18 January 2011

Nahodha ahofia amani kutoweka nchini

Na Peter Twite
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, (pichani amesema kuna dalili za kutoweka maadili miongoni mwa jamii jambo linalotishia kuwepo machafuko yanayoweza kusababisha kutoweka amani nchini. Bw. Nahodha aliitoa
kauli hiyo, alipozungumza katika ibada maalumu ya kuwekwa Wakfu Askofu Mkuu Mteule wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God Tanzania (PAG) jana jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika ibada hiyoiliyofanyika katika Kanisa hilo,Kinondoni, Bw. Nahodha alisema anaona kila dalili za kutokuwepo maridhiano, upendo, upole na uaminifu miongoni mwa jamii ya Watanzania mambo ambayo yanaweza kuleta machafuko katika jamii yetu.

“Naziona kila dalili kwenye ubao, naziona dalili za kutoweka kwa maridhiano, upendo, upole miongoni mwa Watanzania,uaminifu katika jamii yetu,mashauriano miongoni mwa viongozi, mambo haya yasipokuwepo ni hatari kwa taifa letu linalosifika kwa amani na utulivu kwa miaka mingi,” alisema.

Aidha, Bw. Nahodha alisema kuwa zipo dalili zinaanza kujitokeza nchini watu wanaanza kutazamana kwa misingi ya dini zao, hakuna kuhurumiana jambo ambalo ni hatari kabisa kwa kujenga misingi ya umoja wa katika taifa letu.Bw. Nahodha alishauri ni vema viongozi wa serikali wakawa tayari kushauriana na viongozi wa dini badala ya watu kuanza kukosoana kwenye magazeti kwakuwa kwa kufanya hivyo watajenga mazingira mazuri kwa viongozi kuliongoza taifa letu kwa amani na utulivu.

Pia, Nahodha alisema kuwa kuwepo kwa viongozi wasio waadilifu katika jamii ni kielelezo cha matokeo ya viongozi wa dini kushindwa kutekeleza wajibu wa kusimamia na kufundisha maadili nchini jambo ambalo linalosababisha kupatikana kwa viongozi wasio waaminifu na wala rushwa. “Jamii imekuwa ikifanya tathimini ya maadili mabovu kwa wanasiasa pekee yao wanasahau kuwa wanasiasa ni zao la dini zetu, wanasiasa wakiwa wala rushwa ni wazi kuwa viongozi wa dini wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kusimamia na kuelekeza jamii na waumini wao katika maadili mema,” alisema Bw. Nahodha. Pia, Bw. Nahodha alisema kuwa msongamano mkubwa wa mahabusu aliouona hivi karibuni katika magereza, baada ya kufanya ziara ni kielelezo cha tosha kuwa maadili katika jamii yetu yamemong’onyoka jambo ambalo analiona ni hatari kwa taifa letu ambalo linasifika kwa amani.

Hata hivyo, Bw. Nahodha alisema kuwa wizara yake ina mpango mkakati wa kumaliza kabisa matatizo ya wizi wa silaha, wa kalamu na wa kutumia nguvu unatoweka kabisa hapa nchini na kufanya jamii kuishi kwa amani na utulivu.“Najua kuna watu watasema kuwa Bw. Nahodha anaotandoto lakini kila kitu kilianza kwa kuwa ndoto, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani nina ndoto hizo za kuhakikisha kuwa siku moja wizi wa kalamu na wa kutumia nguvu unatoweka kabisa nchini Tanzania,” alisema Nahodha.

Pia, Bw. Nahodha amewataka viongozi wa dini nchini kuhakikisha kuwa wanakuwa na mashauriano na serikali katika mambo yote yanahusu maslahi ya taifa letu, na serikali iko tayari kuwasikiliza badala ya kuwa na kawaida ya kukosoana katika magazeti. Vile vile, amewataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao katika kulijenga taifa kwani kazi ya viongozi wa dini pamoja na kuwaelekeza watu kumjua Mungu bali pia ni wajibu wa viongozi wa dini kuwaandaa watu kumudu maisha yao kwani ndipo wataweza kumtumikia vema Mungu.

Naye, Askofu Mkuu aliyesimikwa wa kanisa hilo Daniel Awatt akitoa shukrani kwa mgeni rasmi, alisema viongozi wa dini wataendelea kushirikiana na serikali, vile vile amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuahidi kuunda Tume ya kushughulikia suala la Katiba mpya, pamoja na kumtaka kuhakikisha kuwa mchakato wa katiba mpya unawashirikisha wadau wote wakiwemo viongozi wa dini. Awali, akizungumza katika ibada hiyo maalumu, Katibu Mkuu wa Kanisa la PAG, Askofu, Charles Kanika, alisema kuwa kanisa hilo mbali ya kujishughulisha na huduma za kiroho, pia limekuwa likifanya kazi katika huduma za jamii kwa kuungana na serikali katika wito wake wa kuelimisha jamii.

10 comments:

  1. Suala la dini ni kisingizio cha siasa zilizoshindwa. Mbona Zanzibar kabla ya serikali ya maridhiano watu walikuwa hawazikani, walitazamana kwa ubaya licha ya wote kuwa waislam? Viongozi wa CCM baada ya kuona wameshindwa kutekeleza walicho ahidi kwa wananchi, wametafuta kisingizio cha udini ili kuficha agenda ya kushindwa kwao. Mbona sisi huku uraiani tu wamoja? Huo udini wanaouhubiri viongozi wa CCM hatuuoni?

    ReplyDelete
  2. Ni kweli mbona kule Zanziba CUF na CCM wote walikuwa waislamu lakini mapambano yale mbona hayakuguza hisia za udini. Hii ni njama ya CCM kujaribu kufukia yale mahofu wanayoyatenda kila kukicha!!!

    ReplyDelete
  3. Naodha acha Hizo! serikali ya ccm ndio itavuruga amani tz c mtu mwengine. cha kufanya ni kupambana na ufisadi na mafisadi, kupanua wigo wa ukusanyaji kodi, kupunguza matumizi ya utawala serikalini, kusimamia maadili mema, kutoa huduma za afya na elimu, kusimamia rasilimali za nchi kwa faida ya umma, kuhakikisha nishati ya umeme na maji vinapatika kwa bei nafuu, mazingira na misitu kulindwa, haki za wafungwa kutolewa, kupambana na bidhaa feki,kujenga miundombinu(barabar na shule na zahanati) kwa kiwango takiwa, kuunda tume huru ya uchaguzi, takukuru huru na uhuru wa habari na maandamano ya amani na ajira kwa vijana, mikopo ya wanafunzi vyuo vikuu, kuwatengea wamachinga maeneo ya biashara na kuwawekea miundombinu. pia ya mwisho na muhimu mlipo serikalini mfanye kazi kwa kujali umma, kujali matakwa yao, kufanyakazi kwa wito, c ubabe, kumbuka umma au wananchi ndio mwaajiri wako mkuu, jifanye mtumwa kwao, mtaarifu vinginevyo kwa busara. mkitekeleza hayo nchi itakuwa na amani na ccm mtaichi milele kiuongozi bila hayo moto utawaka. pia usisahau katiba mpya itakayotunga na wananchi.

    ReplyDelete
  4. Nna imani kubwa aliyo yasema waziri nahodha ni sahihi kabisa 100% kutokana na vigezo vya maoni ya walionitanguliya kuchangia mada hii.wakati wa utawala wa baba wa taifa julius nyerere alieleza wazi ni haramu kuchanganya dini na siasa au kutia ukabila katika siasa kwani kutapelekea watu kubaguwana katika mielekeo ya kimaisha yao wakati wote ni wa moja.Nahodha hazungumzi kama yeye ni mzanzibari au ccm au muislamu anazungumza kama mtanzania mwenye nia ya kuendeleza mshikamano miongoni mwa watanzania.Zanzibar sio bara,zanzibar hakuna kabila na watu wake wote karibu ni wa dini moja na ndio maana leo kuna mapatano,watanganyika msiombe matatizo yaliotokea zanzibar yatokee bara itakuwa balaa na ni vizuri kuchukua hatua madhubuti kuepusha chuki miongoni mwa wanachi kwa misingi ya dini kwani watu wakitoka katika udini wataingia katika ukabila sasa jiulize wewe mwenyewe bara kuna makabila mangapi na kila kabila litataka kuwa ndio lenye nguvu kwa kweli hizi proganda zenu mnazozitapakaza kwenye vyombo vya habari kwa visingizio vya kupanua demokrasia ni sawa na kutoboa jahazi mnalosafiria likizama hazami nahodha peke yake.

    ReplyDelete
  5. Mimi ni yule yule Hafidh- mpenda mageuzi kutoka visiwa vya amani Zanzibar. Jamani jamani ndugu zangu! mbona mbinu ya CCM mnakua hamuijui ! mna mawazo mgando na umaskini wa kifikra?! ok CCM Maisha yote sera yao ni hii ya kupiga kelele watu wasichanganye dini na siasa! kwa sababu wanajua huu ni mwiba kwao.wao wanawagawa jamii ilimradi wawatawale tu= Devide and Rule.Hebu nambieni na kama kuna mmoja wenu anaeweza ku challenge alete hoja hapa tuijadili kua Dini na Siasa ni vitu 2 tofauti!!! mimi binafsi nasema Dini na Siasa ni kitu kimoja kwa sababu hizi zamsingi wa hoja yangu.

    Nini maana ya Dini kwani? Dini ni mfumo wa maisha ya mwanadamu aliotakiwa kufata na Mungu kupitia Vitabu takatifu na kuongozwa na Mitume ili mwanadamu huyu apate maisha mazuri ya duniani na akhera.

    Nini Maana ya Siasa kwani? Siasa ni mfumo wa maisha ya mwanadamu aliejipangia katika kujiletea maisha mazuri Duniani.

    Kwa hiyo ikiwa hii ndio tafsiri ya dini na siasa basi sioni sababu ya watawala kutenganisha !
    2) Ndani ya Dini ipo Siasa - siasa ni sawa na tawi(Branch) ndani ya Dini, Dini ina utawala kamali,(Government)ina Mamlaka ya sheria kwa mujibu wa vitabu takatifu( Justice) na ina mamlaka za kuhoji na kusimamaia utekelezaji yaani Shuura- kwa waislamu (Parliament) kwa hiyo mihimili yote hii mitatu inapatikana ndani ya dini.sasa jee wapi utaweza kutenganisha dini na siasa? naomba kama kuna mtu mwenye mchango au hoja aweke mezani hapo. lakini tusipotoshane kua Dini na siasa ni mbali mabali.

    ReplyDelete
  6. CCM Inapenda kutufanya Viongozi wa dini vikaragosi na vibaraka wao kuwasaidia kutawala hata kama ni kwa dhuluma. Sisi ni watumishi wa Mungu hatapaswi kubariki wizi, uchakachuaji, ufisadi na mauaji.

    CCM inaiba kura halafu wachungaji na maaskofu tunaitwa tukawaombee walioshinda baraka! Hii ni Aibu Kwa kanisa

    ReplyDelete
  7. Inawezekana dini na siasa vikawa ni vitu sawa inategemea ni aina gani wa mfumo wa serikali husika inafuata ikiwa serikali hiyo inaendeshwa kidini kama Irani,saudia arabia na nchi nyengine zinazoendeshwa kidini basi there is no doubt religion can be included with the politics.Lakini hata hizo nchi zinazoendeshwa kidini kama irani zimejikuta zikiingia katika machafuko makubwa ya kisiasa na watu kupoteza maisha yao na mali zao(TANZANIA HAIENDESHWI KIDINI) kwa maoni yangu binafsi kuna dalili kubwa ya kwamba kuna baadhi ya wazanzibari ambao wangependelea na kufurahia kuona kuwa tanzania bara inaingia katika migogoro ya kisiasa kama ilioikumba zanzibari au kuliko sielewi ni kwa manufaa gani na ya nani.

    ReplyDelete
  8. watanzania sasa tufanye kama tunisia tuiondoa ccm kwa maandamano kupinga udhalimu wao.. ufisadi, umeme,shida za walimu,ajira hakuna,madini yananufaisha waliomadrakani, watanzania tusidanganywe na kuwa hii ni nchi ya amani! amani wapi hali wengine wanafaidi nchi, matajiri wachache, wengi wetu ni hohe hahe, tunadanganywa na hii ni nchi ya amani!!!YALIFANYIKA TUNISIA HATA SISI TUNAWEZA!!!

    ReplyDelete
  9. NAHODHA SOMA HISTORIA YA NCHI ZILIZOENDELEA, WAMEPITIA KIPINDI AMBAPO AMANI ILITOWEKA MPAKA WALIPOZIPIGA KWANZA NDO WAKAHESHIMIANA NA KUTENDEANA HAKI, WEWE UNAKULA NA KULALA PAMOJA NA FAMILY YAKO. MAISHA YA WATZ WENGI KWA SASA NI DUNI SANA, WANALALA NJAA, HAWAWEZI KUMUDU GHARAMA ZA IBA NK, HICHO KISIWA CHA AMANI NA UTULIVU KINATOKA WAPI????? SHUGHULIKIA MAFISADI KWANZA NDO UTULIVI NA AMANI VINAWEZA DUMU KWAS SABABU MAFISADI WANAIBIA NCHI MPAKA NA WANANCHI

    ReplyDelete
  10. hivi hao mapadri na wachungaji chadema ikipigwa mabomu na kusambaratishwa maamdamano yao wanakuwa wa kwanza kukemea je yale maandamano ya CUF ya kuwasilisha mapendekezo ya katiba yaliposambaratiswhwa na polisi kwa mabomu kwanini hawakutoa tamko?. msemo wa chadema nguvu ya UMMA sio kweli ni nguvu ya KANISA wanayoitegemea. SLAA Hana akili kwani akili zake ni za kuambiwa na kanisa bila kuchanganya na zake mbayuwayu mkubwa.
    Wavue majoho wahubiri siasa.

    ReplyDelete