25 January 2011

Chadema yamuunga mkono Kafulila

*Ni kuhusu hoja ya Dowans kurejeshwa bungeni
*Lissu asema lengo kupinga kuzawadia ufisadi


Na Jumbe Ismailly, Singida 

HOJA Binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), Bw. David Kafulila
imeungwa mkono na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kupinga kile walichodai ni hatua ya 'kuzawadia ufisadi.'

Hoja hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa pili wa bunge la 10 utakaoanza Februari 8, mwaka huu, inahusu mgawo wa umeme ikilenga kuliomba bunge liazimie kumtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ajiuzulu na kupinga kuilipa kampuni tata ya Dowans sh bilioni 94 bila suala hilo kurejea bungeni.

Lakini Bw. Kafulila, tayari ameonya kuwa iwapo serikali itafikia uamuzi wa kuilipa Dowans haraka, kabla ya mkutano wa bunge kama alivyonukuliwa Bw. Ngeleja akisema, wigo wa hoja yake utapanuka na ataliomba bunge, kadri litakavyoona, lipige kura ya kutokuwa na imani na serikali yote.

Msimamo wa CHADEMA kumuunga mkono Bw. Kafulila umetolewa na Mnazimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw. Tundu Lissu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida.

Bw. Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA), alisema kuwa ni wazi kwamba Watanzania wengi hawakubali kuona nchi yao maskini ikilipa sh. bilioni 94 kwa kampuni ambayo wenyewe hawajulikani, iliyoingia mkataba kwa njia zinazonuka rushwa.

Aliongeza kuwa kuilipa itakuwa ni sawa na kuamua kuuzawadia ufisadi badala ya kuuadhibu.

"Kuhusiana na suala la Dowans ni wazi kabisa kwamba Watanzania hawakubali nchi hii maskini ilipe sh. bilioni 94 kwa kampuni ambayo wenyewe hawajulikani, iliingia kwa njia zinazonuka rushwa rushwa na kwa hiyo kuwalipa itakuwa ni kuzawadia ufisadi badala ya kuadhibu ufisadi," alisema Bw. Lissu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

"Sasa hili suala la Dowans lazima vile vile tukalizungumzie bungeni, nafahamu kwamba Mbunge wa Kigoma Kusini, mheshimiwa David Kafulila ametoa taarifa kwamba atapeleka hoja mahsusi bungeni kuhusu hili suala la Dowans," alisema Mbunge huyo wa CHADEMA.

Kwa mujibu wa Lissu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa CHADEMA, yeye pamoja na wenzake siyo tu watamuunga mkono katika hoja hiyo, kwa sababu ina maslahi makubwa kwa wananchi wengi, bali pia watataka nyaraka zote zinazohusu Dowans, ilivyoingia, wamiliki wake na mkataba wake viletwe bungeni ili viweze kujadiliwa huko.

"Tutataka nyaraka zote zinazohusu hiyo kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO na serikali ya Tanzania ziletwe vile vile bungeni ili wabunge wajiridhishe kwamba kilichofanyika ni kisafi, tufahamu wenye Dowans ni akina nani, mawakala wao Tanzania ni kina nani...

"...Ofisi zao ziko wapi, huo mkataba walioingia na Richmond na baadaye TANESCO una uhalali gani, kesi walioipeleka dhidi ya TANESCO serikali ya Tanzania ilikuwa inadai nini, majibu ya utetezi wa TANESCO na serikali yalisemaje, majibu yaliyotolewa mpaka tukashindwa kesi yakoje," alisema mbunge huyo.

Hata hivyo, Bw. Lissu aliweka bayana kuwa baada ya kupokea taarifa zote hizo ndipo wataangalia kama hawauzawadii ufisadi na kuonya kuwa endapo bunge litaridhika kwamba kilichotokea ni 'uharamia', watalazimika kuchukua hatua za kuwaeleza Watanzania wasikubali malipo ya Dowans.

"Kwa sababu kama ambavyo tumezungumza siku nyingi sisi viongozi wa CHADEMA, chama chetu hatuko tayari kunyamazia ufisadi katika nchi hii kwa hiyo Dowans hatutainyamazia," alisisitiza Bw. Lissu.

Tangu kuibuka kwake 'upya' baada ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), mjadala wa Dowans umeshika kasi katika duru za siasa za Tanzania, ukichukua sura mpya karibu kila siku na kujiongezea wazungumzaji wengi waliogawanyika katika makundi mawili, yenye hoja mbalimbali.

Kundi moja linaloonekana kupinga hukumu hiyo na hatua ya serikali kutaka kuwalipa Dowans sh. bilioni 94 kama ilivyoamuriwa na ICC limekuwa likihoji uharaka unaooneshwa na mamlaka husika kulipa tuzo hiyo. Pia limehoji sababu za serikali kutotaka kutumia 'mianya' iliyopo kuweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Kundi hilo linalowajumuisha wananchi wa kawaida, wanazuoni wa masuala mbalimbali kama vile utawala bora na sheria, viongozi waandamizi serikalini, wanaharakati, viongozi wastaafu na vyama vya siasa vya upinzani, wamekuwa wakihoji pia uhalali wa mkataba wa Dowans, uliorithiwa kutoka Richmond, ambayo tayari ilishaelezwa kuwa ni kampuni hewa.

Lakini pia limekuwa likihitaji wale wote waliohusika kuifikisha nchi katika hali hiyo, kupitia katika mkataba wa Richmond na TANESCO, kisha Dowans na TANESCO wachukuliwe hatua stahili za kinidhamu na kisheria.

Wengine wamekuwa wakihitaji hoja hiyo irudishwe bungeni, ili kama kuna ukweli ambao haujulikani mpaka sasa, ukaweze kuelezwa ikiwemo viongozi wa kisiasa kujiuzulu au serikali nzima kuangushwa. Tayari Bw. Kafulila ameshasema kuwa suala la Dowans litaipotezea serikali uhalali wa kisiasa kutawala machoni mwa wananchi.

Kundi jingine likihusisha watu wenye sifa kama wa kundi la kwanza (kikiwemo Chama Cha Mapinduzi), limekuwa likiunga mkono serikali kuilipa Dowans, likisema kuwa suala hilo ni uamuzi wa kisheria.

Wengine wamenukuliwa wakisema kuwa iwapo serikali itakiuka, itakuwa inajipalia 'mkaa', kuwa nchi inaweza kuwekewa vikwazo na hata mali zake nje ya nchi kukamatwa.

Mbali ya kusema kuwa serikali haiwezi kukata rufaa kupinga uamuzi wa ICC, limekuwa likisema kuwa mamlaka zinazohusika kulipa tuzo hiyo hazina njia yoyote ya kukwepa malipo hayo, bali kukabiliana na hukumu hiyoo, kisha ijifunze kwa ajili ya siku za usoni.

8 comments:

  1. wote hamna akili huyo muha mtumwa wetu mnamuunga mkono basi wote wendawazinu

    ReplyDelete
  2. wewe ndo huna akili wala uchungu na taifa lako, watu wanatetea maslah ya nchi unasema hawana akili tena ukatubu mbele za Mungu mana lazima utakuwa miongoni mwa watu wanaonufaika no huyo dudumtu dowans. inamana ulitaka asiungwe mkono ili hoja ipotezewe! safi sana chadema keep it up! msirudi nyuma teteeni maslahi ya hii nchi Mungu atawalipa, pia nawaomba sana mjiunge na wapinzani wenzenu bungeni ili muikosoe vizuri serikali, naamini mtafanya hivyo mana toka mwanzo mlionyesha nia ila Cuf wakagoma but naamini yamepita madamu wamekubali wote washirikeshen! binafsi nafurahi sana kuona kuwa kwa sasa wapinzani wamekuwa kitu kimwoja coz mara ya kwanza ilikuwa chadema kama mnatengwa, nachowasihi msiangalie ya nyuma unganeni muunde kambi moja, mpaka kieleweke mtanzanie akombolewe kutoka kwa mkoloni mweusi.

    Amina Juma.
    Morogoro

    ReplyDelete
  3. Wanasiasa suala hili lisiwe la kisiasa kwa sababu ni la kisheria,mkiwa mko na taratibu hizo pia muwahi mahakamani kuzuia malipo,mkiitia sana siasa basi litakuwa la kisiasa zaidi kuliko utekelezaji,na vyema ccm na serikali yake ili mpate heshima wekeni mambo yote wazi na hizo nyaraka zinazotakiwa ziende bungeni,hii nchi ni yetu sote. na nyie wajinga mnaotukanana hata kwenye kujadili jambo la faida kwa nchi hamna budi kufikiria mara mbili tatu kwani matusi yako hayasaidii zaidi ya kueneza chuki.

    ReplyDelete
  4. kama ccm inapenda kuendelea kuongoza hii nchi hadi mwaka 2015, waepuke kuilipa dowans (mafisadi). vinginevyo tunawatakia wakalale pema peponi baada ya malipo hayo.

    ReplyDelete
  5. Naunga Mkono Hoja, wananchi wote wa Tanzania Tusimame imara katika kutetea nchi yetu, jamani tujaribu kuwaelewesha hata wale wasio na uelewa juu ya nchi inakokwenda. Together we can make, together we stand. Kamwe tusiwaachie Mafisadi kumaliza nchi yetu.

    NB: Achaneni na huyo aliyetoa comment ya kwanza, mambo ya mtandao ni makubwa huwezi kujua inawezeka ni fisadi mwenyewe, au mwanaye, tatizo letu tunafikiri yeye ni mwanachi kama sisi, nauhakika huyo lazima ni mnufaika wa ufisadi.

    Keep it up. SAFI sana Wabunge wetu.

    ReplyDelete
  6. Watz tuamke tutetee masilahi ya taifa hili. Hakuna mtu asiye mtz atakayekuja kutetea ustawi wa taifa hili lililo na utajiri wa kila kitu lakini watu wachache wanalifilisi. Hawa wajanja wachache tuwapinge kwa nguvu zote. Tuhamasishane wenyewe kwa wenyewe kwani tumeshawajua wabaya wetu. Ukishamjua adui, umeshinda nusu ya vita. Tusikubali kuburuzwa na watu wenye uchu wa utajiri hata kwa kuuza nchi. Hivi vidowans ni vingi mno ukienda ttcl, kipo kidowans kilichoanzisha kampuni ya celtel, kisha ikauzwa na kuitwa zain na sasa wanajiita airtel. Fedha zilizoanzisha celtel ni kodi za wanachi lakini sasa airtel si mali ya watz. Mmeona huo ujanja wa viongozi wetu? Hawafai. Tunatakiwa kuwawajibisha sasa. Wametuonea vya kutosha. Imetosha, tuseme basi.

    Nchi hii ina vyanzo vingi vya maji. Sisi hatukuwa watu wa kutegemea umeme wa majenereta lakini kwa vile serikali ilishakamatwa na wafanyabiashara na kwa kuwa lengo la mfanyabiashara yeyeto ni kupata faida, hawakuwekeza kwenye umeme wa maji, bali waliishia umeme wa dharura ambao ni dili.

    Jingine tuwaulize ile ndege ya rais iko wapi? Mrambaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa? Tulikula nyasi na bado tuanaendelea kula nyasi hadi leo. Tuambie ile ndege uliyonunua iko wapi? Hiki ni kidowan kingine ! Watz amkeni!Nasikia kuna wanaokuja kuwekeza kwenye umeme wa upepo. Kinaweza kuwa kijukuu cha dowans.

    Nchi inaingia mikataba ya ajabu utafikiri hakuna aliyekwenda shule. Wakati mkataba wa dowans unavunjwa, mwanAsheria mkuu wa serikali alishauri nini? maana amekuwa wa kwanza kusema malipo ya dowans hayakwepeki.

    Angalia ya rada, nashindwa kuendelea maana kompyuta yangu inajaa machozi. Ee Mungu sikia kilio cha watoto wako. Tunateseka baba, wengine wanstarehe kana kwamba umeshawaita huko ulioko. Mungu ibariki Tanzania. Amen.

    ReplyDelete
  7. mtoa maoni wa 1 ni kizazi cha fisadi,anaona kula yake inafika ukingoni,labda yeye kizazi cha richmond na dowans,hataki watu wapinge, sasa ajue bunge ndo hilo litapinga ndo atajua kweli wabunge ndo mwisho wa lami brbr hadi kigoma mwisho wa lami!!!!!!!!!!!!!!!!!!!hatudanganyiki tumezinduka..............hongereni kafulila , tisu na wengine

    ReplyDelete
  8. HIZI SIO SEHEMU ZA MATUSI NA KEJELI WANANCHI WENZANGU. TUZITUMIE IPASAVYO KUIKOMBOA NCHI YETU. TUSIJALI UPANDE MMOJA AU KUWA WABINAFSI. TUANGALIE HALI YA MWANANCHI WA KAWAIDA ITAKOMBOLEWAJE. KWA MAONI YANGU NJIA PEKEE NI KUTOKA MTAANI NA KUDAI HAKI ZETU. HAKUNA TUME WALA MUAFAKA WALA VIKAO VINAVYOWEZA KUMLETEA MWANANCHI WA CHINI MAISHA BORA. PEOPLE'S POWER..

    ReplyDelete