02 February 2011

Yanga, Mtibwa jino kwa jino

Na Elizabeth Mayemba

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inashuka uwanjani leo kucheza na Mtibwa Sugar katika mwendelezo wa mechi zao za ligi hiyo
mzunguko wa pili.

Mechi hiyo itapigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaa ambapo Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 31 wakifuatiwa na Simba yenye pointi 27.

Yanga wanaingia uwanjani leo, huku wakiwa na kumbukumbu nzuri katika michezo iliyopita ya ligi hiyo baada ya kushinda mechi mbili mfululizo ambapo waliwasambaratisha vibonde AFC ya Arusha mabao 6-1 na baadaye wakaifunga Polisi Dodoma mabao 2-0.

Akizungumzia mchezo wa leo, Kaimu Kocha wa Yanga, Felix Minziro alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu mzunguko huu ni wa lala salama hivyo kila timu inajidhatiti kwa ushindi.

Alisema siku hadi siku anapokaa na timu hiyo mpya kwake anazidi kupata nayo uzoefu na kugundua kasoro ndogo ndogo, ambazo ameanza kuzifanyia kazi.

Naye Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kuondoka na pointi tatu.

"Safari hii Yanga wasitarajie mteremko kupitia kwetu na sisi pia tunatafuta pointi tatu, hivyo mchezo wa leo utajaa upinzani mkali sana," alisema Maxime.

Alisema timu yake ipo vizuri na wachezaji wake wana ari kubwa ya ushindi, kikubwa ni wao wenyewe kucheza kwa kujituma ili washinde.

No comments:

Post a Comment