18 January 2011

Na Benjamin Masese

SIKU moja baada ya serikali kutoa ajira 9,226 za walimu waliohitimu mafunzo ya ualimu mwaka 2009/2010 katika vyuo mbalimbali jana baadhi ya walioachwa walivamia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutaka kujua hatma ya
ajira zao walizoahidiwa tangu wakiwa vyuoni. Wanafunzi hao zaidi ya 100 kutoka vyuo mbalimbali vikiwemo cha Mtwara, Marangu, Morogoro Kasulu, Tabora na vinginevyo walifikawizarani hapo na kutaka kupewa vigezo vilivyotumika kuajiri walimu na kuacha wengine wenye sifa zinazostahili.

Wanafunzi hao ambao walizua tafrani getini baada ya kuzuiwa na walinzi huku wakitaka kuonana na Waziri wa Elimu Dkt. Shukuru Kawambwa kitendo kilichosababisha ulinzi kuimarishwa kwa kutumia baadhi ya askari wa Ikulu ambao walitoa onyo kuwatahadharisha kuwa eneo hilo halitakiwi kelele, maandamano wala mkusanyiko wowote wa amani. Askari hao waliwataka wanafunzi hao kutafuta eneo lingine na kuchagua wenzao watatu kuwasilisha malalamiko yao wizarani kwa njia ya barua.Wakizungumza na Majira walihoji kuwa hawajui serikali imetumia sifa na vigezo gani kuwaajiri walimu kutokana na wengi wenye sifa kuachwa .

Walisema walipata mafunzo ya ualimu kwa miaka miwili ngazi ya diploma ambapo mwaka mmoja hukaa chuoni na mwingine hupelekwa kwenye mafunzo na baada ya kumaliza mafunzo hayo walirudishwa kufanya mtihani na waliambiwa chuoni kwamba kama mwanafunzi asipofaulu masomo kuanzia moja hadi matatu atapewa ajira serikalini lakini lazima kuyarudia masomo hayo. “Lakini baada ya jana (juzi) serikali kutangaza ajira tumekuta mabadiliko ambayo hatukuambiwa ambapo wameajiri waliofaulu masomo machache na wasiofaulu na kuacha waliofauli masomo mengi na majina yetu hayapo...sisi tunataka vigezo vilivyotumika leo hii pia tunaajiriwa au ‘ilisha kula’ kwetu?”Alihoji mmoja wao ambaye alikataa kutaja jina lake.Alisema kuwa tangu wahitimu masomo yao Mei mwaka jana wamekuwa wakipewa ahadi ya kuajiriwa na serikali lakini hadi leo ajira hiyo ndio inayoanza kuleta ubaguzi na utata.

Hata hivyo wakati hayo yakiendelea getini uongozi wizara ngazi za juu ulipata taarifa ya maandamano hayo na kulazimika kuwasikiliza. Muda mchache baada ya kusilikzwa wanafunzi hao lilitolewa tangazo likisema kwamba kila mwanafunzi ambaye hakuona jina lake katika orodha ya walioajiriwa anatakiwa kuandika barua ya kuomba ajira kwa kutumia anuani ya wizara hiyo na kuambatanisha vyeti vyake chuoni ili kuangaliwa upya. Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizarani hapo ilidaiwa kwamba utaratibu uliotumika wa kutoa ajira 9,000 pekee umetolewa na Wizara ya Utumishi kwamba wanafunzi wote waliofeli somo moja hadi manne hawatakiwi kuajiriwa hadi watakaporudia masomo hayo. Vile vile wanafunzi hao wanatakiwa kuomba kufundisha shule binafsi kwa kuwa muda wa kulipa ada ya kurudia masomo hayo umemalizika hadi hapo mwakani.

Juzi Dkt. Kawambwa alisema kuwa walimu 9,226 wamepatiwa ajira serikalini na miongoni mwao wamo wenye shahada 4,920 na stashahada 4,306 ambao wamepangwa kufundisha katika shule za sekondari na walimu 187 wamepangwa kufundisha katika vyuo vya ualimu.

No comments:

Post a Comment