25 January 2011

Yanga yaendeleza shangwe Jangwani

*Mwape aibuka shujaa tena

Na Zahoro Mlanzi

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana iliendeleza shangwe za ushindi huku ikiongeza wigo wa pointi nne kwa wapinzani wao wa jadi Simba, Baada
ya kuifunga Polisi Tanzania mabao 2-0.

Kwa ushindi huo wa jana uliopatikana katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Yanga sasa imejikita zaidi kileleni mwa ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 31 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 27, huku Azam FC ikikamata nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 23.

Katika pambano hilo, Yanga ilipata bao la kwanza ya dakika ya 45 lililofungwa na Mzambia, Davies Mwape kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari, baada ya kupokea pasi ya Shadrack Nsajigwa.

Awali kabla ya bao hilo la Mwape ambaye jana aliibuka shujaa kwa kufunga mabao hayo, Idd Mbaga wa Yanga dakika ya 25 nusura aipatie timu yake bao baada ya kuunganisha krosi ya Nsajigwa kwa kichwa lakini mpira ukatoka nje ya lango.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa nguvu ambapo, Polisi ilijaribu kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga, lakini hata hivyo washambuliaji wake walishindwa kupenyeza mpira wavuni.

Baada ya mashambulizi hayo, Yanga iligeuza kibao na kuliandama lango la Polisi ambapo Nsa Job alikosa bao la wazi baada ya kuinasa pasi ya Nurdin Bakari kwa kupiga shuti lililotoka nje.

Dakika ya 68 mchezaji, Delta Thomas wa Polisi alitolewa nje kwa machela baada ya kuanguka vibaya wakati akiwa katika harakati za kuokoa akiwa na Jeryson Tegete.

Yanga iliongeza bao la pili dakika ya 80 lililofungwa tena na Mwape kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari, baada ya kupokea pasi ya Tegete. Bao hilo likiwa la tano kwake kwenye ligi hiyo.

Mwape ambaye jana ilikuwa mechi yake ya pili tangu kusajiliwa Yanga katika usajili wa dirisha dogo kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya AFC ambayo timu yake ilishinda mabao 6-1, alipachika mabao matatu.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic alisema hatma yake ya kuendelea kuinoa timu hiyo itajulikana leo baada ya kukutana na viongozi wake.

"Sina la kuongea zaidi na kwamba sina tatizo na Fredy Felix 'Minziro' kama mlivyomuona kwenye benchi, ila kwa sasa kuna vitu natakiwa kuviweka sawa na viongozi, hivyo kesho (leo) nitawapa hali halisi," alisema Papic.

No comments:

Post a Comment