25 January 2011

Madiwani wapanga kumwengua meya

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

BAADHI ya madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa ya Shinyanga wanadaiwa kula njama za kutaka kumuengua Meya wao
, Bw. Gulam Mukadam wakimtuhumu kwa kosa la kubadili kinyemela wajumbe wa kamati za kudumu.

Imedaiwa kuwa kutokana na maamuzi yake hayo, madiwani hao hivi sasa wanajiandaa kupiga kura za kutokuwa na imani naye katika kikao kijacho cha baraza kinachotarajiwa kufanyika Januari 29, mwaka huu ambapo kura hiyo ikifanikiwa meya huyo ataondolewa katika wadhifa huo.

Kwa mujibu wa habari za uhakika zilivyolifikia gazeti hili mjini hapa, hatua hiyo ya madiwani wa CCM inatokana na kuenguliwa kwa baadhi ya wajumbe wawili (majina yao tunayo) katika kamati za ardhi na ile ya miundombinu, uamuzi ambao unadaiwa
kuwaudhi madiwani husika.

Imedaiwa kuwa ili hatua hiyo iweze kufanikiwa tayari baadhi ya madiwani hao wameanza kukutana na wenzao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa lengo la  kuwaomba wawaunge mkono katika kusudio lao hilo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mstahiki Meya Gulam Mukadam alisema hakuwa na taarifa juu ya kusudio hilo lakini pia alikiri kufanya
mabadiliko katika baadhi ya wajumbe wa kamati ndogo kwa kuzingatia kanuni za manispaa.

“Kwa kweli sina taarifa kama wenzangu wemepanga njama za kutaka kunikataa kwa njia ya kunipigia kura za kutokuwa na imani na mimi, lakini ukweli ni kwamba nilichokifanya ni kwa mujibu wa kanuni zetu za Manispaa.

“Tumelazimika kufanya mabadiliko katika baadhi ya kamati zetu ndogo hii ni baada ya kubaini kufanyika kwa makosa wakati tulipokuwa tukiwateua wajumbe wa kamati hizo, kamati ya ardhi ina wajumbe wawili, lakini ni lazima suala la jinsia lizingatiwe.

“Awali sisi hilo hatukuliona, tuliweka wajumbe wanaume pekee, ilibidi tubadili, maana tungepeleka majina ya wanaume watupu kwa waziri angetushangaa, lakini pamoja na kumbadili huyu diwani (anamtaja jina) bado nilimfuata na kumuomba radhi, na
nilimweleza sababu iliyosababisha tumbadilishe,” alieleza Bw. Mukadam.

Alisema mabadiliko ya diwani mwingine katika kamati ya miundombinu yalitokana na umuhimu wa kamati hiyo kwa vile mambo mengi yanahitaji watu wasomi ambapo pia naye alielezwa kuhusiana na mabadiliko hayo akakubali.

“Kwa kweli nitashangaa kama hawa wenzangu watachukua uamuzi huo, itakuwa ni aibu kwa
CCM maana kikao kijacho ndiyo kitakuwa kikao chetu cha kwanza cha kufanya kazi, leo wananchi wakisikia tumeanza na malumbano watatushangaa hawatatuelewa,” alieleza Bw. Mukadam.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Bw. Festo Kang’ombe alisema hakuna taratibu zilizokiukwa katika uteuzi wa wajumbe wa kamati za kudumu katika
manispaa yake na kwamba kila diwani anapaswa kuwa katika moja ya kamati za kudumu na siyo kwa kamati ndogo.

“Ni kweli kuna mabadiliko madogo yamefanyika, na hii ni kwa mujibu wa kanuni za manispaa, meya anayo fursa kwa mujibu wa kanuni hizo kuchagua diwani gani awe kwenye kamati ipi, lakini kila diwani ni lazima awe katika katika moja ya kamati za kudumu,” alieleza Bw. Kang’ombe.

Baadhi ya wanachama wa CCM waliozungumza na Majira
jana wameelezea kushitushwa kwao na hatua hiyo ambapo wamedai inachangiwa na hali ya kutokuelewana kutokana na makovu ya uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Mapema wiki iliyopita mmoja wa wenyeviti wa kata wa CCM, Bi. Rehema Nhamanilo alilazimika kujitoa kwenye chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na tuhuma zilizokuwa zikitolewa juu yake na wana-CCM wenzake akidaiwa kukihujumu wakati wa uchaguzi.

3 comments:

  1. HIYO NDIYO CCM SHINYANGA WAACHE UNAFIKI KWANI KIONGOZI WAO WA MKOA BW MGEJA NI BONGO LALA SASA WANALALAMIKA NINI WANAPENDA KUSHUJUDIA WATU WENYE FEDHA ASILI YA KIASIA SASA WANALIA NINI IGENI MFANO WA SHIBUDA MSUKUMA MJANJA KULIKO WOTE,SHAURI YENU

    ReplyDelete
  2. CCM IMEINGIA WAZIMU,MTU AKIONDOLEWA KWENYE WADHIFA BASI NI BALAA YUKO TAYARI KUHUJUMU CHAMA CHAKE,HII INATOKANA NA KUTOKUWA MAKINI SAA YA KUTEUA KIONGOZI,HAMUANGALII YUKO KWENYE CHAMA KWA AJILI YA KUKIPENDA CHAMA NA SERA ZAKE AU KAFATA MLO,MNA KAZI KUBWA KUIONDOA HALI HII MAANA MMEILEA KWA MIAKA MINGI

    ReplyDelete
  3. Mnataka katiba mpya na hii ya zamani inasema usimbague mtu kutokana na rangi yake,kabila lake,dini yake au jinsia yoyote ile sasa sijui hii mpya mtaiandikaje maana mhindi akifanya jambo tayari mnamsema mhindi huyo,laana ya ubaguzi haiishii hapo,si tayari umemtaja msukuma hapo kesho itakapofika utasema mhaya hatufai hapa. mkataeni na Sabodo anayetoa pesa kwa chadema kwa sababu ni mhindi.

    ReplyDelete