17 January 2011

Uchaguzi Mkuu ZFA waota mbawa

Na Mussa Soraga, Zanzibar                                                 

UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), ambao ulikuwa ufanyike keshokutwa Nungwi mjini hapa umefutwa, baada ya Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Michezo kutaka usitishwe.Agizo hilo limetolewa na
Mrajisi wa vyama hivyo, Mustafa Omari Abdallah ambaye alimwandika barua jana Katibu Mkuu wa ZFA, Mzee Zam Ali na nakala kutumwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na michezo, Abdillahi Jihad.

Barua hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kisheria, ofisi yake imeitaka ZFA kusitisha uchaguzi huo wa marudi uliopangwa kufanyika Jumatano hadi hapo Mrajisi huyo atakapokaa meza moja na uongozi wa ZFA Taifa.

Mkutano wa pamoja kati ya Mrajisi huyo na uongozi wa ZFA utafanyika leo katika Ofisi za Baraza la Michezo la Zanzibar (BMZ).

"Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Michezo kwa mamlaka iliyopewa kisheria, chini ya kifungu cha 19 (b) cha sheria namba 5 ya mwaka 2010 ya Baraza la Michezo la Zanzibar, inatoa agizo kuwa uchaguzi wa ZFA usimamishwe mara moja," ilisomeka sehemu moja ya barua hiyo.

Hata hivyo wakati barua hiyo inawasilishwa katika ofisi za ZFA, chama hicho kilikwishafanya maamuzi ya kutofanyika kwa uchaguzi huo kutokana na ombi la Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Uchaguzi, Abdulghan Msoma.

Msoma, ambaye kamati yake imechukua nafasi ya kamati iliyovunjwa ya Ali Suleimnai Shihata, aliiomba ZFA kuuaghirisha uchaguzi huo hadi baadaye ili yeye na wajumbe wake wapate muda mzuri wa kujipanga.Alisema kazi ya kusimamia uchaguzi si nyepesi kwa sababu inahusisha masuala ya kisheria, hivyo aliomba muda zaidi kwa nia ya kuipitia katiba pamoja na kujiweka sawa kabla ya uchaguzi huo mpya haujafanyika.

Licha ya Msoma kutaka uchaguzi huo usogezwe mbele, alishauri uchaguzi mpya uwahusishe na wagombea wengine kwa vile ule awali uliofutwa na kamati ya Shihata ulikuwa batili.

3 comments:

  1. Kuna mkono wa mtu hapa! Huyo mzee Fereij bado ana nguvu ZFA, japo hatakiwi, na yeye mwenyewe apime tu! kung'ang'ania madaraka ni aibu na ishara ya ki-sultan, akubali tu muda wake umemaliza akae pembeni si tena kutoelana aibu juu ya cheti cha form IV!

    ReplyDelete
  2. Hatakiwi na nani? kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi alishinda.

    Hao walioshindwa kwenye uchaguzi ndio hawatakiwi. Karume ni darasa la sita na aliongoza nchi na kututoa kwenye usultani.

    ZFA haitaki kujenga mtambo wa nuklia kiasi ambacho elimu inayotakiwa iwe ya juu sana.

    ReplyDelete
  3. Ndugu yangu unayemfagilia Fereij hapo CUF nini wewe?

    ReplyDelete