Na Addolph Bruno
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeifanyia marekebisho ratiba ya Ligi Kuu kwa kubadilisha michezo minne ya raundi ya pili
kwa sababu mbalimbali.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema sababu za mabadiliko hayo ni kutokana na mwingiliano katika baadhi ya michezo ya ligi hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu Ethiopia, kuchelewa kutaja tarehe ya mechi ya maruadiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na Debebit FC.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Ethiopia kati ya Februari 11, 12 na 13 mwaka huu baada ya mchezo wa awali kuchezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Uhuru, Dares Salaam ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 4-4.
Wambura alisema kutokana na chama hicho kuchelewa kutaja tarehe ya mchezo wa marudiano, mchezo wa Ligi Kuu namba 96 wa Yanga dhidi ya Kagera Sugar uliopangwa kuchezwa Februari 16 katika Uwanja Kaitaba mjini Bukoba umesogezwa mbele kwa siku moja, ili kuwapa nafasi Yanga kucheza na Dedebit.
Alisema michezo mingine iliyofanyiwa marekebisho ni mechi namba 85 kati ya Azam FC dhidi na Toto African uliopangwa kuchezwa leo katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utachezwa Februari 4 kwenye uwanja huo.
Wambura alisema mechi namba 89 kati ya Simba na Polisi Tanzania, ambao awali ulipangwa kuchezwa Februari 5 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, sasa utafanyika Februari 6 katika uwanja huo.
"Mabadiliko ya mchezo huu yametokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuutumia uwanja wake huo kwa ajili ya sherehe za kuzaliwa kwa chama hicho ambapo kitaifa zinafanyika mkoani Dodoma," alisema Wambura.
Alisema michezo mingine iliyofanyiwa marekebisho ni kati ya JKT Ruvu dhidi ya African Lyon, uliopangwa kuchezwa Februari 5 kwenye Uwanja wa Uhuru sasa utachezwa Februari 7 katika uwanja huo.
Wakati huohuo, Wambura alisema kutakuwa na semina elekezi kuhusu mashindano ya Copa Coca-Cola mwaka huu ambayo itafanyika Februari 5 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam ambayo itashirikisha makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
Alisema michuano hiyo mwaka huu itaanzia katika ngazi ya Wilaya ambapo imepangwa kuanza Machi Mosi hadi Aprili 10, mwaka huu na katika ngazi ya Mkoa itachezwa kati ya Aprili 23 hadi Mei 7.
Ofisa huyo alisema ngazi ya kanda ya michuano hiyo itachezwa katika mikoa ya Dares Salaam, Mwanza na Arusha kuanzia Juni 6 wakati katika ngazi ya Taifa hatua ya 16 bora itachezwa kwenye kitua kimoja cha Dar es Salaam kuanzia Juni 25 hadi Julai 2, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment