01 February 2011

Kijana auawa na wanakijiji Bariadi

Na Bahati Mwiko, Bariadi

KIJANA mmoja Allan Japheti (23) mkazi wa Kijiji cha Mwamapalala wilayani Bariadi Mkoa wa Shinyanga ameuawa na wananchi wa kijiji hicho baada ya
kumjeruhi mwalimu wakati akimdai sh 1,000.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio, na kuthibitishwa na Mtendaji wa Kata ya
Mwamapalala, Bw. George Epaphra, zilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi  wiki iliyopita Majira ya saa 4:30 usiku.

Kaka wa marehemu, Bw. Yusuph Japheti alisema siku  ya tukio majira ya saa 11:30 jioni mdogo wake Allan alikwenda nyumbani kwa Mwalimu Thomasi Matulanya kudai deni lake la sh 1,000 ambazo aliambiwa azifuate siku hiyo.

Awali, alikuwa anamdai mwalimu huyo sh 15,000, akapewa sh 14,000 na kuambiwa afuate sh 1,000 baadaye siku hiyo.

Alisema baada ya muda marehemu alirudi nyumbani  kwa mdeni wake kuchukua sh. 1,000 iliyobakia na alipofika alimkuta mwalimu huyo ambaye
walihitilafiana, akapigwa hadi akazirai, na alipozinduka alishauriwa arudi nyumbani.

Alipofika nyumbani alipumzika na baadaye saa 3:00 usiku aliamka  na kurudi nyumbani kwa mwalimu huyo akiwa na silaha ambayo haifahamika ambayo
ilidhaniwa kuwa ni chuma kizito.

Kaka huyo wa marehemu aliendelea kueleza kuwa baada ya kufika nyumbani kwa mwalimu huyo alimpiga na silaha hiyo kichwani na kumsababishia jeraha
lililomfanya kuvuja damu na kupelekwa katika zahanati ya kijiji cha Mwamapalala kupata matibabu.

Bw. Matulanya akiwa huko akipata matibabu, wake zake waliuarifu uongozi wa kijadi (wasumba watale)  ambao walifika nyumbani kwa mwalimu huyo kujua nini kilichotokea, walipofika na kupata maelezo walidai
hawawezi kuamua hatua yeyote bila kuujulisha uongozi wa kijiji.

“Tuliondoka mimi pamoja na kiongozi mmoja wa jadi, Bw. Ndilanha Malezu kwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Bw. Jeremia Timotheo kumueleza juu ya yaliyotokea, yeye alidai hawezi kuhusika na hilo kwa sababu liko chini ya viongozi hao wa
jadi.

"Viongozi hao wa kijadi walipiga yowe kuita watu ambao walifika kama 150, baada ya kuelezwa wakaamua kumfuata Bw. Allan nyumbani kwao, wakavunja uzio wa nyumbani kwao, baadaye mlango wa chumba chake na kumtoa nje," alisema kama huyo wa marehemu.

Alisema baadaye alianza kumshambulia kwa mawe na vitu venye ncha kali, mikuki, mapanga hadi akafa na baada ya kufa walimbeba hadi barabarani umbali wa hatua 20 kutoka nyumbani kwao wakaleta paa la  kibanda cha nyasi lililokuwa limeezeka wakamwekea na kumchoma moto, kisha wakanyofoa sehemu zake za siri.

Jeshi la Polisi wilayani humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa hakuna mtu yeyote ambaye anashikiliwa kuhusiana na tukio
hilo.

1 comment:

  1. Kila unapopatwa na jambo unalohisi ni zito ni vema kutulia na kutafakari na kutumia hisia za kutokukubali kushindwa hivi vifo vinahusisha walimu sidhani kuwa hali ngumu ya maisha ya walimu ndiyo inapelekea haya ila ni tabia ya uvivu wa kufikiri. Ebu watu wabadilike na waanze kuyaangalia maisha kwa jicho refu na pana si kuwaza kupata kipato tokana na mshahara tu sasa mwalimu anadaiwa sh1000 mwingine anaiba saruji mifuko 8. Pia na wananchi nao ni vema tukawa na watu wanaoweza kushauri kwa busara yanapotokea matatizo ili kufikia njia bora ya muafaka. By dauden mashaka frederick

    ReplyDelete