21 December 2010

Utitiri wa makanisa kuzua balaa

Na Anneth Kagenda

UTITIRI wa makanisa nchini umesababisha baadhi ya viongozi wa dini kuanza kutofautiana huku kila mmoja akijitahidi kuvutia kwake na kushawishi wananchi kusali kwenye kanisa lake jambo ambalo badae linaweza kuleta madhara makubwa.Hayo
yalisemwa Dar es Salaam jana na Profesa. Emmanuel Bava wakati wa mahafari ya kwanza ya Chuo cha dini cha Zoe Institute of Apostolic Testimony yaliyofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa.

Alisema kuwa kumekuwepo na utitili wa makanisa pamoja na ushindani mkubwa wa kila mtu kutaka kuanzisha kanisa la kwake huku wengine wakidai wanaongozwa na roho mtakatifu wakati roho huyo alitaka kanisa moja na muunganiko wa pamoja tofauti na hali ilivyo sasa.

"Haya yote yanasababishwa na utandawazi uliojitokeza ambao unachangiwa na kasi ya maendeleo nchini hivyo kusababisha kuleta athari nyingi kwa wananchi," alisema Prof. Bavo.

Alisema kuwa kuna tatizo la maadili na ambalo linatokana na kasi kutoka nchi za nje na pia tatizo hilo linawakumba vijana ambao hukosa mwelekeo na kuvamia vitu ambavyo hata hawavielewi likiwamo la kufikilia kuanzisha makanisa na kuwashawishi watu kujiunga huko.

"Wahitimu lazima muwasaidie watu mnaowaongoza na kuhakikisha maadili yanarudi ikiwa ni pamoja na kusoma biblia na kuelewa neno la Mungu na kujua Roho Mtakatifu alitaka nini na siyo kila mtu anajiamulia kile anachokitaka," alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Cho Bw. John Mwakilema alisema kuwa kuna tatizo kubwa la watanzania kutojiamini jambo linalosababisha wengine kushindwa kujiunga na vyuo mbalimbali vinavyotoa mafunzo.

"Umefika wakati watanzania kujiamini na kujiunga kwenye vyuo mbalimbali nje na ndani ya nchi lakini hivi sasa hatutakuwa na mzigo mkubwa kwenda nje badala yake tutakuwa tunapata mafunzo kwenye chuo chetu kilichopo hapa Tanzania ambacho wanafunzi wa kwanza ndio hawa waliohitimu," alisema Bw. Mwakilema.

Alisema kuwa Tanzania na waumini wote kwa ujumla hivi sasa hawahitaji wachungaji mbumbumbu na kusema kuwa wanatakiwa kuamka na kufanya yale yanayompendeza Mungu ikiwa ni pamoja na kukemea maovu ambayo mwisho wake unaweza kuwa mbaya zaidi.

Wahitimu waliohitimu ni zaidi ya 65, ambao walipata mafunzo ya uandishi wa habari, shahada ya mambo ya kanisa, ushauri, heshima, pamoja na usimamizi katika maeneo mbalimbali ambapo walikuwa ni mchanganyiko wa makanisa.

No comments:

Post a Comment