01 February 2011

Kigwangalla kuwasilisha hoja kupinga mgodi

Na Reuben Kagaruki

MBUNGE wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla anakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa pili wa Bunge la 10 unaotarajiwa kuanza
Februari 8, mwaka huu kupinga uwekezaji katika migodi ya madini usionufaisha Watanzania.

Dkt. Kigwangwalla alivieleza vyombo vya habari jana kuwa atawasilisha hoja hiyo baada ya kukamilisha utafiti na uandishi wake, ambapo pamoja na mambo mengine ataomba mgodi dhahabu wa Golden Pride ufungwe mara moja kwa kuwa hauna manufaa.

Anataka wachimbaji wadogo na wenyeji waliokuwa wakiishi kwenye maeneo ya mgodi wa Golden Pride wanalipwa fidia mara moja baada ya kunyanyasika na kusumbuliwa na serikali pamoja na wamiliki wa mgodi huo kwa muda mrefu.

Mbunge huyo katika sharti lake la tatu kwa niaba ya ya wapiga kura wake na Watanzania kwa ujumla, anataka mgodi wa Golden Pride utekeleze wajibu wao katika kata 10 zinazozunguka mgodi huo kwa mujibu wa makubaliano.

Kwa mujibu wa tarifa hiyo, mbunge huyo anataka wawekezaji wote kwenye migodi nchini, bila kuangalia makubaliano ya nyuma waigawie Tanzania hisa na haki ya kumiliki migodi hiyo kwa asilimia isiyopungua 20, vinginevyo wafunge migodi hiyo na waondoke.

"Wawekezaji wote wapewe muda wa miezi sita wawe wamekamilisha mchakato huu," alisema na kuongeza; " Kwenye kila mgodi kuwe na utaratibu wa wazi wa kutangaza mapato, matumizi ya mgodi na TRA itengeneze utaratibu mzuri wa uhakiki ili kupata jumla ya uwekezaji na kiasi cha mtaji uliofanyika kwenye kila mgodi."

Mbunge huyo alitaka uwekezaji kwenye sekta ya uchimbaji usimame hadi hapo utakapokuwa tayari kuchangia, kuwekeza na kumiliki raslimali za nchi na walengwa kufaidika nazo.

"Tayari nina nyaraka nyingi na uthibitisho wa nitakayoyasema," ilisisitiza  Dkt. Kigwangwalla na kuongeza kuwa tayari amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio lake la kuwasilisha hoja hiyo tangu Januari 23, mwaka huu.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Tanzania imeshuhudia kukua na kuibuka kwa utafiti, utafutaji na uchimbaji madini lakini bado sekta hiyo inatoa mchango mdogo kwenye GDP na mapato ya serikali.

Mbunge huyo aliainisha changamoto zinazosababisha Tanzania isifaidike na miradi ya migodi ya madini kuwa ni wawekezaji kuongeza bei za malighafi zinazoingizwa nchini, kupunguza bei za mali wanazouza nje na kuongeza kwa maksudi gharama za uendeshaji na ada ya utaalamu.

Zingine kwa mujibu wa Dkt. Kigwangwalla ni kuongeza bei mitambo inayoingizwa nchini, kutorudisha nchini pesa za mauzo ya nje, kulipa wafanyakazi wa nje mishahara na marupurupu makubwa tofauti na wale wa ndani, misamaha ya kodi, misamaha ya kulipa mirahaba na kulipa kodi duni au kukwepa kulipa.

"Kwa ufupi maendeleo ya sekta ya madini yameshindwa kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania... Watanzania wengi wa kawaida wangetegemea kukua huku kwa sekta ya madini kungesaidia kuondoa umaskini na kukuza kipato, au hata kuleta maendeleo endelevu kwenye taifa letu," alisema.

Alisema Watanzania wengi walitegemea kuona mapinduzi katika sekta za elimu, afya, miundombinu na maji, mambo ambayo hawajayashuhudia hadi sasa, badala yake ndoto zao zimepotea.

Anataka serikali ianzishe mchakato wa kujiondoa kwenye mikataba ya kimataifa inayohusu upatanishi wa mikataba ya biashara ya kimataifa ili kujipa uhuru zaidi wa usimamizi na pia kuanza utaratibu wa kutengeneza mikataba bila kuwekewa vipengele vinavyolazimisha upatanishi ufanyike kwenye mahakama za kimataifa.

2 comments:

  1. Dkt. Kigwangwalla una mawazo mazuri sana, tatizo uko kwenye chama ambacho ndicho kilichokuwepo madalakani tangu Uhuru, hivyo matatizo yote hayo unayoyalalamikia ni sehemu ya CCM na serikali zake. Huwezi kurekebisha matatizo ya CCM ukiwa ndani ya CCM, lazima utoke nje ya box ili uweze kutatua matatizo korofi yanayoletwa na kutenda mambo kwa mazoea. Kusema hayo unayoyasema ukiwa ndani ya CCM unajitafutia balaa kwa mafisadi na washirika wao ndani ya CCM na serikali. Toka huko uliko nenda 'kule'vinginevyo labda kama uwe umetuma useme hivyo na watu wazito pia ndani ya CCM na Serikali vinginevyo utazimwa kama kibatali na kusahaulika.

    ReplyDelete
  2. Jamani si kila mtu CCM ni mbaya. Uongozi uliopo ndio mbaya. Yeye ni mwakilishi wa wananchi na ana haki kuuliza juu ya hayo yanayofanyika huko Nzega.

    Mwanche aseme ili tujue kama yanatoka moyoni mwake au ni ya mdomoni tu.

    ReplyDelete