Na Zahoro Mlanzi
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada, Nizar Khalfan analipasua kichwa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mpaka sasa haijulikani lini atajiunga na wenzake.
Nizar ni mmoja wa wachezaji watano wanaocheza soka la kulipwa ambao wameitwa kuipa nguvu Taifa Stars ambayo itakapoumana na Jamhuri ya Afrika ya Kati Machi 26, mwaka huu katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema ujio wa Nizar bado unaonekana una utata kwani timu anayochezea inadai haijauona ujumbe waliowatumia juu ya kumuomba mchezaji huyo.
"Inaonekana hili ni tatizo kwa Nizar, nimejaribu kuulizia hapa ofisini inaonekana wakati wote Nizar anapohitajika kujiunga na Taifa Stars, kunakuwa na vikwazo vingi.
"Tumewatumia ujumbe kwa njia ya e-mail (barua pepe) wakadai hawajaipata, kwa kuona hivyo sasa tumeamua kuwatumia tena e-mail nyingine, hivyo tunasubiri majibu yao na hili limeonekana ni tatizo sasa," alisema.
Alisema watajitajidi kadri watakavyoweza, ili mchezaji huyo ajiunge na wenzake kwa wakati kwani kuwepo kwake katika kikosi hicho, atachangia kwa kiasi kikubwa Taifa Stars kuibuka na ushindi.
Wakati huo huo, Wambura aliongeza kwamba wapinzani wa Taifa Stars, timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, imeendelea kutua nchini kwa mafungu na tayari nusu ya wachezaji wameshaingia nchini.
"Nakwenda Uwanja wa Ndege muda huu (saa sita mchana jana) kuna mchezaji mmoja wa Afrika ya Kati anakuja, na wengine wataingia kwa muda tofauti tofauti, wapo wa saa tatu usiku, saa nne na saa sita usiku," alisema Wambura.
No comments:
Post a Comment