17 January 2011

Jaji Mapigano afariki dunia

Na Gladness Mboma

JAJI Mstaafu wa Mahakama Kuu nchini, Bw. Dan Mapigano amefariki dunia katika Hospitali ya Aghakan Dar es Salaam.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari, Jaji Mapigano alifariki jana baada ya
kulazwa katika chumba cha wagonjwa maututi akiwa anapumulia mashine.

katika uhai wake, Jaji Mapigano alitumikia nafasi hiyo kwa nyadhifa mbalimbali, akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tangu mwaka 1974, baadaye Mahakama ya Rufaa nchini.

Mbali na nyadhifa hizo, akiwa Jaji wa Mahakama Kuu kwa takribani miaka 26, Jaji Mapigano alikuwa miongoni mwa majaji waandamizi na alikuwa akiheshimika kwa kutatua kesi mbalimbali za biashara na utatuzi wa migogoro.

Jaji Mapigano enzi za uhai wake pia imekuwa muhimu katika kukuza mahakama, kusimamia upatanishi na kutafuta mbadala katika kesi mbalimbali hususani za  madai.

Jaji Mapigano alichukua mafunzo maalumu katika upatanishi katika Mahakama Kuu ya Washington DC nchini Marekani na kuwa Mwenyekiti wa Jopo la wakufunzi wa upatanishi wa mahakama inayosimamiwaa na Tanzania.

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Bw. Francis Mutungi alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa taarifa rasmi kuhusu kifo hicho ataitoa leo asubuhi.

No comments:

Post a Comment