Na Mwali Ibrahim
SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limetoa wito kwa kampuni mbalimbali kudhamini mashindano ya wazi ya ngumi hizo, yaliyopangwa kufanyika
Dar es Salaam Februari 26 hadi Machi 5, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa BFT, Eckland Mwaffisi alisema mashindano hayo yanatarajia kushirikisha zaidi ya mikoa 20 ya Tanzania.
Alisema lengo la mashindano hayo ni kutafuta timu ya taifa, ambayo itaiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo michezo ya Mataifa ya Afrika 'All African Game' iliyopangwa kufanyikia Maputo, Msumbiji Septemba 2011.
“Mbali ya mashindano hayo, timu hii ambayo itachaguliwa na Kocha Mkuu Hurtado Pimenter, itaiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olympic, ambayo itafanyika London, Uingereza Julai 2012,” alisema Mwaffisi.
Aliongeza kuwa, gharama za mashindano hayo ni zaidi ya sh. milioni 25 ambazo hadi sasa hakuna kampuni, taasisi au shirika ambalo limethibitisha kutoa udhamini wao.
Mwaffisi alisema, umefika wakati wa kampuni mbalimbali kutoa udhamini katika mchezo huo wenye historia ya kuitangaza Tanzania kimataifa, ili uweze kufika mbali zaidi.
“Leo hii mchezo wa soka ndiyo unaopewa kipaumbele zaidi kuliko michezo mingine, ambayo kama itapewa udhamini na wachezaji kuandaliwa vizuri, wataiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na kuondoa dhana iliyojengeka kwa wachezaji wetu kuitwa watalii,” alisema.
No comments:
Post a Comment