Na Florah Temba, Moshi
WATU watatu akiwemo Askari Polisi F.3486 PC Jakson Deodatus wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Kilimanjaro wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za uporaji wa sh. milion 7.6 mali ya Kampuni ya Machare Investment.Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi mkoani humo, Bw. Lucas Ng’hoboko alisema tukio hilo la uporaji lilitokea Jumamosi Disemba 18, mwaka huu saa 4.30 asubuhi katika eneo la Benki ya NBC tawi la Kibo Moshi wakati karani wa kampuni hiyo Bi. Caroline Ibrahim (28) akielekea kwenye mlango wa Benki.
"Wakati karani huyo akielekea mlangoni ghafla aliporwa mfuko uliokuwa na fedha na mtu mmoja na kuanza kukimbia lakini mama huyo alikamata koti la mwizi huyo na kuling'ang'ania huku akipiga kelele," alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alikimbilia eneo ambalo liliegeshwa pikipiki ambapo wananchi waliokuwa jirani walijitokeza na kutoa msaada kwa kumdhibiti mtuhumiwa huyo kabla ya kupanda kwenye pikipiki hiyo.
Hata hivyo, askari wa doria walifika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada ambapo walifanikiwa kuokoa fedha zilizoporwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Nghoboko uchunguzi wa awali umeonesha kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa ametambulika kwa jina la Ezekiel Kivuyo (28) mkazi wa Arusha ambaye alishirikiana na askari polisi na ndiye aliyeitelekeza piki piki eneo la tukio na kukimbia.
Kamanda alisema imebainika kuwa pikipiki hiyo ni mali ya Sifael Peter Mkoma (23) fundi pikipiki mkazi wa Pasua mjini Moshi ambaye hata yeye anashikiliwa kwa kosa la kuhusika katika uporaji huo.Kutokana na hayo, Kamanda aliwataka askari polisi kulinda maadili ya kazi zao na endapo watashindwa kufanya hivyo ni bora waondoke kwenye jeshi hilo mapema kabla hawajabainika.
“Ni vyema kama kuna askari polisi ambaye anahitaji kuwa jambazi akaondoka kwenda kufanya kazi hiyo na sisi tutapambana naye huko uraiani kuliko kuendelea kujificha kwenye mavazi ya jeshi huku wakiwa na malengo mengine," alisema.
No comments:
Post a Comment