Na Mwandishi Wetu
MJI Mkongwe wa Zanzibar utaendelea kuwa urithi wa ulimwengu na Mamlaka ya Uendelezaji Mji huo, imesema hakuna tishio lolote la kufutwa kama
inavyodaiwa na watu wasiovitakia mema visiwa hivyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamalaka hiyo, Bw. Issa Sarboko Makarani alisema Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sanyansi na Utamaduni limeukubali Mji Mkongwe wa Zanzibar kuwa urithi wa ulimwengu baada ya kuridhika na uhifadhi wake, na umakini wa mamlaka hiyo katika kusimamia sheria za urithi.
"Kama SMZ ingekuwa inakiuka sheria za UNESCO hivi leo Mji huu usingekuwa kama ulivyo sasa, hao wanaosema hawajui, mamlaka yangu ina watendaji makini na mahiri katika kusimamia taratibu, kila kitu sisi tunafanya kulingana na taratibu na sheria," alisema Mkurugenzi Mkuu huyo.
Bw. Sarboko alisema kulingana na taratibu, yapo majengo ambayo huwezi kuyabadilisha sura yake ambayo hayo ni ya daraja la A, yapo pia daraja B ambayo unaweza kufanya marekebisho kidogo na yale ya daraja la C yanayoruhusu kufanya marekebisho.
Vigezo hivyo vinaratibiwa na mamlaka hiyo hivyo si rahisi kwa mtu yeyote ndani ya Mji Mkongwe kufanya mambo anavyotaka.
"Wanaweza kutazama tovuti ya UNESCO wataona nchi ambazo zimo katika hatari ya kufutwa katika urithi wa ulimwengu, lakini sio Zanzibar. Hata huo ujumbe unaokuja hauji kwa sababu Zanzibar imekiuka taratibu la hasha," alisema mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo alisema kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ndio sehemu za kihistoria zilizoorodheshwa na UNESCO katika hatari ya kufutwa katika urithi wa ulimwengu, lakini sio Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Sakata la upotoshaji wa Mji Mkongwe limekuja baada ya SMZ kukodisha majengo ya Mambo Msiige kwa Kempinski, ambayo ujenzi wake utafuata vigezo na masharti ya UNESCO katika uhifadhi wa Mji huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji Mkongwe alisema mwekezaji Kempinski ametakiwa kulifanyia ukarabati jengo la Mambo Msiige kuliweka katika haiba yake kulingana na maelekezo ya UNESCO, ambayo tayari mwekezaji huyo ameyazingatia.
Alisema ujumbe wa UNESCO unatarajiwa kutembelea Zanzibar mwezi ujao ikiwa ni sehemu ya taratibu ya shirika hilo kutembelea sehemu mbalimbali za miji ya urithi wa ulimwengu na sio kwa sababu ya ujenzi wa Kempinski.
Waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya sita ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema uamuzi uliofanywa wa kumkodiosha Kempinski ni kuyanusuru majengo hayo kuanguka, lakini pia ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nyumba na maagizo mengine ya SMZ.
"Unajua si kila jambo lazima lijadiliwe katika Baraza la Mawaziri, suala la kukodishwa nyumba za serikali limeelezwa kwa kina katika Sera ya Taifa ya Nyumba na hata michango ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika vikao tofauti wamelieleza kwa kina suala hilo," alisema waziri huyo.
Ufaransa imelifanyia matengenezo makubwa jengo la kihistoria Kasri la Mfalme Napoleon ambapo matengenezo yake yanafanana na yale yanayokusudiwa kufanywa na Kempinski katika jengo la Mambo Msiige. Mbali na nchi hiyo, Msumbiji nayo ikiwa ni sehemu ya urithi wa ulimwengu Mji wenye majengo ya kihistoria kama San Sebastian Fortress yamefanyiwa ukarabati mkubwa.
Tatizo ni umbeya ya media, haswa IPP! Ni kawaida kabaisa kwa ardhi kukodishwa kwa miaka 100 hadi 150, si jambo geni! tatizo hapa ni huyu His Highness Aghakhan anayetaka kutawa ulimwengu alipoona amekosa hilo eneo akanzihsa hoja zake za chuki binafsi dhidi ya kempinski
ReplyDelete