17 January 2011

Viongozi wa dini wamnusuru mfanyabiashara

Na Gladness Mboma

SERIKALI wilayani Mbarali imewapongeza baadhi ya viongozi wa dini kwa kuzima jaribio la kutaka kuuawa kwa mwekezaji wa shamba la Mpunga lililopo Ubaruku, Bw. Abrahakh Phil Mohamed kwa madai ya kutumia jina la
Rais Jakaya Kikwete  kuwanyanyasa wananchi na kuwaita mbwa.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Cosmas Kayombo alisema kuwa viongozi hao wa dini wakiongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Evangelical Church (PEC), Bw. William Mwamalanga walizungumza na wazee na kuzima jaribio hilo.

Kanali Kayombo alisema kuwa wananchi hao walikuwa wakishinikiza kupatiwa eneo la shamba ambalo wanadai mwekezaji huyo alilichukua kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na kumkataa.

"Hata hivyo, Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa imekaa na viongozi wa vitongoji na vijiji vyenye mgogoro kuona ni nini kifanyike, ambapo walidai kutaka kurudishiwa eneo lao lililomegwa, ikiwa ni pamoja na kutaka mwekezaji huyo kuwapatia maji," alisema.

Alisema kuwa mwekezaji huyo amekubalina na ombi la wananchi, na amewaachia eneo la shamba ambalo wanalihitaji  na kuwapatia maji kwa ajili ya kumwagilia katika mashamba yao.

Kanali Kayombo alisema kuwa pamoja na wananchi hao kumkataa mwekezaji huyo, katika vurugu hizo walichoma gari la mafuta na kituo cha mafuta cha Igurusi, mali ya Bw. Munus Mohamed.

Naye Mchungaji Mwamalanga alisema kwamba katika vurugu hizo iliwachukua saa tisa kuwatuliza wananchi hao, akishirikiana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Advocate Nyombi.

Alisema kuwa wananchi hao walichukizwa na kauli ya mwekezaji huyo kuwaeleza kwamba yeye hawezi kuzungumza na mbwa bali anazungumza na mfugaji, ambaye ni Rais Kikwete.

"Kitendo cha mwekezaji huyu kuwatukana wananchi, ndicho kilichochochea hasira zao na kuamua kufanya vurugu, ambapo walichoma gari na kisima cha mafuta cha ndugu yake na mwekezaji huyo," alisema

Alisema kuwa kama siyo Kamanda wa Polisi Advocate Nyombi kuwa na busara na kuwatuliza wananchi, mwekezaji huyo angekuwa amechinjwa kutokana na vijana 17 ambao walikuwa wameandaliwa maalumu kwa ajili hiyo.

Mchungaji Mwamalanga alisema kuwa pamoja na kutulizwa, ikiwa ni pamoja na mwekezaji huyo kuahidi kuwarudishia mashamba pamoja na maji, wananchi bado wamemtaka kuondoka katika shamba hilo kwa kuwa amewatukana wao pamoja na rais.

"Huyu mwekezaji ametakiwa kuomba msamaha wananchi na pia ametakiwa kumuomba radhi rais kwa kitendo chake cha kuwaita mbwa, pamoja na kutubu," alisema.Naye Kamanda Nyombi alisema kuwa amesikia kwamba wananchi hao wametoa siku tatu kwa mwekezaji huyo kuondoka licha ya kuwatuliza ma kuwasihi wasifanye vurugu zozote juzi.

"Ndugu Mwandishi hivi ninavyozungumza na wewe niko njiani naelekea Mbarali baada ya kusikia kwamba wananchi wametoa siku tatu kwa mwekezaji huyo kuondoka, tumefanya juhudi kubwa sana kuhakikisha kwamba tunazima vurugu hizo ambazo zilikuwa ni za kumwaga damu," alisema.

6 comments:

  1. Viongozi wetu wanajichafua kwa ufisadi kwani wanapopewa pesa na wawekezaji uchwara kama hao wa kiarabu huwatolea siri kuwa nao ni wabia kwa maneno machafu kama hayo ya wananchi kuitwa mbwa na kwamba wanaongea na mwenye mbwa, nchi yetu inakwenda wapi, mzee wetu Nyerere angetoa masaa 48 ya huyo mwarabu kuondoka nchini.

    ReplyDelete
  2. Bora useme tu. wawekezaji kama hao WAISLAMU utaeleweka.

    Warabu wamewkeza hati nchi kubwa duniani kama vile Uingereza, Marekani n.k.

    Hivi kuchoma gari ya kuchukulia mafuta ya mfanyabiashara mwengine hata hahusiki na mwekezaji wa shamba maana yake nini? Ni kwa vile Muislamu. Ni Udini ...udini...udinii tuuuuu

    ReplyDelete
  3. hapo hamna udini kaka ila ni pale tunapoona mtu anakuja anachuma juu ya vichwa vyetu na tunamshangilia hapo ndipo penye utata. Ni lini tutajivunia mali yetu (ardhi na viliyopo chini) na tuifaidi sisi wenyewe

    ReplyDelete
  4. Eneo la Mbarali/Ubaruku ni makazi ya Waburushi (Waarabu toka Uajemi) kwa miaka mingi sana. Kama tatizo ni udini, wakazi wa huko wengi ni Waislamu kutokana na mwingiliano huo wa Waburushi kwa muda mrefu. Inaelekea tatizo hapa ni kwa wenyewe kuonekana kuwa ni second citizens.

    ReplyDelete
  5. Mchangiaji wa pili toka juu, hoja ya udini imetoka wapi tena? Yaani mtu kutaja mwaraabu basi ametaja uislamu? Kwani waarab wote ni waislamu? Tafadhali tuchangie hoja kadri ya ukweli wa jambo na sikukurupuka na kuingiza hoja zisizohusiana na mada yetu.

    ReplyDelete
  6. Kama kweli huyu mwekezaji kasema wananchi ni mbwa na Mheshimiwa Rais ni mfugaji basi anapaswa kushtakiwa kwa kutukana. Mwekezaji kapata wapi jeuri ya kuwaita binadamu wenzie mbwa? Na kwa ya dini mbwa si mnyama wa kuwa karibu nae hata kidogo...

    Lakini pia kuwaita wananchi 'wafugwaji' na Mheshimiwa Rais 'mfuga' mbwa ni jambo ambalo haliingii akilini. Yaani Rais sio kiongozi bali amekuwa anawafuga Watanzania? Wawekezaji ni vema wakaheshimu watu hata kama ni maskini na wana rangi/imani/elimu tofauti na walonayo wao.

    Tumuombe MUNGU aondoe hasira za wananchi wa Mbarali na ampe Rais wetu na viongozi wa mkoa wa Mbeya busara na hekima ili watatue mgogoro huu unaoletwa na mwekezaji huyu kwa amani.

    Kikongoti, KM

    ReplyDelete