Na Masau Bwire, Kibaha
UTATA umeibuka katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani baada ya familia moja kudai kuwa imepotelewa na watoto wawili mapacha katika mazingira
ya kutatanisha hospitalini hapo.
Hatua hiyo imekuja baada ya mmoja wa wanafamilia hiyo kujifungua kwa operesheni hospitalini hapo kuelezwa kuwa mama huyo alijifungua mtoto mmoja wa kiume aliyekufa angali tumboni.
Mume wa mwanamke huyo, Bw. Ernest Yusuph (42) alidai mke wake Bi. Agnes Aberi (32) alilazwa katika hospitali hiyo Machi 13, mwaka huu, asubuhi kwa tatizo la uzazi na kufanyiwa upasuaji Machi 15, mwaka huu mchana ili kutoa mapacha ambao mama yao alishindwa kuwazaa kwa njia ya kawaida kwa kuwa walikaa vibaya tumboni.
Bw. Yusuph alisema walitambua watoto mapacha tumboni mwa mke wake baada ya Daktari mmoja wa mzungu ambaye hawakujua jina lake, kumfanyia vipimo kabla ya upasuaji na kuwaeleza kuwa mimba yake ilikuwa ya mapacha ambao wamekaa vibaya, hivyo atalazimika kufanyiwa upasuaji ili kuwatoa kwa kuwa hana uwezo wa kujifungua kwa njia ya kawaida.
Alisema daktari huyo alimfanyia upasuaji mkewe na kuwatoa mapacha hao wakiwa wazima na mama yao akiwa na fahamu mara baada ya upasuaji, aliwashuhudia watoto wake wakiwa wazima tena wenye afya njema japo alishindwa kutambua jinsi zao.
Bw. Yusuph aliendelea kusema kwamba, baada ya upasuaji huo mke wake alirudishwa wodini bila watoto wake na bila maelezo yoyote kutoka kwa daktari kuhusu afya zao na mahali walipo.
"Baada ya mke wangu kutoletewa watoto wake kwa siku nzima, siku iliyofuata yaani Machi 16 aliniomba nikawaone lakini, wauguzi waliniamabia baada ya upasuaji alitolewa mtoto mmoja aliyekufa, hali ambayo ilinishtua na kunishangaza sana, papo hapo nikaanza kuchukua hatua.
"Katika kufuatilia kujua zaidi kuhusu walipo watoto wangu wawili, nikipinga taarifa ya nesi kuhusu mke wangu kujifungua mtoto mmoja aliyekufa, uongozi wa hospitali hiyo Machi 18 mwaka huu uliitisha kikao cha dharura kilichonijumuisha lakini, nao wakaniambia yale yale. Sikuridhishwa na maelezo hayo na tayari nimefungua kesi polisi kudai watoto wangu wawili," alisema.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Andrew Lwari alithibitisha mama huyo kulazwa Tumbo na kwamba baada ya mama huyo kupimwa hali ya tumbo lake ilionesha mtoto hachezi wala mapigo yake hayasikiki, na uwezekano wa mama huyo kujifungua kwa njia ya kawaida haukuwepo, hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji.
Dkt. Lwari alisema Dkt. aliyemfanyia vipimo mama huyo ambaye pia ndiye aliyemfanyia upasuaji ni Dkt. Sotta ambaye katika upasuaji huo alitoa tumboni mwa mama huyo mtoto mmoja wa kiume ambaye alikuwa amekufa tangu tumboni mwa mama yake.
Kuhusu madai ya mume wa mama huyo Bw. Yusuph kwamba mke wake kabla ya kufanyiwa upasuaji alipimwa na daktari mzungu aliyewaambia kuwa mwanamke huyo alikuwa na watoto wawili katika tumbo lake n uzushi na za uongo.
Alisema hospitali hiyo ina daktari mmoja wa kigeni Dkt. Walfrido Barrera, raia wa Cuba, ambaye ni daktari bingwa wa mifupa hana uhusiano na magonjwa ya akina mama na kizazi.
Dkt. Lwari alisema, kwa hali ya kawaida daktari hawezi mama aliyekuwa amefanyiwa upasuaji wa kizazi muda huo huo kwamba mtoto wake aliyemtarajia amekufa, hali ambayo alisema ingemletea mshtuko na kumsababishia madhara makubwa.
Muuguzi Mkuu wodi ya wazazi aliyekuwa zamu kwa siku hiyo, Bi Beatrice Justine alieleza kushangazwa na kitendo cha wanafamilia hiyo kugoma kuchukua mwili wa marehemu mtoto wao wakidai hafanani na yeyote katika ukoo wao, huku wakikataa kuchukua vipimo vya DNA.
"Jana (juzi) jioni rundo la watu wakiongozwa na baba wa mtoto huyo walifika hospitalini hapa wakidai wamekuja kuchukuwa mwili wa kichanga hicho, walipopelekwa mochwari na kuoneshwa mwili wa kichanga hicho walidai sio wenyewe eti sura yake haifanani na yeyote katika ukoo," alisema Bi. Justine.
Alisema walipowataka wazazi wa mtoto huyo kupima DNA kubaini kama mtoto huyo ni wao au la, wazazi hao walikataa katakata bila kueleza sababu za kukataa kwao kupima kipimo hicho ambacho matokeo yake yangeondoa utata kuhusu mwili wa kichanga hicho.
Bi. Justine alisema mwili huo umehifadhiwa na utaendelea kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo hadi muafaka wa sakata hilo utakapopatikana.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Kike na Kizazi hospitalini hapo, Dkt. Sylvester Mkama alisema mfuko wa uzazi wa mwanamke huyo ulipasuka kutokana na uvimbe uliokuwa chini yake, hivyo kusababisha kiumbe kilichokuwemo kufa na kulazimu madaktari kumfanyia upasuaji ili kukitoa tumboni mwa mwanamke huyo kabla hakijamletea madhara ya kiafya.
Huu ni mtihani! Madaktari wanapaswa kuwapa maelezo sahihi wagonjwa wao wasifikiri kila mtu ni mbumbumbu kwa kumwangakia kwa macho. Bora wakatae kupima dna kwa kuwa majibu yatakuja kama madaktari wa hospitali hiyo wanavyotaka wao. Mnajua tena TZ
ReplyDelete