01 February 2011

Mufti: Waislamu acheni kulalama, tafuteni elimu

Na Faida Muyomba, Geita

MUFTI wa Tanzania, Shekhe Mkuu Issa Shaban bin Simba amewataka waumini wa dini ya kiislamu nchini waache kubweteka na kutoa lawama kwa
serikali badala yake wajikite zaidi kwenye elimu ili kukomboa maisha yao.

Alisema hayo jana wakati akihutubia waumini wa dini hiyo mkoani Geita, ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye harambee ya ujenzi wa mabweni ya wasichana na bwalo katika Shule ya Sekondari ya Islam.

"Huu ni muda mwafaka kwa waislamu kuanza kujikita na kukazania zaidi suala la elimu, na si kubaki kulialia pekee kuomba kuchaguliwa na kupewa vyeo serikalini, hivyo tuchangamke tusiendelee kubaki nyuma tupige hatua kama wenzetu," alisema Mufti.

Alisema waumini wa dini hiyo nchini wako nyuma kwenye suala la kuwaandaa watoto wao katika elimu, jambo alilosema kuwekeza katika ujenzi wa misikiti pekee hakusaidii, kwani iko hatari ya misikiti hiyo kubaki kama maghala ya kutunzia vyakula.

Alisema mwislamu yoyote anayetaka kuwa mfuasi wa kweli wa dini hiyo  lazima ajikite katika elimu kwa sababu ndio mahali pazuri pa kuwekeza na si kwingineko.

Mufti pia alizungumzia namna ya kupata walimu wazuri, akisema huwezi kuwapata bila kulipa mishahara mizuri.

Katika harambee hiyo, jumla ya sh. milioni 17 zilipatikana ambapo Mufti Simba alichangia sh. milioni 5 na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Fillemon Shelutete,ambaye aliiwakilisha serikali alichangia sh. milioni 1.5.

Awali, Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Deusdedith Omchamba katika taarifa yake, alisema ujenzi huo ulibuniwa na waislamu wilayani humo mwaka 2007 baada ya kubaini kuwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wengi wao wakiwa wa wasichana hukosa nafasi za kujiunga na masomo ya sekondari.

Alisema ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana utagharimu sh.320,000,000 huku ule wa bwalo la chakula na jiko vitagharimu sh. 624,087,500.

Alisema shule hiyo ya mchanganyiko ambayo inatarajiwa kufunguliwa Februari 15, mwaka huu, hadi sasa imetumia sh 1,080,175,000 na kwamba hivi sasa wapo walimu watatu.

6 comments:

  1. Ni kweli elimu ni mhimu sana katika dunia ya leo.Mufti umetoa somo zuri waislamu wanatakiwa wazingatie elimu dunia maana ndiyo inayotawala kila kitu.Huwezi kusema namtumikia mungu wakti ujuzi huna wa kikidhi mahitaji yako.Huwezi kuwa na kazi nzuri bila Elimu na huwezi kumwabudu mungu wakati elimu huna. Nakupongeza sana Mufti kwa darasa zuri.

    ReplyDelete
  2. Mzee Simba ni vyema ukasema ukweli namna hii.
    Manake ukweli ni ukweli tu- elimu lazima itiliwe mkazo!!

    Pia tafuta wachangiaji wengiunapoakwenda kwenye shughuli kama hiyo ili michango inayopatikana ifanane na wadhifa wako. Mufti Kuchanga sh mil 17 kwa shule inayohitaji zaidi ya bilioni moja ni hatua ndogo sana na inaweza ikawakatisha tamaa wachangiaji wengine. Michango kama hiyo inatakiwa ianze kwa kishindo. Kuna waislamu wengi sana matajiri na wenye moyo wa kutoa - ni vyema mufti akawashirikisha watu akama hao

    ReplyDelete
  3. Mufti Umesema kweli kabisa. Si vizuri kukimbilia kusema kuwa wakristu wanapendelewa bila kujua kwa kiasi kikubwa wao wamewekeza kwenye elimu. Tusielemee kwenye madrasa tukasahau kuwapa watoto wetu elimu bora.

    ReplyDelete
  4. Mufti kwa hili tu nakubaliana na wewe asilimia 200. Waislamu tuache kulalamuka ovyo kwa lengo la kuonewa huruma. Muda unaotumika kuihifadhi kurani vifuani kwa watoto wa kiislamu na kusali mara tano kwa siku ndiyo muda na umri huohuo unaohitajika kuyaweka kifuani masomo ya hesabu, fizikia, kemia, geografia, kiswahili, historia, nk. Hivyo watoto na wazazi wa kiislamu tunakabiliwa na changamoto kubwa na elimu ahela na elimu dunia. Mtoto wa kiislamu lazima asaidiwe namna bora ya kumudu vyote viwili kwa pamoja, viginevyo tutakuwa walalamikaji kila siku. Idadi ya waislamu katika vyuo vyetu na vyuo vikuu vya umma na binafsi nchini ni ndogo sana na yakutisha, ufaulu wa watoto wa kiislamu ni mdogo sana. Mufti lazima uongoze mjadala kuhusu hili vivginevyo tutaendelea kuwa na marubani wapagani ama wakristo wa kutupeleka Hijja Maka Saud Arabia kila siku.

    ReplyDelete
  5. Aslam aleikum,
    Wewe Mufti wacha unafiki kwani umesikia Waislam hawataki kusoma! wanaowafelisha Waislam ni hao waokulipa mshahara Serikali.

    Kwanza tunataka kujua wewe ni Mufti wa Waislam au wa Serikali maana unaitetea Serikali ya kipagani ambayo wewe unatakia uipige au ndivyoulivyosoma kwenye vitabu vyako kuwa uwatii mapagani?

    Wacha unafiki kwani unafiki wako huna tofauti na Abdala ibn Salul.

    ReplyDelete
  6. Ukisoma historia ya u-Islam utaona kuwa tangu mwanzo u-Islam ulikuwa unahimiza elimu katika taaluma mbali mbali. Mtume Muhammad alikuwa mhimizaji mkubwa wa elimu. Someni historia hiyo na mtaona kuwa anayohauri Mufti Simba ni sahihi kabisa, tena si kwa wa-Islamu tu bali kwetu sote.

    ReplyDelete