21 December 2010

Serikali ilaani vurugu Ivory Coast-CHADEMA

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeitaka Serikali ya Tanzania kulaani hadharani matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia unaofanywa na Bw. Laurent Gbagbo na wafuasi wake
nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Bw. John Mnyika, Rais Kikwete ametakiwa kutamka hadharani kumtambua Bw. Alassane Ouattara kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais katika nchi hiyo.

"Inashangaza kwamba wakati Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na serikali za nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika zimetoa matamko ya wazi serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya diplomasia ya kimya.

"Hii ni tofauti kabisa na wakati Mwalimu Nyerere ambapo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele na kutoa misimamo ya wazi ya kukemea vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora," alisema Bw. Mnyika.

Bw. Mnyika alisema kurugenzi hiyo inatambua kwamba Rais Kikwete alizungumzia kidogo matatizo ya Ivory Coast wakati akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Amani katika eneo la Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika hivi karibuni nchini Zambia, kwamba suala hilo linashughulikiwa na mikono salama na akaonyesha matumaini yake kwamba pande mbili zenye mgogoro zitafikia makubaliano.

"Kauli hii ya Rais Kikwete inalea vitendo vya ukiukwaji wa misingi ya demokrasia vinavyofanywa na Laurent Gbagbo na wafuasi wake kwa kuwa inatoa fursa kwa mgombea ambaye taasisi zote huru zimetamka kuwa ameshindwa katika uchaguzi, kuanza majadiliano na aliyeshinda badala ya kumpisha katika uongozi wa nchi," alisisitiza.

Iliongeza kuwa serikali ya Tanzania inapaswa kuweka wazi msimamo wake ili kuondoa mashaka kwamba ukimya wake unatokana na Rais Kikwete kukosa uhalali wa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa demokrasia na mchakato wa uchaguzi uliomuingiza madarakani kuhojiwa kutokana na tuhuma za matokeo 'kuchakachuliwa' katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Ilisema kuwa kurugenzi hiyo inapinga kauli ya Rais Kikwete kuwa mgogoro wa Ivory Coast 'uko katika mikono salama' wakati kumefanyika mauji ya raia wasio na hatia siku chache zilizopita na sasa wanajeshi wanaomuunga mkono Bw. Gbagbo wamewazingira wafuasi wa Bw. Ouattara katika Hotel Golf, katika Jiji la Abijan na kukwaza shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) ndani ya nchi hiyo.

"Serikali ya Tanzania inapaswa kufanya kazi kwa niaba ya wananchi, na msimamo wa raia wa Tanzania unafahamika bayana kwamba wengi hawakubaliani na viongozi kuingia madarakani wa chaguzi zisizo huru na haki. Tunatarajia kwamba Tanzania itaungana na wapenda demokrasia wengine wanaotoa mwito kwa Gbagbo kuwekewa vikwazo mbalimbali," alisisitiza.

3 comments:

  1. ... kuna tofauti gani kati ya Kikwete na Gbagbo?

    ReplyDelete
  2. Hawezi kulaani kwani hana tofauti na Gbagbo, Gbagbo kachakachua vibaya halafu akachelewa kuapishwa, JK alichakachua akawahi kuapishwa na bado anaendelea kuchakachua mpaka mameya. Watanzania ni wavumilivu wangekuwa Ivory Cost au Kenya hapa tungekuwa tunaongea mengine. Hakuna tofauti kati ya kilichotokea Ivory cost na Tanzania. Habari ndo hiyo.

    ReplyDelete
  3. Chadema acheni kutuzengua. Kumlinganisha Gbagbo na Kikwete, give me a break. Ivory cost wasimamizi wote wanasema Gbagbo hakushinda uchaguzi, wakati Tanzania ni Chadema tu wanaodai wizi wa kura. Wasimamizi wote hakuna anaungamkono madai ya chadema. Waliambiwa wachapishe matokeo ya urais waliyonayo kama walivyodai lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo. Juzi juzi wametangaza kumtambua Kikwete sasa huo wizi umeishia wapi? Kama slaa alishinda na kuibiwa kura zote hizo na kusababisha Kikwete kupata 61% tume itakuwa imefanya kazi sana. Kumbukeni Gbagbo na mpinzani wake tofauti ilikuwa ndogo sana. Tafadhali chadema msituchafulie hali ya hewa, jipangeni vizuri 2015, huu uchaguzi mmeshindwa. Mkiendelea na uanasesere huu watanzania watawanyima kura 2015, hata kama katiba itabadilika. Angalia mmeshindwa kuongoza maridhiano bungeni, mmeshindwa kuongoza serikali ya upinzania bungeni sasa mngewezaje kuongoza serikali ya kweli? Kama mna ushahidi wa kikwete kuiba kura utoeni au fyata mkia msubiri 2015. TUMECHOKA NA KELELE ZENU. AU imelaani kilichotokea Ivory Cost, na kutangaza kuwa mpinzani wa Gbagbo ndiye mshindi, na Kikwete alikuwa kwenye huo mkutano wa AU, sasa mnataka aseme nini zaidi? Chadema mnaprove watanzania walikuwa sawa kuwanyima kura, kama hivi ndivyomngeongoza nchi.

    ReplyDelete