02 February 2011

Wanaharakati wafuatilia fedha za elimu

Na Edmund Mihale

TAASISI za HakiElimu, Twaweza na Jukwaa la Sera jana walizindua mpango wa kufuatilia ni kwa kiwango gani serikali imetimiza ahadi yake ya kupeleka
fedha za kuboresha kiwango cha elimu katika shule za sekondari.

Mpango huo utahusisha shule tano katika kila wilaya kwa mikoa 20 kwa kuwahoji walimu, wazazi, wanafunzi na marafiki wa elimu ana kwa ana au kwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba 0715 723454 au kwa barua pepe: rafiki@hakielimu.org ambapo taarifa hizo zitatakiwa kuonesha jina la shule, wilaya, idadi ya wanafunzi na kiasi cha fedha za uboreshaji elimu zilizotolewa.

Ofisa Mchambuzi wa Sera na Uenezi wa Haki Elimu, Bw. Boneventura Godfrey aliwaambia waandishi wa habari kuwa mpango huo unatokana na serikali kushindwa kutoa fedha zote za uboreshaji wa elimu na kwa wakati.

"Wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari Januari 19, mwaka huu alisisitiza kuwa kipaumbele cha mpango huo ni kuboresha kiwango cha elimu.

"Rais Kikwete alisema kuwa serikali itatoa fedha kwa kila shule ya sekondari na fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya kufundishia na vya kujifunzia ili wanafunzi wapate vitabu na vifaa vingine muhimu," alisema.

Alisema serikali itatoa fedha za ruzuku sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya sekondari kwa mwaka ili kuboresha elimu ambazo zinatakiwa kutolewa kwa vipindi maalumu.

"Inatarajiwa kuwa ndani ya Mpango wa Serikali kwa kutoa fedha za uboreshaji elimu, fedha za Januari zitakuwa mwanzo wa muhula wa masomo zitakuwa asilimia 40 ya ruzuku ya mwaka mzima.

"Fedha zingine zinatarajiwa kupelekwa mwishoni mwa Aprili, Julai na Oktoba ya kila mwaka kwa hiyo ifikapo Januari 31, mwaka huu yaani jana (juzi) serikali ilitakiwa kuwa imepeleka sh 10,000 (asilimia 40 ya sh. 25,000)," alisema.   

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya ufuatiliaji matumizi ya Fedha za Umma kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taarifa zingine za utendaji wa wizara zinaonesha kuwa serikali imekuwa ikishindwa kutoa fedha zote za uboreshaji wa elimu kwa wakati.

Akitoa mfano, Bw. Godfrey alisema kuwa serikali ilikuwa ikitoa sh 7,634 kwa mwaka badala ya sh 25,000, hali ambayo inachangia kuzorotesha elimu nchini.

Alisema utaratibu huo unalenga kuwawezesha walimu, wazazi na wanachi wenye kupenda maendeleo ya elimu iwapo sh 25,000 zilizoahidiwa na serikali zinafika shuleni.

No comments:

Post a Comment