Na Peter Mwenda
WAJUMBE wa kongamano la wadau wa maji katika Jimbo la Ubungo wameitaka serikali kuivunja Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam na
Pwani (DAWASCO) wakidai kuwa imeshindwa kuwaondolea kero ya maji kwa muda mrefu.
Pia wadau hao wamemuomba Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika kushirikiana na kamati iliyoundwa ya wajumbe kutoka Kata 14 za jimbo hilo kufuatilia watu waliojiunganishia maji kinyemela na kama hakutapatikana ufumbuzi wa suala hilo lifikishwe bungeni.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Bw. Mnyika aliyekuwa mwenyekiti wa kongamano hilo alipokea kero za wananchi wa jimbo hilo ambao wengi wao walishauri sheria ndogo ndogo zitungwe ili kuwaadhibu watu wanaokwenda kinyume na jitihada za upatikanaji wa maji.
Diwani wa Sinza, Bw. Renatus Pamba alisema DAWASCO ina mfumo wa maji ya ujanja ujanja ambayo hutumika kuwapelekea maji watu wachache wanaoyauza kwa bei ya juu kwa manufaa yao.
Bw. Paschal Manotata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kimara alisema maji mengi ya DAWASCO yanapotea njiani kutokana na watu kujiunganishia mabomba kinyemela, na magari ya mamlaka hiyo ambayo yamenunuliwa kwa ajili ya doria hayafanyi kazi hiyo badala yake yanaonekana yakiwa yameegeshwa kwenye baa.
Pia ilidaiwa kuwa fedha zilizotumika kutandaza mabomba ambayo mpaka sasa hayatoi maji zingetumika kuchimba visima kwani mpaka sasa maji hayatoki wala hakuna dalili lini yataanza kutoka.
"Tumekubaliana kuwa tunatoa mwezi mmoja kwa DAWASCO kubadili mfumo wa maji, baada ya hapo tutafuatilia DAWASA na wizara ya Maji na Umwagiliaji kama ikishindikana kupatikana maji nitapeleka hoja binafsi bungeni mwezi Aprili mwaka huu," alisema Bw. Mnyika.
Katika kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na taasisi za kiraia, EWURA, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Madiwani na wenyeviti wa mitaa, Bw. Mnyika alisema maji yakipatikana ni sifa kwa viongozi wote si mtu mmoja binafsi.
Bw. Mutaekulwa Mntegeka kutoka EWURA alisema bei ya ndoo moja ya maji ni sh. 20 na kuwataka wananchi wasilipe zaidi maji hayo katika vituo vilivyowekwa na DAWASCO.
Mwakilishi wa Maji katika Manispaa ya Kinondoni, Bw. Ramadhani Mabula alisema wananchi wanakuwa wagumu kutoa taarifa za wizi ya maji na kupasuka kwa mabomba ili hatua za haraka zichukuliwe.
Itakuwa vizuri magari sheria itungwe ili kila gari linalouza maji liandike bei Tsh 20/= kwa ndoo kama daladala zinavyoandikwa ubavuni.
ReplyDeleteHii bei ya Tsh 600/= wanaijua EWURA?
Asante Mnyika kwa kusikiliza maoni ya watu wako.
Naomba uwe na blog au wavuti wa mbunge kwa ajili ya kuweka taarifa za maendeleo ya jimbo la ubungo ili hata wasioweza kufika kwenye mikutano yako tutoe maoni na kujihabarisha.