa kama sehemu ya nyongo ya kushindwa kwao. Watanzania wenzangu nafikiri hakuna mtu aliyeumbwa ambaye hana dosari awe kutoka CHADEMA, CCM, CUF na wengineo. Ombi langu ni kama yatakuwepo mabadiliko ya uongozi basi yawe kwa amani na utulivu kisha tuone wale wataochagulia watakavyotuongoza hata hivyo wanahitaji mikono yetu sote la wala si wale wakaao vijiweni bila kazi wakilalama ugumu wa maisha.

    ReplyDelete
  23. Kila lenye mwanzo lina mwisho! CCM ilizoea kuwadanganya wananchi wengi, hasa waishio vijijini (more than 80% of the population) kwa vile wengi walikuwa na elimu ndogo. Hivyo upeo wao wa kufikiri na kupembua mambo ulikuwa kidogo. Matokeo yake walizoea kujipatia ushindi ktk chaguzi mbali mbali kila mara pamoja na UOZO, UFISADI, WIZI, UDANGANYIFU NA UMBUMBUMBU wao. Lakini sasa mambo yameanza kubadilika kwani Wa-Tz wengi sasa wameelimika na wanaona kinachoendelea Tanzania na duniani kote. Maisha duni pamoja na shida nyingi wanazopata Watanzania hivi sasa vimesababiswa na uongozi mbumbumbu wa CCM.

    Rais JK baada ya kuchaguliwa tu alianza mizunguko duniani - safari za US, Europe, nk. kama vile ndiyo kazi tuliyompa. Huku nyuma akawaachia MAFISADI, ambao ndiyo waliompa fedha za kampeni, waibe watakavyo. Hatimaye wameifikisha nchi ktk hali mbaya tuliyonayo sasa hivi. Lakini Mungu katupa mkombozi - CHADEMA. Watanzania tuamke sasa na tuungane na CHADEMA tuikomboe nchi toka kwa hawa manyang'au na mafisadi wa CCM. Tutaendelea kuumia na kulala usingizi mpaka lini?

    ReplyDelete
  24. Nyie chadema kazi yenu ni kuwaita mbumbu wote wenye mawazo tofauti na nyinyi. Sijui mna matatizo gani? Toeni hoja siyo kuwatukana wengine. Kama viongozi wenu hamtumii busara kama viongozi wenu kazi kuropoka ovyo. Mchagiaji wa kwanza amesema kweli. Sasa hivi mbowe kukwepa kuwa hawana haja ya kuiondoa serikali madarakani inachekesha sana wakati tuliwasikia wakisema Kikwete asipotimiza masherti katika siku 9 wataongoza yale yaliyotokea Misri Tunisia na Libya na kumuondoa Kikwete madarakani. Jibuni hiyo hoja badala ya kuwaita wengine mbumbumbu. Haya maneno hamkuyasikia?

    ReplyDelete
  25. WEWE UNAEPIGA KENGELE NA CCM YAKO ENDELEA KUOMBOLEZA LABDA KITAFUFUKA. UMMA UKIAMUA KUINGIA BARABARANI HATA MBOWE HAWEZI KUZUIA ACHA KELELE ZAKO. KAMA AMEVUNJA SHERIA MKAMATENI BASI. ACHANI KUWASINGIZIA CHADEMA UONGO TULISHAWAJUA CCM NI CHAMA CHA WATU WA MANENO MENGI SASA, YAKUSEMA YAMEKWISHA MNATAFUTA MTU WA KUMALIZIA HASIRA ZENU.

    ReplyDelete
  26. Pengine ndiyo kusema 'samahani' katika lugha ya kisiasa zaidi. If thats the case, thats fine with me, na kazi iendelee...

    ReplyDelete
  27. Kama chadema mnataka moto endeleeni ni hizo sera zenu za nguvu ya umma. Ingieni mitaani kwa lengo la kuiondoa serikali mtaona ccm ni akina nani. Nyie mnaiga iga tu. Ya Libya Tunisia na Misri hayawezekani hapa. Watu wa nchi hizo walichoka na viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu, na katika nchi hizo hamunda uhuru wa kujieleza. Tanzania mnamtukana rais lakini bado mnaendelea na maisha. Hayo ndiyo watu wanayopinga. chadema mmekaa kuigaiga. Mnasahau ccm ina wafuasi wengi kuliko chama chochote kile. Mkitaka kujua chokoza muone. Tanzania itafurika kumlinda Kikwete ndipo mtajua maana ya nguvu ya umma nyie mnaoroka ovyo hapo juu. Kwanza wengi mliotoa maoni mpo nje ya nchi mmezamia huko muda mrefu hamko in touch na kinachoendelea huku. Wengi mmeshapoteza hata uraia wa Tanzania.

    ReplyDelete